Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii nzuri sana ya mtani wangu Mheshimiwa Ulega. Jana kila akitaja alikuwa akitaja Wasukuma, akasema amepigiwa na mama Bogohe, akasema msukuma mmoja tena amelala kwenye barabara ya lami pale Busisi. Tunamshukuru, lakini tunamshukuru sana kwa kuendelea kutupangia fedha kwenye bajeti yake hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote tunayoyazungumza katika Bunge lako Tukufu, bila kuwa na pesa hakuna kitakachofanikiwa. Waziri atakuja na mbwembwe hapa, atasema kila aina ya maneno na Mheshimiwa Waziri hatukufundishwa hivyo kwenye Umoja wa Vijana. Lazima tufike sehemu tuwe wakweli, tusimamie Serikali, tuipe ushauri zitoke fedha tufanye kazi. Kama kuna tatizo lijulikane wananchi tuwaambie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho kingine ni kibaya kabisa, Viongozi wetu Wakuu wa Kitaifa wanapofanya ziara wanapotoa ahadi mbele ya wananchi, halafu baadaye utekelezaji unakuwa ni shida, tunaingia kwenye matatizo kama viongozi na tunaingia kwenye matatizo kama Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombeni sana Wizara ya Fedha itoe fedha ili kusudi watu wafanye kazi. Hakuna chombo ambacho kilikuwa kinasifika kama TANROADS na ni chombo ambacho, kwa ukweli usiopingika kilitufanya Chama Cha Mapinduzi tuwe na nguvu ya kusimama mahali popote na kusema utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Waziri; iko Barabara ya kutoka Mkoa wa Arusha – Karatu – Mbulu – Singida – Sibiti – Meatu – Lalago – Kolandoto mpaka Mwanza. Wamekaa Mheshimiwa Olelekaita amezungumza hapo kwamba, wananchi wamekusanyika na mahema yakawepo, wakatia sahihi kwamba, sasa mipango inaenda kufanyika, mpaka leo utekelezaji wako hujafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukirudi kule tunawaambia nini? Ifike mahali sisi kama viongozi, sisi kama Taifa, mambo ya msingi tuyape kipaumbele. Tunajua tuna mambo mengi ya kufanya yanahitaji fedha, lakini kupanga ni kuchagua kwamba, ni kitu gani kilichoko mbele yetu. Tukifanya hivyo, matarajio na kujenga nchi si kwa siku moja, kila Mbunge aliyeko humu anahitaji maendeleo, ni jambo ambalo ni la muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Waziri kuhusu Barabara yetu ya kutoka Bariadi - Kisesa, ambayo inakuja na kukutana na Sibiti, inakuja kukutana na Singida, ameitengea kwenye upembuzi sasa, kilometa 102. Ziko kilometa 20 pale Itilima, kwa mwaka ni mara nne wanapitisha sijui ule wembe, (wanasema kitaalam sijui kufanya nini) imechoka na magari yameongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwenye Mikoa hii ya Simiyu ni wakulima, kwa hiyo, mazao yetu yanayotoka kwenye Vijiji vya Laini, Migato, Chinamili kwenda kuuzwa kwenye NFRA, pale Ikindilo hayatafikika. Maana yake, tunarudi kwenye umachinga wa kawaida, watu watakwenda kununua mazao kwa bei ya chini, halafu tunarudi kuanza kulalamika huku hatujasimamia uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Wizara ya Fedha, hapa ni eneo moja tu, Wizara ya Fedha itoe pesa. Wataalam wa TANROADS wana uwezo mkubwa mno. Tuna engineers wazuri sana, wana uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyinyi ni mashahidi, pale Ubungo wame-design viongozi wa TANROADS, ukienda pale TAZARA, TANROADS imefanya hiyo kazi. Hatuna sababu ya kuwa na mashaka na chombo hiki. Yawezekana sasa Mawaziri, wanapoingia kwenye vikao hawasimami imara, wanakuwa na uswahili, uswahili, unaosababisha wataalam wetu wasifanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, jambo hili alifanyie kazi. Akumbuke alifanya ziara na Mheshimiwa Rais kwenye eneo letu. Mheshimiwa Rais alisema aweke mataa katika Wilaya ya Itilima, ili wale watu wasiwe wanapitapita usiku. Ninadhani alisimama na akasema, tayari atafanya hiyo kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru, amefanya hiyo kazi. Kilometa 118 ameziweka kwenye mpango wake za Barabara ya kutokea Luguru kwenda Madirana, kwenda Migato, kwenda Longalombogo, inakuja Ndolelezi, inakuja kuungana na Mheshimiwa Kadogosa na Mheshimiwa Kundo. Ni jambo la msingi sana, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri tusimamie fedha. Hata vyanzo hivi tunavyovizungumza kuviongeza kila kukicha, kama hatusimamii tulichokipitisha toka mwanzo, tutakuwa ni watu wa ajabu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili Bunge ni Bunge la Tatu. Wizara ya Ujenzi ilikuwa ikisimama ni makofi na kupongeza na kuondoka, lakini hii ni ishara Wizara hii na Mheshimiwa Waziri, watu tunampenda na Wabunge wanampenda. Wanataka sasa aende akatekeleze kazi kwa vitendo. Jambo hili ni la muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, ujenzi wa barabara zetu kwa sasa ninashindwa kuelewa. Sijui utaalam umepungua, au yawezekana magari yameongezeka zaidi kuliko zamani. Barabara inajengwa ndani ya miaka miwili, mitatu inakuwa inafanyiwa maintenance kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Barabara ya kutoka Shinyanga - Maswa - Lamadi, ni fedha nyingi sana zinazotumika. Pale tender inapotangazwa kwenye maeneo yale, kuna wakandarasi, kuna washauri, wanajengewa nyumba nzuri sana za kushauri kwamba, ni namna gani watakavyojenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi barabara Mheshimiwa Musukuma amezungumza tu kwamba, kuna mtu mmoja, Mheshimiwa Kiswaga tu huyu hapa tairi nne zilipasuka siku moja kwenye gari yake, zikapiga shimo kaa! Safari ikaishia hapo, hapo. Hata jana usiku kule Lamadi, jamaa mmoja akasema, hivi kuna Mbunge kwenye Mkoa huu wa Simiyu? Imepiga ikapasuka. Kwa hiyo jambo hili ni muhimu sana wataalam wabadilishe kusimamia mipango yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja, ili mtaalam aende akafanye kazi yake. Wabunge niwaombe tupitishie bajeti yake ili akafanye kazi zake, hizi hizi ndogo, zimsaidie. Huyu bwana ana maneno mengi sana na Wazaramo kazi kwao hawaiwezi, lakini sasa tunaamini ataiweza. Ahsante sana. (Makofi)