Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2026/2027.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu na baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu. Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, nichukue nafasi hii kumpongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kufanya mageuzi ya kiuchumi nchini kwetu, lakini katika kuhakikisha tunaendelea kuunganisha mikoa kwa kiwango cha barabara za lami lakini pia tunaunganisha kupitia reli pamoja na anga. Haya ni mageuzi makubwa na hatua kubwa kabisa katika Nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri kweli nimeamini; umoja wa vijana ni tanuri la kupika na kuoka viongozi na ndiyo maana leo Mheshimiwa Waziri Abdallah Ulega ameiva katika Wizara hii na katika kuhakikisha kwamba anatutumikia sisi Watanzania na kutusikiliza sisi wawakilishi wa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri bila kusahau Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na watumishi wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nichukue nafasi ya kumpongeza sana Meneja wetu wa Mkoa ndugu yetu Masele kwa kazi kubwa ambazo anazozifanya: Meneja wa TANROADS Mkoa pamoja na timu nzima ya TANROADS, Mkoa wa Manyara, bila kumsahau Meneja wa TARURA Mkoa pamoja na Meneja wa TARURA na watumishi wote wa TANROADS pamoja na TARURA katika Mkoa wa Manyara na hususani Jimbo la Hanang.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Manyara una takriban ya barabara zinazosimamiwa na TANROADS kilometa 1,657 lakini katika kilometa hizi tuna kilometa 257. Kati ya kilometa hizi 257 sisi kama Mkoa wa Manyara tuna kilometa 52 pekee za lami. Kilometa 257 ni kilometa zinazounganisha Mkoa wa Manyara, Babati - Dodoma, Babati - Singida, Babati - Arusha zinasababisha kuwa na kilometa 257, lakini ukiingia ndani ya mkoa tayari sisi tuna kilometa 52.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Manyara tuna uchumi wa kutosha. Tuna imani sisi Wanamanyara na wananchi wametutuma hapa tuje tuipishe Serikali bajeti hii, lakini tuombe kwamba watuondoe kwenye kilometa 52 za barabara watuongezee tuwe na mtandao mkubwa wa barabara na sisi tunufaike na mema ya Nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara ya muhimu sana inayopita katika Mkoa wa Manyara. Barabara inayounganisha Mkoa wa Manyara na mikoa yote ya Tanzania, lakini Mkoa wa Manyara, Nchi ya Tanzania pamoja na nchi zingine za jirani. Kipande cha Barabara ya Dareda mpaka Gehandu yenye kilometa 82 kwa sasa kipande hiki kimeharibika, kimechakaa, tumekwishafanya marekebisho ya mara kwa mara, tumekwishaweka viraka mara kwa mara, lakini na viraka kwa sasa vimekataa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna imani tunakwenda kupitisha bajeti tunaomba tupewe fedha tukaikomboe barabara hii ya msingi na ya umuhimu katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo Bandari ya Tanga ambayo kwa sasa hivi inatuletea fedha za kigeni, lakini fedha zenyewe za nchi yetu ya Tanzania. Kama haitoshi Mkoa wa Manyara hususani Wilaya ya Hanang tunapokea magari ya kutosha kwa ajili ya mazao. Tuna chumvi ya kutosha, dhahabu pia ipo na uchumi mkubwa. Tunaomba sana ndani ya Wizara ya Ujenzi leo akianza Dar es Salaam, aje Tanga, aje Kilimanjaro, aje Arusha, aje Manyara atoke aende Singida mpaka Mwanza hakuna kipande kibovu kilichoharibika zaidi kama kipande cha kilometa 82, kipande cha kutoka Dareda mpaka Gehandu. Mheshimiwa Ulega is my brother, yeye ni Youth League mwenzangu ninamhakikisha siwezi kuishika shilingi yake kwa sababu ninahitaji fedha, wananchi wa Hanang wamenituma, akina mama, akina baba, vijana, wazee, lakini viongozi wote wa dini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Hanang wamenituma wanaomba sana, wana mapenzi mema na Serikali yao, wanatambua kazi ambazo zimefanyika kwenye vituo vya afya, elimu, maji na miundombinu mingine na sasa ni zamu yetu tukitengeneze kipande hiki ili tuweze kuupata