Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi. Ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuona watu wa Tarime, Mugumu, Serengeti kupata barabara ya kilometa 87; barabara imeanza ujenzi, imefika Makao Makuu ya Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amefika hivi karibuni akaona, yule mkandarasi anadai shilingi bilioni 4.8 na kule Serengeti mkandarasi aliweka camp na imedondoka, ametoka site. Basi ninaomba atakapopata fedha apeleke, hii kazi iweze kufanyika, tuunganishe Wilaya ya Tarime pamoja na Wilaya ya Serengeti. Watalii wanapata shida sana kutoka kule Mugabili – Nginjanginja; unashangaa namna ambavyo wanachangia mapato, tena in terms of dollar, lakini barabara zetu ni mbovu kiasi kile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo machache ninataka nipitie kwa harakaharaka kwa muda ambao amenipa. Tunazo barabara zetu za Mkoa wa Mara; Barabara ya Musoma – Makojo – Busokero, kwa Mheshimiwa Profesa Muhongo. Barabara ya Musoma – Bunda, ambayo inamuunganisha Mheshimiwa Bulaya na kule Mheshimiwa Kangi Lugola. Barabara ya kutoka Tarime – Serengeti, ambayo nimeitaja mimi na Mheshimiwa Esther Bulaya, Barabara ya kutoka Utegi kwenda mpaka Shirati na Barabara ya kutoka Makutano kwenda Mugumu, Serengeti, ambayo inapita Butiama kwa Baba wa Taifa; hizi ni barabara muhimu sana, zikifunguliwa zitasaidia sana watu wa Mkoa wa Mara kuwasiliana kufanya shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa ambayo nimeisoma hapa, summary ya Kamati, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba, wenyewe wameandika 70% ya barabara zetu ni mbovu, 30% tu ndiyo zina afadhali, lakini 39.4% barabara hizi zimezeeka. Maana yake ni kwamba, haya mambo ambayo wenyewe wataalam wameandika anapokwenda kutafuta fedha ajue kwamba, kuna kazi kubwa ya kufanya ku-maintain barabara hizi ziweze kupitika. Siwezi kurudia kwa sababu, Waheshimiwa Wabunge wametaja kila mkoa na kwa kweli, maeneo haya ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri ana kazi ya ziada hapa, ziko barabara, kwa mfano Barabara kutoka Iringa – Dodoma, barabara hii hata kabla ya muda wake kwisha imeharibika. Barabara kutoka pale Mwigumbi – Maswa – Bariadi, mkandarasi hatoki site, haifanyi kazi, achilia mbali hii shida ya Singida – Babati – Arusha. Sasa Mheshimiwa Waziri hawa watu ambao wanajenga hizi barabara, zinaharibika kabla ya muda, unachukua hatua gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, unapeleka fedha kujenga barabara, kabla hajaikabidhi, barabara ni mbovu na hatujawahi kuona mtu amepelekwa mahakamani, amewajibishwa au ametaifishwa mali. Wanapoteza fedha za wananchi, lazima Bunge hili liweke mpango mkakati, watu ambao wanajenga barabara chini ya kiwango. Tusiishie kutafuta fedha na kupeleka, watuambie kwa nini wanajenga barabara chini ya kiwango?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawawajibishwe, watoe mfano kwa mtu mmoja tu. Mtu akafilisiwa kwa kuharibu fedha za Watanzania watashika adabu na mtu akipewa kazi atafanya. Barabara zingine zipo, kwa mfano kutoka pale Bunda mpaka Sirari, miaka nenda miaka rudi utafikiri imejengwa jana; hawa wakandarasi wapo na hii inazua maswali mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ninataka niiseme hapa ni tunayo Sheria ya Mwaka 2019 ile, ambayo inazungumzia Mfuko wa Barabara. Tufanye mambo mawili; moja ni, kama kuna mianya, kuna matobomatobo pale tuyazibe, fedha ile ikitengwa iende moja kwa moja kwenye kazi ambayo tumekusudia hapa kutenda. La pili ni, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, fedha zote ambazo zilitakiwa ziende Mwaka 2024/2025 walipeleka 35%. 35% hii iende ikajenge barabara zetu! Mwaka 2025/2026 ni 44%, kuna 54% haijaenda! Fedha hizi zikienda zitasaidia sana hizi barabara ambazo kila Mbunge anataka barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mapendekezo, ile habari ya kuchukua asilimia tano ikafanye kazi zingine, mimi siungi mkono, fedha hii yote iende kwenye barabara. Mapendekezo ya Kamati yote ninayaunga mkono, lakini hili la tozo! Sasa hivi kuna mambo haya ya mafuta, maisha yamekuwa magumu, wananchi wanalalamika, hatuwezi kuongeza mambo ya tozo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, TRA kwa taarifa zao wenyewe hawajafikisha 60% ya makusanyo kwa vyanzo halali. Ninauliza Waheshimiwa Wabunge humu ndani, wanafanya manunuzi, wangapi wanapewa risiti na wangapi wanadai risiti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda hapo center tu, mtu ananunua simu ya shilingi 3,000,000 au 4,000,000, hakuna risiti. Maana yake ni kwamba, hapo kodi ya Serikali haipo, kwa hiyo, kuna mianya mingi ya usimamizi wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha na watumishi wake na TRA wanakusanya kodi. Kodi ikikusanywa shida pia ya Watanzania, tupunguze mambo ya anasa, maneno ya mzahamzaha kwa matumizi ya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ikikusanywa Watanzania wanataka kuona, tumesema tunajenga barabara, kusanya fedha, jenga barabara. Kama ni fedha ya umeme, kusanya fedha, nenda kwenye umeme. Watanzania wakigundua kama fedha yao wanayotoa inafanya kazi iliyokusudiwa, hawatapinga mipango ya Serikali, watatuunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeenda hata Marekani pale, mama ntilie tu anauza chipsi ana computer, anatoa risiti ya mashine, analipia na usipolipia kodi wanakuona wewe ni mkosefu. Sisi hapa mtu asipolipa kodi ndiyo mjanja, anayelipa kodi analalamika, hatuwezi kuwa na double standard. Kila mtu ambaye anapaswa kulipa kodi, alipe kodi na fedha ikikusanywa ifanye kazi ambayo tumekusudia, tuwaondoe Watanzania kwa mambo ya mzahamzaha haya, itatusaidia sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango wako.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sekunde moja nimalizie. Ninaomba nimpe kazi Mheshimiwa Waziri, hii habari ya madeni na riba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mianya, wanatengeneza mikataba, wanawaambia nikichelewa kulipa fedha nitakulipa riba! Mikataba hii wanatengeneza wenyewe, wabadilisheni mikataba ile. Hii habari ya madeni na riba inaweza ikawa ni uchochoro fulani, 10% mikataba ya uongo uongo ibadilishwe.