Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Patrick Adkin Mwalunenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara yetu ya Ujenzi. Kwanza kabisa ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa maono yake na kutupa barabara kile kipande cha njia nne pale Mbeya Mjini kuanzia Jimbo la Uyole mpaka Ifisi, ninampongeza sana kwa niaba ya Wanambeya, ninaomba Waheshimiwa Wabunge tumpigie makofi sana Mheshimiwa Rais kwa sababu barabara ile ni barabara ya uchumi karibu 60% ya mizigo inayotoka bandarini inapita kwenye ile barabara. Kwa maana yake ni kwamba kama ni pesa tunazitafuta basi ziko kwenye barabara ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri na nimeona kwenye vitabu vyake amesema, ameiongelea hiyo barabara na Wanambeya wamekusikia, basi flow ya pesa iendelee kwenda pale ili mkandarasi asitoke kwenye site.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa fedha alizozitoa shilingi 27,000,000,000 za fidia kwa waliopisha ujenzi wa barabara ya mzunguko. Ninakumbuka Mheshimiwa Waziri alikuja Mbeya na yeye mwenyewe akasema nikirudi tu bajeti ya mwaka jana ile na akasema hizi fedha nitazitoa wakati huo Mheshimiwa Mbunge alikuwa ni dada yangu Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson na shilingi bilioni 27 zilishalipwa fidia kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hii ni dhamira njema ya Mheshimiwa Rais kwamba anataka kutukwamua Wanambeya kuepukana na foleni, lakini na ajali ambazo zinatokea mara kwa mara kutokana na jiografia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up atufahamishe Barabara ya njia ya nne hiyo ambayo inaanzia Igawa mpaka Tunduma ni lini itaanza kujengwa? Ili kukamilisha hicho kipande chote kiishe lakini na zile barabara zinazoilisha hiyo barabara ya njia ya nne ya Mbeya. Tunazo barabara ambazo zinazounganisha mikoa; iko Barabara ya kutokea Makongolosi kwenda Rungwa ambayo inaunganisha Mikoa mitatu Singida, Tabora na Mkoa wa Mbeya, lakini kwa bahati...

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Patrick kuna taarifa kutoka Mheshimiwa Kasaka.

TAARIFA

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kumpa taarifa mchangiaji pamoja na maneno mazuri anayoendelea kuyasema, lakini barabara hii aliyoitaja ya Makongolosi kwenda Mkiwa ni barabara ya kimkakati ambayo inaunganisha na kwenda kufungua fursa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na mikoa ya kati. Hivyo ni muda mwafaka sasa Serikali itoe fedha ili barabara hii iweze kwenda kutengenezwa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Patrick taarifa unaipokea?

MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipokea taarifa hiyo kwa sababu ninajua hawa ni wachimbaji wa madini na matajiri wengi wa Tanzania sasa hivi wanakimbilia kule Makongolosi na Chunya. Kwa hiyo, ni hii barabara ina umuhimu mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine tunayo barabara nyingine kwenye Mkoa wetu wa Mbeya na Mheshimiwa Waziri anaelewa kwa nini ninazitaja barabara zote za Mkoa wa Mbeya. Tunayo Barabara pia ya Mbeya Vijijini ya Mbarali - Shigamba na yenyewe imetajwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie hiyo barabara ianze kujengwa, kwa kuwa Mbeya Vijijini ndiyo wilaya pekee nchini inayolima zao la pareto na ni zao la kiuchumi kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo Barabara ya Kyela inayoanzia Ibanda – Kajunyumbele - Itungi Port. Ile barabara tayari ilishakuwa na mkandarasi ambaye mkataba wake ulivunjwa, kwa hiyo siyo barabara ambayo inaanza usanifu upya, lakini tunashangaa mpaka leo hii hakuna mkandarasi kule site na sijui itakuwaje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, watu wa Kyela wanamsikiliza kwa sababu ni wakulima wakubwa wa kokoa na Serikali inapata fedha nyingi za kigeni kupitia zao lile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wameongea hapa na malalamiko makubwa ni upatikanaji wa fedha. Hata hivyo, ninaweza kusema jambo moja, Sheria yetu ya Manunuzi ndiyo imekuwa ni kansa kubwa sana kwenye Wizara ya Ujenzi. La kwanza inashawishi mianya ya rushwa na ndiyo maana unakuta barabara nyingi zikijengwa ndani ya miaka miwili mitatu zinakufa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine linaongeza gharama kubwa sana ya ujenzi; nitoe mfano leo hii, ni mkandarasi nina tenda, ninatangaza kwenye NeST maana yake tunashirikisha dunia nzima, watu washiriki kwenye zile tenda, anashinda mtu kutoka nje ya nchi anakuja na begi lake anasaini mkataba. akishasaini sisi tunamtafutia advance payment na tunasema tuna shida ya fedha, wakati ilitakiwa wale watu waliotoka nje waje na mitaji yao ili wakandarasi wetu wa ndani tuwajengee uwezo ikiwezekana hao ndiyo wapewe advance payment. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini mtu umpe pesa? Kwa mfano miradi ipo mitano kila mkandarasi anataka shilingi 25,000,000,000, maana yake ni shilingi 100,000,000,000 inatumika kwa advance payment. Kwa nini Wizara isipeleke zile fedha kwenye benki zetu za ndani wale wakandarasi wakawa wanapewa mikopo kupitia benki zetu za ndani na mwisho wa siku Wizara inatoa guarantee tu pale kwenye mabenki kwamba huyu ni mkandarasi fulani, amejenga barabara imekaguliwa kilometa 10 apewe malipo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii unampa advance payment mkandarasi ya shilingi 25,000,000,000 yuko hapa ndani miaka zaidi ya mitano, ukimuuliza shilingi 25,000,000,000 umejenga wapi barabara anasema hii pesa ni mobilization, amejenga mabanda na kununua magari ya wafanyakazi halafu anajenga barabara kilometa 10 labda certificate ya shilingi 10,000,000,000 pesa inachukua mwaka mzima hajalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii tunafanya nini sisi, hii sheria ipo kwa ajili ya kum-favor nani? Ninaomba Mheshimiwa Ulega ninajua ni mtu makini na ana Mheshimiwa Naibu Waziri mzuri, ni injinia hebu aiangalie vizuri hii sheria inatu-favor sisi kama nchi au inawa-favor watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba uniongezee hata dakika mbili nimalize.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa malizia muda wako umekwisha.

MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mimi ni mtu wa mwisho, ninaomba dakika mbili tu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, bado bado kuna wachangaji wengine, malizia sekunde 30.

MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Jambo lingine tunao sisi wasomi wetu hapa ndani ambao ni wataalam, tuwajengee uwezo, wafungue makampuni wale vijana wetu ili wao ndiyo wawe wanajenga hizo barabara na tuwape hizo advance payment.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi imekuwa ni tabia kampuni za nje zinakuja kufungua kampuni hapa nchini zinajifanya ni local company ambayo tunaangalia local content kumbe ni kampuni za nje, wanapewa advance payment zinakwenda nje, ndiyo wanaamua shilingi ngapi zije kujenga barabara. Hatuwezi kufikia malengo na kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie sana. Ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)