uchumi na watu wetu wapite kwa masaa yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kabisa ukiachana na hiki kipande cha national road ambacho kinaunganisha Mkoa wa Manyara na mikoa mingine lakini Mkoa wa Manyara na nchi zingine. Sisi Wanahanang tuna kipande cha barabara kinachoitwa Mogitu - Haydom chenye kilometa 68. Kipande hiki cha barabara kipo katika awamu zote kwenye Ilani za uchaguzi na hata sasa nje ya Ilani ya Uchaguzi bado imekuwa ni ahadi ya viongozi wetu wakuu wa nchi. Tunaiomba sana Serikali, kipande hiki mwaka 2016 upembuzi yakinifu ulianza; 2016 mpaka sasa 2026 ni takriban miaka 10. Tumeona tumewekwa kwenye mpango lakini mwendelezo wa upembuzi yakinifu. Tunaomba sana kwa mara ya kwanza na sisi tupate hata lami kilometa moja ya kuanzia licha ya 68 ambazo tunazihitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu umekwishachukua takribani miaka 10, sasa wananchi wa Hanang wanasubiri lami kwa heshima na unyenyekevu mkubwa sana kwa sababu ni wakulima wazuri, wana uchumi mkubwa wa nchi hii, magari yanaingia ya kutosha na sisi katika Taifa letu tuweze kuchangia mapato yale ili yaweze kufanya kazi ya kufanya maendeleo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo barabara ya kimkakati. Wanaposimama hapa Wabunge kuongelea habari ya Barabara ya Sibiti inayokwenda Simiyu, barabara hii ni nyepesi sana. Kuna Barabara ya kutoka Nangwa - Gisambalang kuja Daraja la Munguri, Mkoa wa Dodoma, Jimbo la Kondoa. Hii ni barabara nyepesi sana itakayounganisha Mkoa wa Dodoma, Mkoa wa Manyara pamoja na mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa maana ya Simiyu, Mara na mikoa mingine. Barabara hii ina jumla ya kilometa 79. Tunaomba sana imekuwepo kwenye Ilani, imeanza upembuzi yakinifu, ni ahadi ya viongozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa barabara hii iweze kufanyiwa kazi...
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Asia Halamga kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mariam Ditopile.
TAARIFA
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. Ninaomba kumpa taarifa Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Hanang.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara anayoizungumzia inayounganisha Jimbo la Hanang kwa maana Mkoa wa Manyara na Jimbo la Kondoa Mjini kwa maana ya Mkoa wa Dodoma ni kweli pamoja na kilometa hizo 70 pia linajumuisha daraja ambalo ni la msingi na daraja hili limevunjika miaka 15 iliyopita, Daraja la Munguri B.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapojibu na taarifa ninamwongezea tu kwamba upembuzi yakinifu tayari na vilevile Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatoa kauli kule kwamba daraja hili na barabara hii litajengwa kwa kiwango hicho cha lami.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Asia unaipokea taarifa hiyo?
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni lazima niipokee kwa mikono yote miwili na mimi ninaendelea kupiga dua kwamba fedha zipatikane, tupitishe hapa bajeti na tuweze kujenga barabara hii ni kiunganishi kikubwa sana cha uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi nilichotaka kuomba ni Barabara ya Mogitu - Haydom kilometa 68, lakini Dareda - Gehandu kilometa 82, lakini Nangwa kwenda Daraja la Munguri kilometa 79. Bila kusahau mkoa wetu una kilometa 52 tu, tuna mapenzi makubwa, tuna imani kubwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Mheshimiwa Rais amejenga vituo vya afya, amejenga majengo kama uyoga, hatuna hofu wala shaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishapitisha bajeti hapa ninamwomba sana Mheshimiwa Ulega, wananchi wa Hanang wapo tayari kupokea mema ya nchi na wanapenda chama hiki na wanapenda Serikali hii na wanampenda Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tuna imani kubwa kwa matunda ambayo ametupatia miaka mitano iliyopita, hatuna hofu na 2026/2030. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.