Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwenye enzi na utukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa wanayoifanya katika sekta hii ya ujenzi. Kiukweli kabisa kazi kubwa imefanyika katika Taifa letu, hilo halipingiki, ukichukulia zero ya barabara zote nchini pale Clock Tower Dar es Salaam mpaka Kigoma unakwenda bila kukanyaga vumbi, ni mapinduzi makubwa na tuipongeze Serikali kwa kazi kubwa inayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ya ujenzi katika sera yake ya mwaka 2003 ilishazungumza suala la ushirikishwaji wa wanawake na vijana katika shughuli za ujenzi. Miaka yote hiyo hatua kadhaa zimekuwa zikifanyika, lakini tumpongeze Dkt. Samia Suluhu Hassan, significant impact imekuja kutokea awamu hii ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu mwanamke Eng. Aisha Salim Amour.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya wanawake wakandarasi imetengwa kwa kiwango cha shilingi 40,000,000,000 na zaidi, haijawahi kutokea. Huko nyuma mimi binafsi nilishiriki sana kuwa-train wakandarasi wanawake, lakini hili jambo lililotokea kipindi hiki ni jambo kubwa na ni jambo la kupigiwa mfano. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Ulega kwa kusimamia jambo hili kuweza kutokea. Hongera sana TANROADS kwa utekelezaji wa jambo hili. Mimi nina hakika wataiona tofauti. Wakandarasi wanawake wakipewa fedha hawazipeleki sehemu nyingine, fedha yote inarudi barabarani, hongera sana Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kusema kwamba kuanzia mwaka 1980 mpaka 1990, Taifa letu lilikuwa linatekeleza ujenzi wa barabara kwa kutumia mfumo wa nationalization of the budget; kwamba, fedha yote inawekwa katika kapu moja. Haya yanayotokea sasa barabara kuweza kwisha muda wake na zikawa na hali mbaya yaliwahi kutokea mwaka 1980 mpaka 1990.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo sababu ilianzishwa Road Fund Board mwaka 2000. Ilionekana kwamba, haiwezekani kuweka fedha pamoja, utahakikisha tu unajenga, unajenga, unasahau maintenance. Ndiyo sababu ulianzishwa Mfuko huu mwaka 2000. Hiki kinachotokea sasa hivi ina maana tunarudi miaka ya 1980 na 1990. Barabara kweli zilifunga na tukaanza kujenga upya. Hiki kinachotokea sasa hivi ina maana tunarudi tena kule nyuma. Maana yake ni nini? Tunataka kuiua Road Fund Board ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingi za Afrika wapo walioanzisha Mfuko wa Barabara na ukafa kwa sababu hii na mmojawapo ni Ethiopia. Kwa hiyo, kama Taifa tunataka kurudi kule kujenga tena barabara upya kama tulipotokea miaka ya 1980 hadi 1990, basi tuendelee kuzichanganya hizi fedha katika Mfuko mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme kwamba, licha ya kwamba Serikali imefanya kazi nzuri kwa wakandarasi; nami ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipoingia tu madarakani, yeye ndiye aliyetunga kanuni kwa ajili ya ile sheria ya kubaini matatizo ya kodi, ile taasisi ya kushughulikia malalamiko ya kodi. Hii iliwasaidia sana wakandarasi wa ndani kwa sababu walikuwa na changamoto nyingi; na yeye tunampongeza sana kwa jambo hilo. Hata hivyo, sasa ukweli ni kwamba ni lazima wakandarasi hawa tuwaangalie kwa jicho la pekee hasa wakati huu ambao mafuta yamepanda bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi anayetekeleza mradi sasa hivi wakati ali-tender mafuta yakiwa ni lita shilingi 2,000 sasa hivi mafuta ni shilingi 4,000, hali ya mkandarasi huyu kiukweli ni kwenda kufilisika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri sekta hii ilishaliona jambo hili muda mrefu kimataifa na kitaifa; FIDIC Condition of Contract Red Book, huu ni mkataba wa kimataifa wa utekelezaji wa kazi za ujenzi; unazungumza vizuri kwenye clause ya 13.7, suala la cost adjustment iwapo tu Serikali inapotangaza kupanda kwa bei ya mafuta. Vilevile, PPRA yenyewe kwenye mikataba yetu ya ndani Kifungu Namba 17.8 kinazungumza suala la cost adjustment iwapo tu Serikali imetangaza kupanda kwa bei ya mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la kutafuta fedha kwa ajili ya kuiongezea wizara hii is inevitable; ni lazima fedha zitafutwe kuweza kusaidia kuinusuru sekta hii ya ujenzi. Kwa suala la kutafuta fedha ninaunga mkono kwa asilimia mia moja, shemela (shemeji) wangu Mheshimiwa Ulega kuhusiana na suala la hatifungani. Kitu ambacho kilichelewa tu kufanyika ni kuja kutupiga semina hapa ndani. Watu wanachanganya mambo, hatifungani ni tofauti kabisa na EPC + F, ni vitu viwili tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kupata elimu na kulielewa jambo hili vizuri. Hatifungani inaelekea katika ile sera ya Serikali ya kufanya uchumi fungamanishi na uchumi shirikishi; kwamba wananchi wenyewe tunashiriki kujenga barabara zetu wenyewe kwa kutumia fedha zetu na halafu tunapata faida.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE … kwa hiyo, suala hili tupate kuelewa zaidi, lakini ninaunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie, kwamba sishiki shilingi kwa sababu lililokuwa likitugombanisha katika Barabara ya Kiomoni limeanza kufanyiwa kazi na mkandarasi yuko kazini. Ahsante sana.