Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Yohana Stephen Msita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itigi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. YOHANA S. MSITA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii adhimu sana. Nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ametukumbuka sana watu wa Jimbo la Itigi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Itigi kwangu Mjini tuna kilometa 10 za barabara ya lami. Jambo ambalo kwa kweli hapo nyuma lilikuwa ni hadithi. Nikushukuru sana Mheshimiwa Rais, nikushukuru sana Waziri wa Ujenzi kwa kazi kubwa ambayo imefanyika pale, mabilioni ya fedha yamelala pale kwenye Jimbo langu la Itigi pale mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru pia maana nisiposhukuru nitakuwa ninajifunza roho mbaya na mimi bado kijana. Tuna kilometa 25 ambazo zinatoka Noranga mpaka Itigi, hii Barabara kubwa ya kwenda Rungwa mpaka Makongolosi. Tayari kilometa 25 zimekamilika na mkandarasi saa hizi yupo site anafanya finishing kumalizia ile barabara. Tunashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninataka nizungumzie Barabara hii ya kutoka Mkiwa - Itigi kuelekea Rungwa - Makongolosi ambayo kwa kweli barabara hii ndiyo imebeba uchumi mkubwa, ndiyo imebeba siasa kubwa sana ya Jimbo la Itigi. Hii barabara ya kutoka Mkiwa mpaka Makongolosi takriban kilometa 356. Ni kipande kidogo tu cha kilometa 25 ndiyo kimekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimeona kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri kwamba, wametenga bajeti, kwa ajili ya mwaka huu wa fedha takribani shilingi 6,000,000,000, lakini bado fedha hii haitoshi kwa sababu, hii barabara inaunganisha Mikoa karibu sita ya Singida, Tabora, Katavi, Songwe, Mbeya. Ili tuweze kutengeneza uchumi lazima tuhakikishe hii barabara yenye urefu wa kilometa 356 ikamilike kwa kiwango cha lami; imekuwepo kwenye ilani karibu awamu tatu tangu 2015, 2020 na sasa 2025 kwenda 2030, bado barabara hii imekuwa ni kizungumkuti, haijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema tu, Itigi pale ndiyo kitovu hasa, watu wanaotoka Tabora, watu wanaotoka Mbeya, watakutana pale, kwa ajili ya kupanda treni ya mwendokasi kwa sababu, Stesheni kubwa sana ya SGR pale inakwenda kujengwa. Kwa hiyo, tunakwenda kuifungua nchi yetu kutoka Nchi za Zambia, Malawi na kadhalika na ile mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yote itapita kupitia Itigi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema tu, kama barabara hii itakamilika maana yake ni kwa miaka mitano tutakuwa tumeokoa takribani shilingi 40,000,000,000 kwa sababu, mtu anapotoka Mbeya akazungukia hii Barabara ya Iringa kuja Dodoma anakuwa ametembea zaidi ya kilometa 300 mpaka 400, wakati angepita hii ya kutokea Makongolosi kuja Itigi angeokoa kilometa 300. Sasa ukifanya rate utakuta gari moja likitembea kilometa 300 litatumia karibu lita mia moja za mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukitumia lita 100 za mafuta unazungumzia karibu shilingi 450,000. Hiyo ni kwa lori moja, maana yake ni ukiwa na malori 50 kwa siku, unazungumzia umepoteza fedha shilingi 22,500,000 kwa mwezi tutakuwa tumepoteza shilingi 675,000,000. Kwa mwaka tutakuwa tumepoteza shilingi 8,100,000,000 kwa miaka mitano tutakuwa tumepoteza jumla ya shilingi 40,500,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunatenga shilingi 6,000,000,000, lakini tunakwenda kupoteza shilingi 8,000,000,000 kwa mwaka. Ninadhani hii barabara sasa, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha, atuambie Barabara kutoka Noranga kuelekea Rungwa kuelekea Makongolosi, bado hatuna mkandarasi pale. Imefanyiwa upembuzi, imefanyiwa usanifu, lakini bado hayupo mkandarasi wa kujenga ile barabara. Sisi barabara ile ndiyo imeibeba uchumi, ndiyo imeibeba siasa ya Jimbo la Itigi. Ninaiomba sana Serikali, hii barabara tuitazame kwa macho mawili, ili tuitengee fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema tu hapa na tunakubaliana na Wabunge wenzangu kwamba, Wizara ya Fedha hata tungesema mpaka jioni hapa, kama Wizara hii haiongezewi fedha! Tukate matumizi mengine mahali pengine, ili tuiongezee fedha, shilingi trilioni 2.5, bado haitoshelezi kwenye ukarabati wa ujenzi wa barabara za nchi hii. Ninaomba sana Wabunge wenzangu tuungane pamoja, ili tuweze kuiambia Serikali iongeze fedha kwenye Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha nasema tu kwamba, sisi tunaunga juhudi za Serikali mkono, jinsi ambavyo inaendelea kupambana na ujenzi wa barabara na marekebisho ya barabara. Wabunge wote tunakubaliana hapa kwamba, upitaji wa barabara umekuwa ni mgumu sana, barabara zimechimbika, kuna mahali barabara hazipitiki. Leo mazao yanashindwa kusafirishwa, watu wanapata changamoto barabarani, wagonjwa wanapoteza maisha, changamoto kubwa ni hii barabara. Nchi ili iweze kukua kiuchumi ni lazima ihakikishe miundombinu ya barabara inapitika vizuri, ili uweze kwenda kwenye uchumi mkubwa ambao tunautarajia kwenye Dira ya 2050.

Mheshimiwa Mwenyekiti baada ya maneno hayo, ninakushukuru sana kwa nafasi, lakini ninaomba tujifunze kwa Mataifa mengine katika kusimamia matumizi ya fedha za barabara zinazopelekwa kule kwa wakandarasi na kuzingatia ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, ninakushukuru sana, ninaamini Itigi baada ya mwaka mmoja sasa inakwenda kung’aa. Ninaunga mkono hoja. Ahsante sana.