Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Japhael Masanja Lufungija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi. Lakini nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kunipa uwezo wa kuweza kujadili Hotuba ya Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na kauli yake yenye utu tusonge mbele tunaendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana pia Waziri wa Ujenzi na Naibu Waziri, Katibu Mkuu dada yangu Aisha na daktari bingwa sana Dkt. Charles Msonde kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya, bila kumsahau Engineer wangu wa Mkoa ndugu yangu Mlimaji kwa kazi nzuri ambazo anazifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kuona imepanga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu na ujenzi wa Barabara ya kutoka Kahama – Ushetu – Ulyankulu kwenda Kaliua. Barabara hii ni barabara muhimu. Barabara hii ilianzishwa mwaka 2010 na imekuwepo kwenye Ilani zetu muda wote, lakini kwa umuhimu wa barabara hii inaunganisha mikoa zaidi ya kumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niitaje barabara hii inaunganisha Mikoa ya Tabora, Shinyanga, Geita, Bukoba, Mwanza na Mara kwa maana ya kanda maalum. Barabara hii itakapojengwa kutokea Mwanangwa itakuja mpaka maeneo ya Kahama na ndiyo barabara inayotoka kwenda huko Mpanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mikoa ya Kusini, barabara hii inaunganisha Barabara ya Tabora, Mkoa wa Tabora, Mpanda, Mkoa wa Katavi pamoja na Rukwa. Barabara hii imekuwa busy sana. Kwa takwimu za kawaida, kwa siku barabara hii inatumika na magari makubwa sita mabasi ambayo yanasafiri kila siku. Gari ndogo ndogo kwa maana ya hiace ni hiace tatu, mabasi ya kati ni mabasi ishirini na tano lakini malori kwa wastani wa kawaida kila siku inapitisha malori mia moja na kumi, ina maana kwa mwaka malori yanayopita ni 39,600. Kwa hiyo, unaweza ukaiona barabara hiyo ilivyo na umuhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninamwomba Waziri nimeona ameweka token pale kwamba imepata kifungu kwa maana ya kuingiziwa fedha. Tumwombe Mheshimiwa Waziri nchi hii imeundwa ikapewa kila eneo na vipaji vyake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukanda wa kaskazini wenzetu wanategemea mazao mengi yatoke Mikoa ya Kusini. Kwa maana ya wenzetu wa Katavi, Mpanda, Kaliua na Tabora sisi ni wazalishaji wakubwa sana wa zao la tumbaku, mahindi, mpunga, mifugo lakini pamoja na uzalishaji wa asali na misitu. Kwa hiyo, ni barabara ambayo ni ya muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza suala hili ili Waziri aipe kipaumbele kuhakikisha kwamba upembuzi sasa uanze, ikimpendeza hata kama ungeanza na Mwamnange - Ulyankulu kwenda Kahama halafu huku atoke Mwamnange kwenda Kaliua ili kuhakikisha kwamba ile barabara inaanza kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Waziri, nimeona Barabara ya kutoka Tabora kuja Ulyankulu kujengwa kwa kiwango cha lami. Ameitengea shilingi 2,000,000,000 nimshukuru na kumpongeza, kwamba barabara hiyo ni ya muhimu, ni barabara inayotuunganisha Mkoa na Jimbo la Ulyankulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikia tumbaku Tanzania tunazungumza Mkoa wa Tabora, ukisikia tumbaku Tanzania tunazungumza Wilaya ya Kaliua. Siyo Kaliua tu tunazungumza pia Jimbo la Ulyankulu lakini Ulyankulu tunayo madini, tuna mgodi pale Nsungwa, kwa hiyo, tuone umuhimu wa kuifungua barabara hii ili kuhakikisha inachochea uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru nimeona barabara inayotoka Ulyankulu kwenda Urambo kwa mama yangu Margaret Sitta, imepewa token, Mungu akubariki sana mjukuu wangu, huyu ni mtu muhimu sana katika maisha yetu, nimwambie mimi sitashika shilingi yake, ninaamini tunapitisha mpango wa PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kule Ugalla muhimu kabisa ile barabara tukijenga daraja na sisi hatuna matatizo ukanda ule jenga Daraja la Ugalla ambalo miaka ya nyuma liliingiwa mkataba wa kujengwa kwa muda wa miezi 18, lakini fedha hizo hazikutoka. Likijengwa hilo daraja ninaamini litatuunganisha vizuri na mama yangu Mheshimiwa mama Lupembe pamoja na Haidary na ndugu yangu wa kule Mpanda, Katavi na Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi tunayo hii Barabara ya Tabora – Ibiri – Ulyankulu. Sasa kwa sababu tayari kuna madaraja alishajenga ninamwomba hatua nyingine za kuanza kuwafanyia tathmini watu wanaostahili kulipwa, ianze kufanyika ili kuhakikisha kwamba shughuli inafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya kutoka Kahama, limejengwa daraja zuri sana pale Kashishi baina ya Sunga na Kashishi. Barabara ya kiwango kizuri ndiyo hayo ambayo pia Serikali kupitia Waziri Mkuu amekuwa akieleza Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba inajenga daraja, kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri ajenge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo pia barabara inayotoka Jimbo la Ushetu kwa maana ya Halmashauri ya Ushetu. Barabara hii inatokea Masumbwe inapita Mwabomba inakuja mpaka Ulowa namba nne lakini inakuja kuniunganisha huku na Sungwa. Liko daraja moja limejengwa zuri sana Serikali imewekeza fedha nyingi. Ninaiomba Serikali yetu pendwa, bila kujenga Daraja la Mto Igombe linalotuunganisha sisi na Ushetu bado tutakuwa hatuitendea haki barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma ninakumbuka barabara hiyo pia ilikuwa kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuwapunguzia watu wanaotoka Mikoa ya Geita na Mwanza wanapotaka kwenda mikoa aidha ya Katavi na Mbeya watatoka wakifika Masumbwe wanakata kupunguza umbali, wakija wanafika Ulyankulu watapita Urambo watakwenda Ipole, wataunga kwenda Mkoa wa Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa hawa wanaohitaji kwenda Mkoa wa Katavi watafika Ulyankulu. Waziri anitengenezee roundabout nzuri pale Mwenda Kulima, kwa maana ya Uyowa, aweke roundabout nzuri pale Barabara Sita Ulyankulu ili kuhakikisha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha…

MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: …wanaokwenda Urambo watakuwa wanakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)