Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Emmanuel John Khambay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara yetu hii ya Ujenzi. Awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuweza kusimama mahali hapa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Babati Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu waliopata nafasi ya kuchangia wa Bunge hili na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka Mkoa wa Manyara. Mkoa wa Manyara ni miongoni mwa mikoa mikubwa katika nchi yetu, lakini ni mkoa ambao umekuwa na changamoto kubwa ya barabara. Sasa ni wakati wetu watu wa Mkoa wa Manyara, Wizara hii chini ya ndugu yetu Mheshimiwa Ulega, utupe kipaumbele na sisi walau katika hizi kilometa zaidi ya 1,600 ambazo ziko chini ya TANROADS, lakini kilometa 259 ndiyo zenye lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo kilometa ni kilometa zinazotoka kwenye Makao Makuu yetu ya Mkoa kuelekea Dodoma, kuelekea Singida, kuelekea Arusha, lakini kama mkoa wenyewe una kilometa 207 ambazo zinahitaji kuwekewa lami. Mheshimiwa Waziri ndugu yetu Mheshimiwa Ulega, tunatambua kwamba, Wizara hii ni ngumu na inahitaji fedha na fedha alizotengewa bado hazitoshi. Hata hivyo, fedha hizi zilizotengwa, kama zitapatikana na zisiposimamiwa kwa weledi, bado hazitoweza kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia nafasi hii kuungana na wenzangu kama nilivyokwishatangulia kusema, Mkoa wa Manyara hususan Wilaya yangu ya Babati Mjini, tuna uhitaji wa bypass.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bypass ni hitaji muhimu kwa Makao yetu Makuu ya Mkoa ambapo ni Wilaya yetu ya Babati Mjini kama ambavyo Singida ilivyo ina uhitaji wa bypass, kama ilivyo Tabora ina uhitaji wa bypass. Kwa hiyo ninamwomba Mheshimiwa Waziri, atakaposimama, sitamani kushika shilingi yake kwa sababu amekuwa ni mtu muungwana, wakati wote tumesema na yeye na amekuwa akitenga muda wake kutusikiliza, hatutamani kushika shilingi yake lakini asimamapo, tunaomba aje na majibu sahihi kuhusiana na suala la bypass. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona nimetengewa kilometa 15.5 bypass ya Babati – Dodoma, lakini kuna mkanganyiko kidogo. Kuna eneo ambalo linaonesha Mhandisi Mshauri amepewa jukumu la kufanya utafiti katika barabara hizi mbili (Barabara ya Babati – Dodoma yaani bypass na bypass ya Babati – Singida). Hivyo asimamapo, ninaomba anipe uchambuzi sahihi juu ya suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Barabara ya kwetu ya Singe – Kimotorok na Ngoytok. Barabara hii inaunganisha Jimbo la Babati Mjini, Jimbo la Babati Vijijini na Jimbo la Kiteto pamoja na Simanjiro. Mheshimiwa Waziri upembuzi yakinifu umekwishafanyika juu ya barabara hii, lakini na usanifu wa kina umekwishafanyika, hivyo tunamwomba Waziri atusaidie ili barabara hiyo iweze kukamilika kwa sababu ni barabara muhimu katika uchumi wa Mkoa wa Manyara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tuna wananchi wetu katika barabara hiyo hususan kwangu Jimbo la Babati Mjini eneo la Hala na maeneo mengine katika barabara hiyo, wananchi wanahitaji kulipwa fidia. Tunaomba wananchi waweze kulipwa fidia kwa sababu taratibu zote zimekwishakamilika ili shughuli hiyo iweze kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Babati, ina uhitaji pia, kwa sababu ya msongamano wa magari. Sisi watu wa Babati Mjini tuna uhitaji wa double road. Double road ya Babati – Singida, double road ya Babati – Arusha na double road ya Babati – Dodoma kwa sababu barabara ile imezidiwa, magari zaidi ya 600 kila siku yanapita katika barabara ile. Sasa ni wakati sahihi wa wizara kuangalia namna sahihi ya kutusaidia kuepukana na msongamano wa magari makubwa kwa sababu Bandari yetu ya Tanga imekuwa ikihudumia nchi za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo barabara yetu imekuwa busy kuhudumia usafirishaji wa magari hayo katika kusafirisha mizigo. Hivyo ninamwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie sisi watu wa Babati, watu wa Mkoa wa Manyara kwa sababu tuna uhitaji mkubwa wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunipa kilometa moja ya Barabara ya kutoka Kiru – Mbulu. Barabara hiyo pia ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wa maeneo hayo kwa sababu inaunganisha Jimbo la Babati Mjini, Jimbo la Babati Vijijini na Jimbo la Mbulu. Mheshimiwa Waziri, kilometa moja haitoshi, kwa heshima ya kaka yangu Mheshimiwa Naibu Spika, kutupa kilometa moja bado haitoshi. Tunamwomba, katika bajeti hii ya mwaka huu, atuongezee fedha ili barabara hiyo walau iweze kusogea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ninamwomba kwa Barabara ya Mbuyu wa Mjerumani – Magara – Mbulu. Barabara hiyo pia iweze kukamilika ili kuweza kusaidia wananchi wa eneo hilo. Barabara hiyo pia ni muhimu kwa sababu inatumika pia kwa utalii. Kwa hiyo, ninamwomba, kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wa Mkoa wa Manyara waliotangulia kusimama walivyozungumza, sisi Mkoa wa Manyara tuko nyuma kwenye suala zima la barabara. Tunaomba asimamapo hapa, atuambie ni kipaumbele kipi anatupa katika kutusaidia ili walau barabara hizo ziweze kuboreka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata zile za kiwango cha changarawe zimechakaa. Sisi watu wa Mkoa wa Manyara tuna changamoto kubwa sana. Tunaomba Waziri atusaidie ili suala hilo liweze kwenda sawasawa na wananchi wa Jimbo la Babati Mjini na majimbo mengine ya Mkoa wa Manyara waweze kutufurahia sisi wawakilishi wao kwa majukumu ambayo wametupatia. Kutokutusaidia ni kutuweka katika mtego sisi Waheshimiwa Wabunge wote tunaotoka kwenye Mkoa wa Manyara kutokana na changamoto ambayo tunayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufikia hapo, ninaunga mkono hoja, lakini asimamapo Waziri ninaomba majibu ya kina kuhusiana na bypass ninarudia tena. Ahsante. (Makofi)