Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Emanuel Qambaji Nuwas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu katika majimbo yetu wanahitaji mambo matatu; la kwanza wanahitaji maji, la pili wanahitaji barabara na la tatu wanahitaji nishati. Hayo ndiyo mambo matatu ya msingi sana ambayo wananchi wetu wanalilia kule katika majimbo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Manyara ambako ndiko Jimbo langu Mbulu Vijijini liliko tuna kilometa chache sana za lami. Kwa haraka haraka barabara ambazo zinahudumiwa na TANROADS ni kilometa 1,657. Kati ya hizo ni kilometa 259 tu ndizo za lami. Vilevile, pamoja na hiyo ni 16% tu peke yake za kilometa ambazo zinahudumiwa na TANROADS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mkoa wetu kwa kweli una kilometa chache sana za lami; na hivyo nimwombe Waziri wetu wa Ujenzi autazame mkoa wetu. Ninaamini kwamba tunalitendea haki Taifa letu kwa kufanya uzalishaji katika eneo la kilimo, eneo la ufugaji, eneo la madini na vilevile na eneo la viwanda. Kwa hiyo, tunahitaji kutazamwa kwa namna ya pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika barabara hizo barabara pekee ukiacha barabara za TANROADS ambazo ni takribani kilometa 206, kilometa 52 ndizo ambazo zinaunganisha halmashauri zetu sita. Kwa kuangalia kwa haraka haraka Wilaya yangu ya Mbulu ambako ndiko Jimbo la Mbulu Vijijini liliko, tuna kilometa 12.5 tu za lami na ndiko ambako tunalia kwa namna ya pekee sana. Wananchi hawa wana haki ya kupata barabara za lami na wana haki ya kupata barabara zinazopitika majira yote ili kufanya shughuli zao za uzalishaji hasa katika eneo la kilimo, eneo la mifugo, lakini vile vile na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana, Mheshimiwa Waziri ametenga fedha, ukiangalia zile barabara za changarawe zilizotengewa fedha kufanyiwa maintenance kwa mwaka huu wa fedha wa 2026/2027, mkoa pekee ambao unaongoza kwa kuwa na barabara za changarawe na za udongo ni Mkoa wa Manyara; zaidi ya kilometa 1,356. Tofauti na mikoa mingine yote ya Tanzania. Kwa hiyo ninaomba Mheshimiwa Waziri atutazame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ninakuja kwenye eneo la pili, kwamba tunajua hizi zina athari kubwa sana katika shughuli za uchumi za wananchi. Kwa hiyo, lazima tuone Wanamanyara hatujawakosea lolote, tunaomba tuzingatiwe kwa namna ya pekee. Tunashukuru tumepata fedha, ametutengea kiasi cha fedha katika Barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Lalago mpaka kwenye barabara ile ya Maswa Road. Kwa kweli tunashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata kilometa 25 za Barabara ya Mbulu – Garbabi na pia tumepata kilometa 25 za Barabara ya Labay – Haydom, lakini bado kasi ya ujenzi ni ndogo sana. Hadi sasa kwa kipande kile cha Mbulu – Garbabi ni kilometa tatu tu zimekamilika. Je, itahitajika miaka mingapi kukamilisha? Bado tuna safari ndefu sana. Ninaomba Mheshimiwa Waziri aongeze fedha pale; na ninaomba sana nipate maelezo, je, barabara hii itakamilika baada ya miaka mingapi? Tunahitaji kuona barabara hii ikikamilika ili wananchi wakafanye shughuli zao za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna wananchi ambao wamekutwa na ile barabara, bado wanahitaji kulipwa fedha zao kwa ajili ya kupitiwa na barabara ile. Ni takribani miaka mitatu na tayari muda ule wa mkataba umekwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba atakaposimama Mheshimiwa Waziri atupe maelezo ya kwamba ni lini barabara hizi zitakamilika lakini pia wananchi hawa watalipwa lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa Barabara ya Dareda – Dongobesh, tumepata fedha kidogo kwa kilometa chache, tunaomba fedha ziongezewe. Hii barabara ni muhimu, ndiyo inayounganisha Wilaya ya Mbulu kwenda Makao Makuu ya Mkoa. Tunaomba ipate lami ili iweze kukamilika. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri aitazame kwa namna ya upekee. Hatuwezi kwenda kutumia masaa zaidi ya matano au sita kwenda Makao Makuu ya Mkoa ambako ndiyo eneo la kiutawala na wananchi wanahitaji kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata Barabara ya Haydom – Katesh, tunashukuru usanifu umekamilika, imetengewa fedha shilingi 250,000,000 lakini haitoshi. Barabara hii ni muhimu kwa ajili ya hospitali yetu ya Kilutheri ya Haydom ya Rufaa ya Mkoa. Pia, ngano inalimwa kule kwa wingi na ngano haiwezi kutoka kama hatuna barabara nzuri. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tunaomba barabara hii tuiongezee fedha. Kwa kuwa umesema mwenyewe hapa, ziko barabara mpya ambazo tumesema ziachwe kwanza. Zile ambazo usanifu umekamilika na tayari ziko kwenye mpango zitengewe fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru pia kwa Barabara hii ya Haydom – Ilongero kwenda Singida kilometa karibu 96, imetengewa fedha, pia tunaomba Waziri aiongezee fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kusema mawili ya mwisho. Tuna barabara za mkoa; tuna Barabara ya Babati – Singida ambayo imeharibika, tunaomba itengewe fedha. Ile barabara ni aibu kwa Taifa lakini pia inaangusha biashara. Tunaomba ifanyiwe ukarabati ili iweze kutumika kwa ajili ya shughuli za kibiashara lakini vilevile kwa shughuli nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara za mkoa; Barabara ya Arusha – Kibaya kwenda Kongwa, ni barabara muhimu sana na ndiyo ambayo inaturudisha nyuma kama mkoa kuwa na kilometa chache za lami. Tunaomba tutazamwe kama Mkoa wa Manyara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuna Barabara ya Handeni – Kibaya – Singida ambayo ni muhimu pia kwa Bandari yetu ya Tanga. Tunaomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama, basi atujibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, Mheshimiwa Waziri tumetenga fedha kwenye Road Fund kwa ajili ya marekebisho. 35% TARURA, 65% kwenda TANROADS, lakini bado hatuipati hii fedha. Wananchi wanaochangia, ni wale wanaolipishwa nauli, ni wale bodaboda, ni wale wa bajaji ndiyo wanakatwa kwenye mafuta kila lita. Tunaomba hizi fedha ziheshimiwe na kama ambavyo iko fenced, ziweze kwenda kutengeneza barabara. Wananchi wanataka kuona ma-grader yakiwa yanatengeneza barabara ili waweze kuendesha maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo ya simu hatuwezi kukubaliana nayo kwa sababu inakwenda kugusa maisha ya wananchi wetu. Lazima tutafute vyanzo ambavyo havigusi maisha ya wananchi wetu. Kwa sasa wana maisha magumu kutokana na gharama kubwa za bei ya mafuta, kwa hiyo lazima tuondokane na hiyo. Hata hivyo, ninaunga mkono suala la kuangalia bond ili kuona namna ya kupata fedha za hakika ili kutengeneza barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kukushukuru sana na ninaomba kusema, Mheshimiwa Waziri atakaposimama atupe maelezo haya ili tuweze kuunga mkono hoja yake na aweze kwenda kutekeleza. Ahsante sana. (Makofi)