Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Msalala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninapenda nimshukuru na kumpongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Ulega na Naibu Waziri Engineer Kasekenya kwa kutupatia Barabara ya lami kilometa 75, Kahama - Kakola.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hiyo mpaka sasa hivi tayari imekwisha jengwa kwa kiwango cha lami kilometa 25 na mkandarasi yuko site anaendelea, lakini tunashukuru kwa sababu barabara ile ni matokeo ya usimamizi mzuri wa sera ya CSR. Barabara ile inafadhiliwa na Barrick kwa 100%. Kwa hiyo, tuna uhakika barabara ile itakwenda kukamilika bila kusuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenye barabara hii, ninaomba barabara hii ikamilike kwa viwango vyote kama ilivyokuwa designed. Tunaomba taa zote ziwekwe kwenye vijiji vyote ambavyo barabara hii inapita kama ilivyokuwa kwenye mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizi, ninaomba nishukuru kwenye mpango huu wa bajeti wa Wizara ya Ujenzi. Nimeiona barabara ambayo ni barabara inaunganisha Kata Saba, Barabara inayotoka Didia – Chana – Mwankima – Mwakuhenga – Ngaya - Busangi - Ntobo Makao Makuu. Barabara hii kwa mara ya kwanza imeweza kutengewa pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wetu, hizi kata nilizozitaja zote ni kata ambazo zina wakulima wakubwa. Ndizo kata zinazochangia 50% ya mchele katika Mkoa wa Shinyanga. Kwa hiyo, ujenzi wa barabara hii ni wa muhimu sana kwa ajili ya kukuza uchumi wa Mkoa mzima wa Shinyanga, lakini kwa wananchi wa Msalala pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ambayo nimeona kwenye mpango huu ni Barabara ya Kahama – Bulige - Solwa na yenyewe tumeweza kutenga pesa. Barabara ya Nyambula – Chela - Nyang'olongo na yenyewe tumeweza kutenga pesa kilometa 95.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, tunayo changamoto kubwa ya upelekaji wa pesa. Bajeti hii tunayotekeleza Mkoa wa Shinyanga ulitengewa shilingi 12,000,000,000, pesa zilizopelekwa ni shilingi bilioni 1.7 tu mpaka sasa. Kwa hiyo, tunapotenga pesa tutapitisha bajeti hapa, lakini niiombe Wizara ya Fedha wapeleke pesa Wizara ya Ujenzi. Hatuisaidii Wizara ya Ujenzi kwa kuipitishia bajeti halafu tusipeleke pesa kwa ajili ya kutekeleza miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunapopitisha bajeti hapa tunalia kuhusu pesa nyingi kwa ajili ya matengenezo ya barabara zetu, lakini ninajiuliza ni kwa nini, ni kitu gani kinachotusababishia mizigo yetu yote ya transit ambayo inakwenda Nchi za Rwanda, Burundi, Congo na Uganda, kwa nini malori yanaifuata Dar es Salaam wakati tunayo Bandari Kavu pale Isaka na ilishawahi kuwa hivyo huko nyuma? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunaendelea kutumia gharama nyingi za matengenezo ya barabara kipande hiki? Mabilioni na mabilioni tunatenga kila mwaka ya kutengeneza barabara wakati tunazo bandari kavu ambazo zinapunguza msongamano wa malori kwenye barabara zetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kwa nini Wizara ya Uchukuzi - TRC hawaioni hii fursa. Reli ya Kati inafika pale kwenye ile bandari kavu na SGR inapita pale kwenye bandari kavu. Kwa nini Serikali sasa haifikirii kupunguza mzigo kwenye barabara zetu kwa kuanza kutumia bandari kavu ya Isaka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, msongamano wa malori, hivi kweli! Malori kutoka Rwanda, Burundi yanafuata nini Dar es Salaam? Kama waliwahi kukosea huko nyuma walikuwa ni babu zetu, sasa hivi sisi ni vijana tuko kwenye Bunge hili, Serikali ichukue mawazo yetu sisi vijana na sisi tuweze kuokoa Taifa hili, tutumike na sisi kwa wakati wetu wa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutumie njia mbadala ili kuokoa gharama kubwa tunayotumia kwenye matengenezo ya barabara zetu ili sasa pesa yetu tutakayokwenda kuiokoa twende tukaongeze mtandao wa lami kwenye barabara zetu nyingi ambazo sasa hivi ni za changarawe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo mimi kwa kweli kwa barabara hizi ambazo nimepatiwa nimeona kwenye bajeti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)