Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na afya. Niendelee kuwa pamoja na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo imeendelea kuifanya ya kujenga miundombinu kwenye nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nitajikita kwenye fidia. Nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri, naomba ku-declare interest; Mheshimiwa Waziri ni youth league mwenzangu, kwa hiyo sitachukua shilingi yake; lakini nitaelezea ukweli wa mambo jinsi yalivyo katika jimbo langu na kwenye Mkoa wangu wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Barabara ya Stalike – Mpanda – Mpanda Ndogo. Barabara hii ilianza ujenzi wake mwaka 2015 na imekwishakamilika; lakini hadi leo wananchi walio kandokando ya barabara hiyo, hawajalipwa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, tumefanya ziara na Mheshimiwa Waziri Mkuu, hoja za wananchi zilijitokeza kwenye mikutano; na majibu ya Wizara ya Ujenzi ilikuwa ni kwamba katika bajeti hii watatenga pesa ili uthamini ukafanyike upya kwa sababu uthamini huu umefanyika kwa muda mrefu. Nimwombe sana ndugu yangu, kaka yangu Mheshimiwa Ulega, tunaomba wananchi wale waende wakafanyiwe uthamini na ikiwezekana waanze kulipwa fedha zao kwa sababu jambo hili limekuwa ni la muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba jambo hili linawa-cost wanasiasa kwa sababu Serikali inaahidi lakini hili jambo halitekelezeki; na tukienda kwa wananchi, wananchi wanashindwa kutuelewa. Kwa hiyo, ninamwomba sana; hilo la kwanza liko kwenye jimbo langu, liko kwenye jimbo la Mheshimiwa Lupembe - Nsimbo, lakini liko pia kwenye jimbo la Mwenyekiti wa Kamati hii, Mheshimiwa Kakoso huko Tanganyika. Kwa hiyo ninamwomba sana alichukulie uzito unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwa sisi watu wa Mpanda na watu wa Tabora maeneo ya Kaliua, tunayo barabara ya kuanzia Mpanda mjini – Ugala – Kaliua – Kahama. Barabara hii imeanza kuwekwa kwenye Ilani tangu mwaka 2015, lakini mpaka leo nimesoma kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri sijaiona hii barabara. Hiyo siyo shida kwa sababu bado tuna miaka minne ya utekelezaji wa Ilani ya chama chetu. Ningemwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwenye maeneo mengine, ninatolea mfano Barabara ya Sumbawanga ilivyoanza kujengwa, yalianza kujengwa kwanza madaraja kabla ya barabara ya lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, kwamba tunataka Daraja la Ugala lenye urefu wa meta 150 lijengwe ili tuanze kuona picha ya hiyo Barabara sasa ya kutoka Mpanda – Kaliua – Kahama itakuwaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wamekwishaanza kazi pale, wameweka fedha, wamejenga box culverts nne, lakini sasa zile box culverts walizozijenga pale kama hamna la Ugala zile box culverts zilikuwa na maana gani ya kujengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, chonde chonde, tunaomba Daraja la Ugala. Ninataka majibu kwamba Daraja la Ugala litajengwa lini. Ndiyo, Ugala si jimbo langu, lakini ninatoka jimbo la mjini pale katikati ambazo barabara zote zinazojengwa kwenye Mkoa wa Katavi mimi ndiye mnufaika namba moja kwa sababu jimbo langu ndilo jimbo la mjini. Kwa hiyo ninamwomba sana ndugu yangu atusaidie kwenye hilo Daraja la Ugala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona amelieleza kwenye ukurasa wa 11 wa hotuba yake, lakini tunataka majibu ya kina tuone ni namna gani sasa wananchi wa Katavi watafunguka. Katavi imekaa kwenye jiografia ambayo inaunganika na mikoa zaidi ya minne na kote huko kuna barabara. Nimwombe barabara ya Kigoma imeongelewa na nimeona kwenye bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ni moja kwenye hizi barabara ambazo zinakaa muda mrefu. Hii pengine Waheshimiwa Wabunge ni lazima tufahamu. Kwa mfano Barabara ya Kibaoni, toka ilivyotangazwa kilometa 50, leo hii ni mwaka wa nne. Hivi yule mkandarasi aliyeko pale site kwa miaka minne ile gharama ya shilingi 52,000,000,000 ndiyo itakuwa hiyo hiyo ya kwenda kumlipa atakapokamilisha hii barabara? Jibu ni kwamba siyo, tutakwenda kumlipa zaidi ya shilingi 100,000,000,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini tutekeleze hii miradi kwa gharama ambazo zilikuwa zinawezekana, lakini kwa kuchelewesha mradi unakwenda unaongeza gharama kubwa zaidi kwenye mradi? Vivyo hivyo kwa Barabara ya Kigoma. Nimwombe sana ndugu yangu, barabara hizi ni muhimu kwa uchumi wa Mkoa wetu wa Katavi, lakini na mikoa ya ukanda huo wa Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme machache tu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante, muda wako umekwisha Mheshimiwa.
MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, sekunde chache tu. Mkoa wa Katavi ndiyo mkoa uliobaki ambao haujaunganishwa na mikoa mingine. Sisi watu wa Mkoa wa Katavi tumelikosea nini hili Taifa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako. Sasa ninamwita Mheshimiwa Simon Songe…
MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)