Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Charles Jacob Sungura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. CHARLES J. SUNGURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi. Kwanza nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu Mkoa wa Tanga umetengewa takribani shilingi 78,000,000,000 kwa ajili ya ukarabati wa uwanja wetu wa ndege. Fedha hizi zitasaidia katika upanuzi wa uwanja ule kwa sababu mpaka dakika hii eneo la kutua na kurukia ndege ni meta 1,268 ambazo zilisababisha mpaka ndege kubwa zitakuwa hazitui pale Tanga lakini kwa fedha hizi tayari itaweza kuongeza mpaka meta 2,500 takribani kilometa 2.5 ambayo itawezesha kutua kwa ndege kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, fedha hizi pia zitasaidia katika ujenzi wa eneo la kuegesha ndege, pia ujenzi wa jengo jipya la abiria pamoja na mnara wa kuongozea ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu utakapokamilika utasaidia sana wananchi wa Mkoa wa Tanga hasa katika kukuza utalii pamoja na kuchochea biashara katika Mkoa wetu wa Tanga. Kwa maana hiyo ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu ya fedha hizi shilingi 78,000,000,000 ambazo zitakwenda kusaidia kukuza utalii pamoja na biashara katika mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sasa nijikite katika barabara zetu za kimkakati. Ukiangalia Mkoa wa Tanga tuna hii Barabara yetu ya Tanga – Segera - Chalinze. Barabara hii ni mshipa mkubwa sana katika maendeleo ya Mkoa wetu wa Tanga na Jimbo la Handeni. Kwa sababu barabara hii si kwamba tu inaunganisha mkoa na mkoa, lakini pia inaunganisha Tanzania na Nchi ya jirani ya Kenya, kwa maana hiyo ni barabara muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano sasa hivi ukiangalia Bandari ya Tanga imetanuka, kutanuka kwa Bandari ya Tanga kunaongeza msongamano mkubwa wa maroli katika Barabara yetu ile ya Segera - Tanga - Chalinze. Kwa maana hiyo ninamwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aje na maelezo yaliyonyooka ya kwamba ni lini miradi hii itaanza ili kuhakikisha barabara hii inaongezeka, lakini pia inatanuliwa kutoka njia mbili kuwa njia nne.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ninaomba Waziri atambue kwamba Ukanda wetu wa Pwani kuanzia Chalinze, Mkata, kwa Msisi, kwenda Kwedizinga, Kabuku, Segera mpaka Tanga ni ukanda ambao una viwanda, ni ushoroba ambao una viwanda vingi. Katika kongani za viwanda za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anakwenda jenga viwanda vingine zaidi katika ukanda ule kwa maana hiyo tutegemee kuongezeka kwa malori mengi sana mbali na haya ambayo yanatoka katika bandari zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo ninaomba kumsisitiza Mheshimiwa Waziri, atakapokuja atupe uhakika namna gani hii barabara itaenda kujengwa na lini itaenda kujengwa. Barabara hii ni East African Highway nilishasema mwanzo inaunganisha Nchi jirani ya Kenya kupitia Handeni kwa maana hiyo bado umuhimu wake ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mbali na hapo barabara hii inaruhusu magari yanayotoka upande wa kaskazini kwa maana ya Kilimanjaro na Arusha yanapita katika njia ile, hivyo msongamano bado ni mkubwa zaidi. Ninaomba atakapokuja pia atupe maelezo yaliyonyooka, sina lengo la kushika shilingi, lakini nataka maelezo yaliyonyooka. Ni lini barabara hii itajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo Barabara nyingine kutoka Handeni - Mziha - Turiani yenye kilometa 108. Barabara hii ni shortcut ya usafiri wa mizigo kutoka Bandari ya Tanga kama nilivyosema, lakini pia na maeneo mengine ya kaskazini kwa maana ya Arusha na Kilimanjaro barabara hii itasaidia kurahisisha usafiri wa mtu ambaye anazunguka kupitia Chalinze mpaka Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, barabara hii ikitengenezwa inakuwa ni shortcut. Kwa mfano mtu anayetoka Handeni apitie Chalinze mpaka Morogoro mpaka Dumila atatumia takribani masaa sita na nusu, lakini kama itawekwa lami mtu atatoka Handeni mpaka Dumila atatumia masaa mawili na nusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo tuiangalie hii barabara kwa jicho la kiuchumi kwa sababu ni barabara muhimu sana na pia itachagiza sana mizigo inayotoka kwenye Bandari yetu ya Tanga itapita katika barabara hii lakini pia itaenda maeneo mengine ya Iringa na maeneo mengine ya Nyanda za Juu Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara nyingine ninaomba niizungumzie, ipo barabara inayotoka Mkata - Pozo - Kwa Msisi. Barabara hii inasikitika kwamba ni miongoni mwa barabara za RISE za World Bank, lakini mpaka dakika hii sijaona Wizara kama wameitangaza. Kwa hiyo, ninaomba anapokuja kwenye majumuisho atuambie ni lini atatangaza barabara hii ili zabuni itangazwe na iweze kujengwa wananchi wangu wa Kwamkata Kwamsisi na Pozo waweze kunufaika. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. DKT. CHARLES J. SUNGURA: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho kabisa…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, muda wako umekwisha malizia.

MHE. DKT. CHARLES J. SUNGURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana. Lipo Daraja la Mto Mligazi, daraja hili linaunganisha Kata ya Kwasunga pamoja na Kata ya Miono. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa sababu ameshalitembelea na nimeshamletea BOQ ya shilingi 989,000,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba sasa kwenye majumuisho yake aniambie kama mwaka huu kama alivyoahidi atalijenga daraja lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)