Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisesa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUSA G. MBUGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi hii uliyonipa kuongea kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo la Kisesa, nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii. Ninampongeza Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega, kaka yangu sana pamoja na Naibu wake Engineer Godfrey Kasekenya huyu ni zaidi ya encyclopedia, hii ni encyclopedia inayotembea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Katibu Mkuu, Balozi Engineer Aisha, ninampongeza Naibu Katibu Mkuu Dkt. Charles Msonde, ninampongeza pia Meneja wangu wa Mkoa wa Simiyu Engineer Boniface Mkumbo. Nami ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, tumetembelea miradi mingi ya TBA, ninaomba nimpongeze sana Kiongozi Mkuu DG wa TBA pamoja na taasisi nyingine ambazo ziko chini ya Wizara ya Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda sitaweza kuongelea kazi za TBA na mengine, naomba nijielekeze kwenye upande wa barabara. Ninashukuru Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha ambazo zimekuja Jimboni Kisesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya ufinyu wa muda nijikite kwenye changamoto zilizopo Kisesa. Ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, kuna changamoto kubwa sana ya barabara inayotoka Maswa inakuja mpaka Mwabusalu inaenda Mwandoya inaenda mpaka Sakasaka. Barabara hii ina hali mbaya. Ninaomba atakapokuwa anafanya majumuisho aeleze mkakati ambao alionao pamoja na viongozi wengine walio chini yake kwenye hii barabara inayotoka Mwabusalu mpaka Sakasaka, hali ni mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ninapongeza na ninatoa shukrani, nimeangalia kwenye randama nimeiona barabara ambayo inatuunganisha na Singida pamoja na Simiyu, ninaipongeza sana Serikali, Wizara hata tu kwa huu utayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa imeshatengewa fedha ninakuomba ndugu yangu hii Barabara ya kutoka Singida kuja Sibiti kuja Mwanhuzi inakuja mpaka Ng’oboko, Mwandoya mpaka Bariadi, kwetu sisi hii ni barabara ya muhimu sana kiuchumi hata kwenye utalii. Jimbo la Kisesa na Jimbo la Meatu tumepakana na Hifadhi ya Pori la Akiba la Maswa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watalii wengi wanapokuja wanapata shida sana. Hata Mheshimiwa Rais amekuja ameona hali halisi ya barabara hii. Hata hivyo, barabara hii imekuwa inawekwa kwenye ilani. Kila ilani unakuta ipo, lakini unakutana na maneno upembuzi yakinifu, upembuzi yakinifu. Ninamwomba ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, upembuzi ufikie mwisho. Tumechoka kusikiliza mambo ya feasibility study, sasa tunamwomba aje na mkakati wa namna gani anaenda kuikamilisha hii barabara. Kwa hiyo, tunamshukuru kwa sababu ameiweka kwenye bajeti, sasa tunamwomba atekeleze kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ndiyo inafungua mazao yetu ambayo tunalima. Sisi ni wafugaji tunasafirisha mifugo yetu kwenda kwenye minada mbalimbali kwa kupitia barabara hii. Kwa hiyo, tunamwomba sana Waziri, mazao yetu yaweze kwenda kwenye masoko mbalimbali. Atakuwa ameongeza mzunguko wa uchumi kwenye jimbo la Kisesa pamoja na Meatu kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa leo sitaki kuwa na mengi sana, ninachohitaji ni Barabara ya kutoka Mwanhuzi kuja mpaka Bariadi. Ninachohitaji ni Barabara ya kutoka Mwabusalu kwenda Sakasaka. Barabara ya kutoka Ng’hoboko kwenda Itinje kuelekea mpaka Lalago.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja ya bajeti hii. (Makofi)