Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lindi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MOHAMED M. UTALY: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika bajeti hii. Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kusimama leo kutoa mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati ambao tulikutwa na majanga ya El Nino katika nchi nzima kuna miradi 81 ya ujenzi wa madaraja ambayo yametekelezwa katika mikoa 22 na zimetumika pesa jumla ya shilingi bilioni 556.93 na miongoni mwa madaraja hayo ni pamoja na madaraja yaliyojengwa katika Barabara ya Kibiti - Lindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, niseme jambo moja tu kwamba madaraja haya ili tuweze kuyafikia ni lazima barabara iweze kujengwa. Hapa ninakusudia kuzungumzia Barabara ya Kibiti – Lindi - Mingoyo ndiyo barabara ambayo ninaizungumzia. Barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa mikoa minne na mikoa miwili iliyokuwa mwishoni ndiyo inanufaika zaidi. Barabara hii ilijengwa kwa kiwango cha lami kwa awamu kuanzia mwaka 1994 mpaka mwaka 2008, ambapo kipande cha mwisho cha Malendegu ndiyo kilikamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ni miaka 18 tangu barabara hii imejengwa. Nikichukua maelezo ya Mheshimiwa Profesa Mhongo maana yake barabara hii sasa hivi kipindi chake cha kuishi kimekwisha tangu zamani, kipindi cha kuishi kimezidi miaka minane.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii iliposanifiwa ilikuwa hakuna magari mazito yanayopita kwenye barabara hii ilikuwa ni barabara ambayo inapita mabasi tu na magari madogo madogo. Sasa hivi kuna mizigo mizito ambayo inapita, ni barabara hii tunayoitumia kusafirishia makaa ya mawe, ni barabara hii tunayoitumia kusafirishia mawe ya jasi ambayo yanaenda katika maeneo mbalimbali katika viwanda vya cement, ni barabara hii tunayoitumia kusafirishia bidhaa mbalimbali zinazotoka katika Bandari ya Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu ya mizigo mizito barabara hii imechakaa, imechakaa, imechakaa mno katika kiwango ambacho huwezi kuikarabati kwa sababu katika maeneo ambayo yanaharibika sana sasa hivi ni maeneo yale ambayo tunajaribu kuyakarabati.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mohammed kuna taarifa kutoka Mheshimiwa Katani Katani.
TAARIFA
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimetoka Mtwara leo usiku nikiwa ninapita kwenye barabara hii tairi zangu zote nne zimepasuka, gari imechakaa kabisa. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mohamed, taarifa hiyo unaipokea?
MHE. MOHAMED M. UTALY: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hiyo ninaipokea kwa mikono miwili. Sasa hivi ukitembea katika barabara ile huwezi kujua kiraka ni kipi barabara mpya ni ipi kwa sababu kiraka kinazidi barabara iliyokuwepo. Tunaiomba sana Serikali itusaidie watu wa Kusini hali yetu ni mbaya, hali ni mbaya sana. Mheshimiwa Mbunge yeyote akisimama hapa asipoitaja barabara ya Kusini haturudi, hili ndilo jambo ninataka nilizungumze wazi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba barabara hii ijengwe na barabara hii ina ahadi nyingi sana, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuja kwenye kampeni alisema barabara hii itajengwa kilometa 477 kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Uchaguzi wa safari hii tumeambiwa barabara hii itajengwa kilometa 166. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uchaguzi wa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Lindi, Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema mkeka utatandikwa kuanzia Dar es Salaam - Lindi - Mingoyo. Leo tunakuja kwenye bajeti hii hatuoni kiasi kilichotengwa kwa ajili ya Barabara, inatusikitisha, inatuhuzunisha, inatuumiza. Tunaomba, imefikia mahali sasa hivi wawekezaji hawawezi kuja Lindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa juzi tumezungumzia habari ya umeme ambayo ni nyenzo nzuri sana ya kuhakikisha wawekezaji wanakuja, jambo lingine ambalo ni tatizo kwetu ni barabara, barabara ni tatizo kubwa sana na sasa tunakwenda katika LNG.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana niliuliza siku ile hivi ni kweli tuna uhakika kwamba sisi tunakwenda ku-sign LNG au hatuna uhakika, kwa sababu kama tuna uhakika barabara hii ingewekwa kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba barabara hii ijengwe na suala langu la kuunga mkono hoja litakuja baada ya Mheshimiwa Waziri kusema kwamba barabara hii ameitengea kiasi chochote cha pesa.
NAIBU SPIKA: Ahsante sana.
MHE. MOHAMED M. UTALY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)