Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kija Limbu Ntemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyosaidia kuifungua nchi yetu barabara zote ambazo zinapitika kwa sasa. Pia niipongeze Wizara ya Ujenzi ikiongozwa na Mheshimiwa Waziri Ulega mwenyewe. Mheshimiwa Ulega ni mtu mzuri, mwaminifu na msikivu, anayeshirikiana na mtu yeyote na anasikiliza mawazo ya kila mmoja, hicho ndicho ninachompongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri anapokea na mengine anayafanyia kazi na yasiyowezekana anasema atalifikisha kwenye Wizara ili waweze kulichambua, ninampongeza sana. Nimekuwa nikimfuata kila siku, nina Barabara yangu ya kutoka STAMICO kwenda CCM, angalau basi kilometa tatu amenitia moyo sana, amenishauri vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea mawazo yake, lakini ninamwomba atakapopata fedha, ameniambia kuna kilometa 47 kutoka Ushirombo kuja Katoro na kule Ushirombo walishaanza kujenga japo walisimama kwa wakati, basi ninamwomba atakapoweka bajeti zake vizuri, aje aanzie pale Katoro anipe kura zangu maana atanipotezea kura. Aje pale Katoro anisaidie kuanzia Katoro, anitoe tu kidogo, watu wale wanapata vumbi sana. Ninaamini Waziri atafanya kwa sababu yeye ni mtendaji mzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemshukuru sana Waziri Ulega amenikumbuka kwenye Barabara ya Chibingo - Chigunga – Bukondo, amenitengea fedha za kurekebisha ile barabara na watu wangu walikuwa wanapata shida sana na walikuwa wanasubiri hii bajeti wajue, je, watapewa fedha kwa ajili ya marekebisho ya ile barabara. Nitamuunga mkono Waziri Ulega kwa asilimia zote 200 ili apitishiwe bajeti ila nimwombe kitu kimoja, nimekubali safari hii kwa sababu mimi ni Engineer, yule mkandarasi atakayemleta nitakwenda kumsimamia. Maana barabara zetu zinaharibiwa na wakandarasi, wanatujengea barabara za kiwango cha chini kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata barabara zetu za lami zimekuwa na changamoto hizo kwa sababu wale tunaowapa kazi, yaani mimi huwa ninashangaa sana anakuwepo mtu anaitwa consultant ila ukiangalia consultant anachoshauri baada ya miezi sita alichoshauri ni nini mbona barabara imeharibika? Nimwombe Mheshimiwa Waziri, baada ya bajeti yake, akae na wataalam, tunataka sasa anapokwenda kuanza kufanya kazi mwaka huu barabara zetu zitakazojengwa zote ziwe kwenye kiwango kinachotakiwa.

(Hapa Mhe. Kija L. Ntemi aliongea lugha ya Kisukuma)

MHE. KIJA L. NTEMI: Olo udumha, nikharibishage onhe nakoghunane nanhe, nadolile. Obhebhe olo odumha hange nikharibishege nakoghunane nang’ho ili tujelhaneje pyabhose bhapamoja. [MANENO HAYA SIYO SEHEMU YA TAARIFA RASMI ZA BUNGE]

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kija kwa mujibu wa Kanuni zetu ni lugha mbili tu zinatumika ambazo ni Kiingereza na Kiswahili.

MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana ninarekebisha.

MWENYEKITI: Hivyo, Hansard ifute haya maneno uliyoyataja.

MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme kwamba nilikuwa nasema hivi, Mheshimiwa Ulega baada ya bajeti hii aniite na mimi tusaidiane ili twende pamoja ili tutafute watu wanaotujengea barabara zetu kwa kiwango cha chini tuwaondoe. Tunataka kiwango cha lami standard.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Barabara kutoka Kahama kwenda Runzewe malori yote yanayotoka bandarini yanapita miaka yote katika ile barabara, ile barabara sijajua nani aliyeijenga ni barabara bora miaka yote, haijawahi kuharibika, kwa nini? Barabara zingine zimekuwa na changamoto sana. Kwa hiyo, tunaomba yule mkandarasi aliyejenga wataalam wako hapa, wamtafute, yule aliyejenga Barabara kutoka Kahama kwenda Runzewe, wampe tenda na wampe fedha atutengenezee barabara zetu zote zilizoharibika ili ziweze kuwa imara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kurudiarudia kila mwaka tunarudi nyuma, yaani miezi sita umerudia, miezi sita umerudia, hatuwezi. Tunamuunga mkono Waziri, lakini kwenye timu yake tunaomba akawarekebishe, akawaambie wajipange kwa ajili ya kutengeneza barabara vizuri ili barabara zipitike vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, ninaiomba sana Wizara inapokwenda hata kuziba ile mitaro ambayo imeshatokea, ninaomba jambo hili, watakapokwenda kuanza kuziba zile barabara watafute lami sahihi ya kuziba, siyo kutuwekea mchanga. Mheshimiwa Waziri tunaumia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi juzi kidogo nife, nilikuwa ninatoka Bariadi ninaenda airport nimechelewa, nikapiga shimo, yaani kui-control gari ni kazi sana nikasema sasa mimi Mbunge ningekufa leo halafu na miezi nane wananchi wangu wangefanyaje, lakini ni kwa sababu barabara mbovu. Tuanze tena uchaguzi leo tu kwa sababu ya mashimo? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana ili tuishi vizuri na tuendelee vizuri na watu wengi wamezungumza humu zile barabara nyingi ndiyo maana unatuona tunazungumza hivi kwa sababu barabara zetu nyingi zina changamoto. Namwomba Mheshimiwa Ulega baada ya kutoka hapa babu yangu, yaani yeye ni babu yangu kabisa, lakini ninamwomba atuhakikishie barabara zetu zinakuwa salama kwa muda wote na watu wetu wapite kwa usalama na hata Mheshimiwa Musukuma, msafishaji wa mabasi asafirishe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninamuunga mkono Mheshimiwa Waziri Ulega, bajeti yake ipitishwe kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)