Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon Zacharia Paulo Issaay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kwa ajili ya muda nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa rehema zake kwetu sote, niishukuru sana Serikali yangu kwa kazi kubwa iliyofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda huu ni miaka karibu 10 niko ndani ya Bunge hili na sasa tunaenda awamu ya tatu kazi kubwa imefanyika. Waheshimiwa Wabunge wenzangu wanakumbuka kwamba tulipoanza wakati ule 2015 kazi kubwa imefanyika kwa sekta ya barabara iwe TARURA, iwe TANROADS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa eneo hili ni kwamba, kuna baadhi katika maeneo ya nchi hii kama Wilaya ya Mbulu sisi tuko juu ya Bonde la Ufa, kule ni juu ya Bonde la Ufa, kwa hiyo hakuna jiografia inayofanana na Mlima Magara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri wengi wamekwenda Mbulu, lakini kila tulipofika walisema Mheshimiwa hii ndiyo barabara yako, hakuna barabara nyingine? Kwa kweli tunaipongeza Serikali ilichukua hatua kubwa ikaweka zege kwenye Mlima Magara, pia ikajenga Daraja la Magara. Tunampongeza sana Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuja 2015 hatukuwa na Daraja la Magara wala hatukuwa na zege kwenye Mlima Magara kwa sehemu kubwa, kwa hiyo kazi hiyo kubwa ilifanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali ni kwanza kazi zote tulizoanza tuendelee kuendeleza hizo barabara zimekaa muda mrefu. Barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla alivyokuja, mara baada ya ziara yake nilipokuja kwake hapa Bungeni Serikali ilimlipa yule mkandarasi na lakini bado hajarudi site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kabla Bunge halijakwisha arudi site. Baada ya Bunge hili Waziri afanye ziara ya kutembelea Barabara hiyo ya Mbulu – Garbabi na kipande cha Labay kwa sababu eneo hili la barabara limekuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Mbulu na hali imekuwa mbaya sana, hali ya usafiri na barabara zinajifunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali ni kwamba gharama tunazopata baada ya miradi kukaa muda mrefu, riba inakuwa kubwa na baadaye tunalipa hela nyingi sana kwa mkandarasi kutokana na hii hatua ya miradi kukaa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, eneo hili wameweka kilometa mbili tu za lami hadi sasa, lakini bado kilometa 23 zimebaki na mkandarasi hayupo site. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atakaporudi atuambie sisi Wabunge wa Mbulu Mkandarasi wa Mbulu – Garbabi atarudi lini site kwa sababu tayari Serikali imeshamlipa na hii ni hatua kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Mbuyu wa Mjerumani – Magara kwenda Mbulu usanifu umefanyika kwa takribani miaka miwili sasa, lakini ninachohofu ni kwamba baadaye tutarudi tena kufanya usanifu. Kwenye fedha za mwaka huu wameweka sehemu kidogo ya zege katika Mlima Magara

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali ikamilishe zege katika Mlima Magara na Mheshimiwa Waziri atakapokuja Mbulu, apite barabara ya Magara ndiyo atajua kwamba jiografia ya Wilaya ya Mbulu katika Mlima Magara na Mlima Dabidi, hakuna eneo kama hilo katika Tanzania hii, hakuna mwinuko wa mlima mkali wenye kona 130 ni Mbulu Mjini unapokwenda ambako inatuunganisha sisi na Mkoa wetu wa Manyara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika fedha za barabara tunazochanga kwa sasa bado tuendelee kutafuta vyanzo vya mapato. Mimi kwenye tozo ya simu na tozo nyingine mnazosema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha…

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti…

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha…

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru ninaunga hoja mkono, ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)