Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buhigwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PIUS Z. YANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nichangie hiyo hotuba ya bajeti ya ujenzi. Awali ya yote ninaomba kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwezesha kufungua Mkoa wa Kigoma na kuwezesha miundombinu mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka wakati wa ziara yake ya kugombea uchaguzi uliopita, aliweza kutamka neno moja muhimu sana. Akasema, mikoa ya pembezoni siyo ya pembezoni tena, ni mikoa ambayo ni ya kimkakati kwa hiyo, yuko tayari kuweza kuifungua, ili kwa kweli, iweze kuchangia katika maendeleo ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hilo kwa sababu, ule ulikuwa ni mkoa ambao kwa kweli, tukizungumzia miundombinu, mkoa ule ulikuwa katika hali mbaya sana. Kwa mara ya kwanza ni kipindi ambacho tulianza kupata Barabara kutoka Tabora kwenda Kigoma mpaka Kasulu, lakini barabara ya pili, ambayo tuliipata hivi karibuni inatoka Nyakanazi – Kibondo – Kasulu mpaka mpakani mwa Tanzania na Burundi. Hiyo barabara imeweza kufungua milango mikubwa sana huko, lakini kana kwamba haitoshi, kuna ujenzi ambao unaendelea pia, wa Kituo cha Forodha cha pamoja ambacho na chenyewe kitafungua milango ya kiuchumi kati ya Tanzania na Burundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uwekezaji huo bado kuna changamoto chache ambazo tunahitaji kuziangalia. Kwa mfano, ile Barabara ya Nyakanazi mpaka mpakani mwa Burundi, kupitia Buhigwe, maeneo makubwa hayajawa na barabara na taa za barabarani, ikiwemo Buhigwe Center na vijiji vyote kandokando ya hiyo barabara, lakini changamoto nyingine ni vijiji vilivyoko jirani na Buhigwe; kwamba ile barabara ina mifereji mikubwa sana, hawajaweka matoleo ya wananchi kuweza kutoka barabarani kuvuka kwenda kwenye makazi yao. Kwa hiyo, inabidi wazunguke eneo kubwa sana, mbali, ili kuweza kuvuka ile mifereji. Sasa ni ombi langu kwa Wizara husika kuwezesha hilo liweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ziara ya kampeni ya kuomba kura kwa wananchi, Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Kalela – Buhigwe mpaka Muyama – Mugera na kuelekea Kibondo. Juzijuzi wananchi waliona kibao kikubwa kimewekwa, kwa ajili ya ujenzi wakafikiri sasa ule ujenzi wa lami unaanza na walianza kusherehekea, kesho yake nikawaambia wapige picha wanitumie, lakini walipotuma tukakuta kwamba, kumbe ni ukarabati wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walinyong'onyea pamoja na kwamba, jana yake walikuwa wanasherehekea. Sasa ombi langu, kwa niaba ya Wanabuhigwe, ile ni barabara ya kimkakati, ambayo inaunganisha kata zaidi ya 10 kati ya 20 na inakuja kuungana na Wilaya ya Kibondo na Kakonko. Kwa hiyo, ninaomba pia, Wizara iweze kufikiria na kuona ni jinsi gani inaweza kuwezesha hilo jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Barabara ambayo inatoka Makere na kwenda kuungana na hiyo barabara nyingine. Hiyo pia, tutafurahi kuona kwamba, inaanza kufikiriwa kuwekewa lami, ili wananchi waweze kupata nafuu ya kutembea kutoka maeneo mengine kwa shughuli za kiuchumi na za kijamii pia. Itakuwa ni rahisi kwa wananchi kwenda kupata huduma kwenye vituo vya afya na pia, hata hospitali kubwa za wilaya. Sasa maombi yangu kwa Wizara husika ni waangalie ni jinsi gani waweze kulifanyia kazi hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni kubwa zaidi ni, tunazungumza barabara zinajengwa, kesho yake zinaanza kuharibika. Kuna sababu moja ya msingi ambayo inabidi pia tuifikirie, mabadiliko ya tabianchi yanabadilisha mfumo wa mvua. Kwamba, mwaka hadi mwaka kiasi cha mvua kinachonyesha ndani ya muda mfupi kinazidi kuwa kingi, sasa maji yakituama kwenye barabara ambayo imejengwa, ya lami, kwa vyovyote vile lazima ibomoke. Sasa ninachotaka kupendekeza ni kwamba, tufike mahali tusitumie design ya business as usual kwenye design stage, tuanze kufikiria business unusual, ambapo suala la mabadiliko ya tabianchi liweze kuhusishwa kwenye design za barabara hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa nimesema hayo, ninaunga mkono hoja iliyoko hapo mbele yetu. Ahsante sana.