Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kupata fursa hii ya kuchangia hotuba ya bajeti hii muhimu ya Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wasaa huu na dakika hizi katika wakati wote tukiwa kwenye hivi vikao vya bajeti, leo hii Jimbo la Mbeya Vijijini takriban wananchi 500,000 wamenyamaza kimya kusikiliza juu ya mustakabali wa barabara zao za kimkakati, barabara tatu. Nami ninaomba niseme kwa niaba yao. Barabara ya Mbalizi - Shigamba nimepitia bajeti vizuri barabara hii ipo, ninaishukuru Serikali. Barabara ya Isyonje - Kikondo mpaka Makete nimepitia vizuri bajeti hii barabara hii ipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mbalizi - Chang’ombe inayoenda Mkwajuni - Makongolosi mpaka kuunganisha mikoa ya karibu Singida mpaka Tabora nimepita vizuri bajeti hii barabara hii ipo. Kwa heshima kubwa ninaomba niiombe Serikali kuwepo kwenye bajeti barabara hizi ni jambo moja. Sasa baada ya Wanambeya Vijijini kusubiri kwa zaidi ya miongo mitatu, niisihi sana Serikali yangu barabara hizi zikajengwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hizi Barabara, lakini ninaomba niseme jambo moja, niliuliza swali la nyongeza kupitia Wizara hii ya Ujenzi; Barabara ya Mbalizi Shigamba. Nikajibiwa kwamba mwaka huu tumepewa kilometa 10. Ninaomba Mheshimiwa Waziri kaka yangu Ulega, sina shaka naye na yeye ndiye Waziri pekee ambaye ameapishwa tu amefika jimboni kwangu Mbeya Vijijini pale Songwe. Kwa hiyo, sina shaka na utendaji wake, ninaomba hizi kilometa 10 zianze haraka vile inavyowezekana twende tukawafute vumbi Wanambeya Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na barabara hii Mkoa wa Mbeya, mkoa ambao ni mkoa wa tatu kwa kuchangia pato la Taifa, nyuma ya Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanza, barabara zake zimekuwa katika hali mbaya sana. Ninaomba nichukue fursa hii kwa moyo wa unyenyekevu mkubwa kumshukuru sana Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, baada ya kelele nyingi za Wanambeya Vijijini ametufuta mavumbi, ametupatia fedha zaidi ya 4,000,000,000 ambazo zimemrudisha mkandarasi site. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la msingi kwenye jambo hili. Ninaomba Mheshimiwa Waziri mkandarasi huyu asimamiwe asiondoke site tena ikiwa ni pamoja na kumaliza certificates zake anazodai zaidi ya shilingi 4,000,000,000 zingine ili aongeze kasi ya kutengeneza barabara hii Wanambeya waondokane na hii adha ya vumbi ambayo wameipata kwa zaidi ya miezi minne sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nishauri hapa Jiji la Mbeya lina barabara moja tu, ile highway ambayo ni TANZAM. Mheshimiwa Waziri kwa kuwa wamekuja kupitia TANROADS na mpango wa kutengeneza barabara ya mchepuo; na hapa nimpongeze sana Engineer Bishanga, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya kwa usimamizi wake makini sana. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri ile barabara ya mchepuo kutoka Uyole kupitia Kata ya Swaya inaenda kutokea Songwe ianze sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, ile barabara ikianza itapunguza msongamano katikati ya Jiji la Mbeya. Jambo la pili, itaharakisha matengenezo ya barabara sababu magari pale katikati yatakuwa machache; na jambo la tatu na la muhimu, itafanya hizi barabara zidumu kwa sababu yale malori makubwa yatapita kwenye hii njia ya mchepuko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba nishauri jambo lingine la msingi. Serikali hii tunatambua jitihada kubwa zinazofanywa kuwaletea maendeleo Watanzania hususani hapa kwenye uwekezaji wa miundombinu kwenye nchi yetu hasa barabara zaidi ya 40,000,000,000,000 sasa zimewekezwa. Ni dhahiri kwamba uwekezaji huu uende sambamba na maono ya usimamizi wa quality ya hizi barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri jambo moja; ninaomba Serikali ione haja ya kutenganisha majukumu ya usimamizi wa quality ya barabara pamoja na majukumu ya utengenezaji wa barabara. Niishauri Serikali kuona haja ya kuunda chombo mahsusi kinachojitegemea cha usimamizi wa quality za hizi barabara zinazojengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto kubwa na Waheshimiwa Wabunge watakubaliana na mimi, barabara zetu zinatengenezwa baada ya muda mfupi zinaharibika. Sasa tuliondolee jukumu hili la usimamizi wa TANROADS. TANROADS ibaki na jukumu la utengenezaji wa Barabara, lakini usimamizi wa quality wa zile barabara kuwepo kuna agency inayojitegemea na hii agency iwe na watumishi ambao ni well vetted na hawana mashaka yoyote na uzalendo wao wa juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba nihitimishe na jambo moja la msingi na kwa kifupi sana kwa dakika moja. Miaka ya 1990 ninakumbuka magari yote nchi yetu yalikuwa yanasajiliwa kimkoa, lakini nimebahatika kutembelea Nchi ya South Africa nimeona magari yanasajiliwa GP, Gauteng yanasajiliwa kimkoa au ki-province.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ninalolitazama.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante kwa mchango wako muda wako umekwisha.
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaomba niunge mkono hoja. (Makofi)