Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Zuberi Yahya Mfaume

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi. Kwanza, nianze kwa kuipongeza Wizara yenyewe kwa kazi nzuri inayoifanya, lakini zaidi kwa ushirikiano inaotoa kwa sisi Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niweke historia sawa. Sisi Jimbo letu la Morogoro Kusini lina sifa moja, Rais wa Kwanza wa Tanganyika na baadaye Tanzania ndiye aliyekuwa Mbunge wetu wa kwanza. Kwa hiyo, aliingia katika utumishi wa Serikali kuwatumikia wananchi akiwa anatokea Jimbo la Morogoro Kusini japo ni mzaliwa wa Butiama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa kwanza mwanamke wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yeye ni mkulima kutoka Jimbo la Morogoro Kusini. Kwa hiyo, tuna historia ya kuweka viongozi wawili wa kwanza ni Rais wa kwanza akitokea kule kama Mbunge lakini na Rais mwanamke wa kwanza akitokea Morogoro Kusini kama mkulima wa kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Morogoro Kusini tuna kauli mbiu inayosema kila jambo na wakati wake. Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye kampeni pale Ngerengere mwaka jana alituahidi kutujengea Barabara ya Bigwa - Kisaki na ndani ya siku 100 tumeona site clearance na kazi ikawa imeanza. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa juhudi zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ninataka niseme kwamba sisi sote Wabunge hapa tunajua juhudi kubwa anazozifanya Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kila sekta inapata fedha za kutosha, siyo katika elimu, afya na mawasiliano. Ninawaomba tupitishe bajeti hii kwa moyo mmoja na kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia atakuwa wa mwisho kuona barabara za nchi hii zinaharibika na hazitengenezwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe na uhakika kwamba tunakwenda kupata pesa za kutosha kutokana na juhudi zake. Baada ya kusema hayo niiombe sasa Wizara ya Ujenzi kilio chetu kikubwa ni Barabara ya Bigwa – Kisaki, Mheshimiwa Rais ameliona hilo na ndani ya siku 100 ujenzi wa Bigwa – Kisaki umeanza, tumeona pia katika bajeti tuna 2% ya ujenzi. Nimwombe ndugu yangu Mheshimiwa Ulega waende wakaongeze kasi sasa, wananchi wa kule wanalia sana hawana barabara na kwa miaka yote tumekuwa watu wa vilio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna barabara niliyoielezea jana, Barabara ya Msalabani - Tawa, ninaomba wakaharakishe hiyo feasibility study ili waweze kuitafutia pesa na barabara hii ikaanze. Pia, kwa kuwa ninatoka katika Jimbo katika Wilaya ya Morogoro, tuna Barabara inayotoka Ubena Zomozi - Ngerengere, Ngerengere - Tununguo, Tununguo – Mvuha, tunaomba pia barabara hii wakaiangalie. Mkandarasi yuko pale lakini kwa kweli anasuasua. Kazi yake inakwenda polepole sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)