Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Benjamin Lukubha Ngayiwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana pia kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia Bajeti ya Wizara yetu nyeti kabisa ya Ujenzi. Sote tunafahamu kwamba, kama ilivyo katika mwili wa binadamu, barabara zinakuwa kama blood vessels, zinapitisha damu katika mwili mzima. Ndivyo ilivyo katika kusafirisha bidhaa na binadamu kwa maana ya abiria katika kukuza uchumi wa nchi yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru sana Serikali na hasa Wizara ya Ujenzi. Nimeona katika bajeti yao na katika makadirio yao, wametenga shilingi 500,000,000 kwenda kukarabati Barabara ya kutokea Kahama, inapita Nyandekwa, inaenda Nyamilangano mpaka Uyogo kwa Mheshimiwa Cherehani, shilingi 500,000,000. Ninaishukuru sana Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, Barabara inayotoka Kahama - Kakola kwenda Bulyanhulu kwa Mheshimiwa Magangila, na yenyewe inatengenezwa kilometa 73. Pia, Barabara kutoka Kahama – Tulole – Muhuridede mpaka huko Mambali, Tabora kilometa 152 imetengewa na yenyewe bajeti ya shilingi 500,000,000 lakini kipande cha kilometa 20 kutoka Kahama kwenda Tulole na chenyewe kimetengewa fedha kwa ajili ya kukarabatiwa. Kwa hiyo ninaishukuru sana Wizara, ninaishukuru sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Jemedari Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninajielekeza katika hoja nyingine na Mheshimiwa Abdallah Ulega kaka yangu ninaomba anisikilize hapa, ninaomba ombi hili muhimu sana. Ile barabara ya kutoka Kagongwa unaenda mpaka Nzega yenye kilometa karibu 73, karibu kilometa 65 imejengwa mpaka kufikia tabaka la tatu kwa maana ya lugha ya kitaalamu G-45 kupitia ufadhili wa kampuni moja ambayo ni ya EACOP inayotengeneza mabomba ya mafuta kwa ajili ya Mradi wa EACOP kwenda Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilichobaki ni tabaka la kuwekewa lami tu. Sasa majibu ya Serikali hapa wanasema wanatafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha tabaka la lami. Ninamwomba ndugu yangu Mheshimiwa Abdallah Ulega, afanye juhudi za makusudi kwenda kumalizia tabaka hili la lami kutoka Kagongwa kwenda pale Igusule ili tuiweke lami barabara hii isije ikaharibika. Tukikaa muda mrefu na mvua zikanyesha tena za msimu ujao, barabara zile tabaka la tatu, la pili mpaka la kwanza zitaharibika, tutaanza tena upya kwa gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumebakiza kipande cha kumwaga lami tu kilometa 18.3, Kagongwa – Igusule. Ninamwomba sana kaka yangu Mheshimiwa Abdallah, sitaki kusema mambo ya kushika shilingi. Ninamwahidi, akinitengenezea barabara hii, kwa kuwa wao ni Waislamu wanaruhusiwa mathna na kule tuna Wasukuma wazuri wazuri, aje aniambie tutampatia mke mwingine kutoka kule Kahama. Siyo rushwa lakini ninakuombea mema ndugu yangu Mheshimiwa Abdallah Ulega. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara nyingine ile inayotoka Kahama, inapita Nyandekwa inaenda mpaka Nhwande, Ugalla, Kaliua, inatokezea Ulyankulu mpaka Mpanda. Hii barabara inaunganisha Mikoa hii ya Shinyanga mpaka Mpanda. Ni barabara muhimu, inasafirisha mazao, tumbaku kutoka kwa Mheshimiwa Cherehani, inasafirisha mbao, mpunga, mahindi na alizeti. Ni barabara muhimu sana hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba tena Mheshimiwa Abdallah Ulega, barabara hii amesema kwamba imetengewa fedha shilingi 150,000,000 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu. Ninamwomba Mheshimiwa Abdallah Ulega, hizi lugha za upembuzi yakinifu, usanifu sijui feasibility study, zimekuwa ni lugha za kawaida sana na hii barabara imekuwa ikitengewa bajeti kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Waziri tuanze hata na kipande cha kutokea Kahama tufike Nyamilangano twende mpaka Kaliua huko, Bulyanhulu na twende polepole tuweke lami barabara hii ili wananchi wetu wasafirishe mazao na waweze kusafiri kipindi chote bila kupata shida yoyote. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana kwa muda huu. Mheshimiwa Abdallah Ulega ile Barabara ya Kagongwa kwenda Igusule, kilometa 18 tuimwage lami ndugu yangu, nitakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaomba kuunga hoja mkono. (Makofi)