Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpwapwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja hii iliyoko mezani. Kwanza ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye ametupa uhai na afya, tunaendelea na shughuli zetu mahali hapa. Pili, ninampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye anafanya kazi kubwa sana, pamoja na ufinyu wa bajeti ya Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Waziri wa Ujenzi, ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, yeye ni Waziri mzuri. Ni Waziri ambaye anafaa, anafikika. Mara nyingi nimemtafuta, nimempata, amenipa matumaini hata kama ujenzi wa barabara yangu haujaanza, lakini nina matumaini mengi kwa sababu ya usikivu wake, lakini ninampongeza sana Naibu Waziri wake, hata anapojibu maswali hapa Bungeni, utafikiri ni Kamusi ya Barabara na Vichochoro vya nchi hii, hakuna barabara asiyoijua. Tafsiri yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni kwamba, huyu mtu kwanza anazunguka kutembelea barabara, lakini anazijua zote na mwisho anapenda kazi yake. Ninampongeza sana Naibu Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kuchangia. Sisi wa Mpwapwa tuna shida ya barabara mbili; ya kwanza ni Barabara ya kutoka Kongwa kwenda Mpwapwa, yenye urefu wa kilometa 32 na ya pili ni Barabara ya kutoka Mpwapwa kwenda Kibakwe. Barabara hizi ziko katika majimbo yetu mawili; Jimbo la Mpwapwa Mjini na Jimbo la Kibakwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Barabara hii ya kutoka Kongwa kuja Mpwapwa tayari tuna mkandarasi kwenye site, ambaye amekaa pale zaidi ya miaka miwili, lakini kazi haijaanza sababu hajalipwa fedha yake ya awali shilingi bilioni 5.3. Ninataka nikwambie ukweli Mheshimiwa Waziri, uchumi wa wananchi wa Mpwapwa unategemea sana barabara hii. Wananchi wa Mpwapwa wanaishi maisha magumu sana, bei ya vitu madukani iko juu kwa sababu ya usafirishaji wa kutoa bidhaa Dodoma au Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, malori mengi yanayoleta bidhaa hayakubali kufika Mpwapwa kwa sababu ya ubovu wa barabara kwa hiyo, tunaishi maisha ya umaskini kwa sababu ya barabara hiyo, lakini tuna kilimo kule. Wananchi wa Mpwapwa wanalima sana vitunguu na mazao mengine ya biashara, lakini hawawezi kupeleka kwenye masoko kwa sababu, barabara yetu ni mbovu, wasafirishaji hawawezi kuleta magari yao kwenye barabara mbovu na pia, hata wawekezaji hawawezi kuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwenye Wilaya ya Mpwapwa hatuna interaction ya watu wengi kwa sababu ya ubovu wa barabara kwa hiyo, ninasimama hapa kueleza, Mheshimiwa Waziri, Wananchi wa Mpwapwa wanamwangalia Waziri leo, wanamtegemea sana kwamba atawakomboa. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri, akamlipe mkandarasi wa barabara hii, mkandarasi huyo ni mzawa, lakini ni mtu mmoja bora sana katika kazi yake, anajua kazi yake, anachosubiri ni malipo yake ya awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani kubwa sana na Mheshimiwa Waziri na sikusudii kushika shilingi yake, lakini ninaomba sana ajenda hii ya barabara hizi mbili, Barabara ya kutoka Kongwa mpaka Mpwapwa, Mpwapwa mpaka Kibakwe, ziwekwe katika hesabu. Ninaomba sana, atakapo-wind up jioni hii tafadhali awaambie wananchi wa Mpwapwa, barabara hii ni lini itaanza kujengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata habari njema kutoka kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, huko nyuma tulikuwa na kazi nyingi za miradi mikubwa ya kimkakati ilikuwa bado itekelezwe na akatuambia sasa mingi imekwisha, kwa hiyo tunakokwenda huko hali itakuwa tofauti, ninaomba Mheshimiwa Ulega aikumbuke sana barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama yetu Samia anapambana kuboresha Jiji la Dodoma na sisi watu wa Dodoma tunamshukuru sana, lakini ubora wa Jiji hili hauwezi kukamilika kama Wilaya mojawapo katika Wilaya saba za Mkoa wa Dodoma kuwa haina barabara ya lami inayounganisha kutoka wilayani kuja Makao Mkuu ya Mkoa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ulega ajue kwamba ni Wilaya ya Mpwapwa tu ndiyo haijaunganishwa kwa barabara ya lami kutoka Mpwapwa kuja Makao Makuu ya Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la pili, tunalo Daraja maarufu la Godegode. Mheshimiwa Naibu Waziri tuliwahi kufika pamoja, wananchi wakatushangilia wakaona kwamba sasa mwanga umeonekana, lakini toka wakati ule hawajaona chochote. Nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri kwamba, baada ya mvua zilizonyesha miaka miwili au mitatu eneo lile aliloliona sasa limeongezeka kuharibika, limepanuka sana hata survey iliyokuwa imefanyika itabidi ifanyike upya kwa sababu tumechelewa kwenda kulijenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja hili ni muhimu sana kwa Majimbo yetu yote mawili ya Jimbo la Kibakwe na Jimbo la Mpwapwa. Kule Jimbo la Kibakwe kuna wakulima wengi wanaolima mazao ya biashara ya vitunguu, ufuta na mambo mengine, lakini hawawezi kuyaleta Mpwapwa, Dodoma au Dar es Salaam kwa sababu ya daraja hilo. Ikifika masika mawasiliano yanakatika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi huwezi kupita pale maji yanaendelea kupita, lakini wanafunzi wanaacha shule hawawezi kuvuka kwenda shuleni wanakaa nyumbani miezi minne mpaka mitano. Daraja hili tuliambiwa liko kwenye hatua ya manunuzi, lakini mpaka leo hatuoni kinachoendelea.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri azingatie hicho kitu na anapo-wind up, basi atuambie sisi wa Mpwapwa tunategemea kusikia kutoka kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)