Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tandahimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu. Asiyeshukuru kwa kidogo hawezi kushukuru hata kwa kikubwa, nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha ambayo inajenga Barabara ya Mnivata – Nanyamba – Tandahimba mpaka Masasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia, kwa kutupa fedha pia ya Barabara ile ya Mingoyo – Lindi, Mingoyo – Mtwara na Mingoyo – Masasi lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua ndugu yetu Ulega na baada ya kushika madaraka haya ya Uwaziri ameweza kutembelea barabara tunazozitaja za kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo changamoto kwenye Barabara ya Mnivata – Nanyamba – Tandahimba mpaka Mitesa, mkandarasi aliyepewa barabara China Wu Yi ambao mkataba wake unamalizika tarehe 31 ya mwezi Oktoba mwaka huu. Tunapozungumza leo ameweka lami kilometa nne, mwenzie mwenye kilometa 60 China Communication ameweka lami zaidi ya kilometa 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amepata bahati ya kuja kwenye barabara ile na ile ni barabara ya uchumi. Tunapozungumza zao la korosho 60% ya korosho za Tanzania zinatoka kwenye hii Barabara ya Mnivata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, yeye ni mtu mwema sana, tunapomaliza kupitisha bajeti yake twende tukajue changamoto ya mkandarasi yule kama kuna namna ya kumfukuza, wamfukuze, wamweke mwingine wananchi wanataka barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanamtwara, Wanatandahimba, Wanananyamba, Wananewala, wanataka kuona barabara imekamilika kwa kiwango cha lami. Bahati nzuri fedha ya barabara ile inatoka Benki ya Maendeleo ya Afrika hakuna kona kona ya fedha, hapa pana janjajanja ya mkandarasi. Wenzetu wamesema kazi hizi kubwa zote wanawapa wakandarasi wa nje ya Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila ukisikia mradi mkubwa wa barabara wanawapa watu nje, tunashindwa namna ya kukabiliana nao. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri tukimaliza, ikiwezekana twende tukaangalie changamoto ya barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza wenzangu hapa, ili ufike Mtwara ni lazima uanze kutoka Mbagala, uende Mkuranga, Kibiti, Muhoro, Nangurukuru, Lindi. Barabara hii tunayoisema Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni amezungumza vizuri kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi tunaipongeza Serikali kwa kujenga madaraja, imefanya kazi kubwa sana. Tunataka tuone wakati una-wind up Mheshimiwa Waziri barabara hii mpango wake ukoje? Ninamwomba sana kaka yangu, nimepita usiku nikiwa ninatoka Mtwara kuja kwenye hili Bunge na kilichonileta hasa juu ya barabara hii nimepasua matairi manne, matairi manne nimeacha gari kwa ubovu wa barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba barabara hii tumekuwa na Mradi wa Cement wa Dangote, magari yale makubwa yote yamepita kwenye Barabara hii, sasa imekufa. Tumekuwa na Mradi wa Makaa ya Mawe umepita mle barabara imekufa lakini Serikali wakati wote wanazungumza juu ya Mradi wa LNG. Mwekezaji gani atakuja akapita barabara mbovu hii akaja kuwekeza Lindi, ni Mwekezaji wa aina gani apite kwenye barabara ile ya kwenda Lindi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wametengeneza pale Kilwa ipo bandari ambayo wamewekeza mabilioni ya fedha. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu, wakati ana-wind up hapo hapo wakati tunataka kupitisha bajeti yake nami nitakaa ndani humu. Nami katika watakaoshika shilingi na mimi ndugu yake nitashika shilingi kama sikusikia maneno mazuri juu ya Barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nami sitafika Mtwara hata kama atanijengea barabara yote ya Mtwara ya mzunguko, lakini kama kutoka Dar es Salaam kwenda Lindi kuna vumbi, kama ile barabara ni mbovu, maana yake sina sababu ya kufika Mtwara kwa sababu njia haipitiki. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha…
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho wenzetu wametoa mapendekezo hapa juu ya watu kuchangia sijui kwenye simu. Hivi mkulima wa korosho ambaye leo hata vocha ya shilingi mia tano hawezi kuweka, umwambie atozwe fedha eti achangie ujenzi wa Barabara, jambo hili halikubaliki, halikubaliki kabisa, halikubaliki kabisa. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha, unga mkono hoja.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)