Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilwa Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KINJEKITILE N. MWIRU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo kunifikisha hapa niweze kuongea. Pili ningependa kumshukuru Mheshimiwa Rais wangu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu, kwa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya kisasa katika Wilaya yetu ya Kilwa ambayo ni jambo ambalo watu wa Kilwa wanamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ningependa kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia, kwa madaraja, sasa hivi kusini na wilaya yangu ya Kilwa hakuna tena mambo ya daraja kuvunjika, watu kulala njiani, mambo hayo yamekwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijikite kwenye hoja zangu tatu. Kwanza ni Barabara yetu ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mnazi Mmoja – Lindi. Hii barabara haifai, haifai kabisa yaani imekwisha. Haiwezi hata kuwa repaired tena, Mheshimiwa Dkt. Samia ametujengea madaraja mazuri sana, lakini barabara haifai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Kilwa mpaka Dar es Salaam ni kilometa 330, basi linatumia masaa nane mpaka tisa, jamani wananchi wanateseka sana. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri aangalie huko kwenye jungu kuu tunaweza tukaanza vipi kuitengea hela hii barabara. Kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, atupe maelezo yanayoeleweka kuhusu Barabara hii tunafanya nini kuanza kuirekebisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya pili Mheshimiwa Waziri anaifahamu sana Barabara ya Nangurukulu Zinga - Liwale. Mheshimiwa hii barabara haifai jamani kama mnabisha naombeni wabunge twende tufanye ziara kule watu wanateseka mpaka leo miaka yote ya uhuru watu wanalala njiani. Mimi mwenyewe Mheshimiwa Mbunge ninalala njiani, haifai kabisa ile barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, ninajua nimepata lami kilometa 72 zinaanzia Liwale lakini tuangalie huku Ngea – Miguruwe - Njinjo tunafanya nini ili watu wapite mwaka mzima wakati tunatafuta pesa za kuimalizia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya mwisho ni Barabara ya kutoka Tingi Njianne kwenda Kipatimu. Hii barabara juzi ndiyo imeweza kufunguka kuwa na mabasi ya kufika Kipatimu. Mabasi yalikuwa yanaishia Chumo na Mheshimiwa Waziri anajua kule kuna wazee, kuna wagonjwa, unavyoanza kusema kwamba wapande boda boda au wabebwe kichwani mpaka Chumo ndiyo wapande mabasi ni tatizo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anaifahamu sana Kilwa nikigombea naye anaweza akanishinda kwa vile anavyojulikana katika Wilaya ya Kilwa, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, aifikirie hii barabara iweze kupitika wakati ule utaratibu wetu wa lami unakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ninamwomba Mheshimiwa Waziri taa katika kata zangu za Kilwa; Kata ya Mingumbi, Chumo na Mayuni Kipatimu, Njinjo na Miguruwe ninamwomba Mheshimiwa Waziri basi hata watu waone wakitembeatembea hivi wakati wanasubiri mambo mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana. (Makofi)