Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia niseme kidogo kwa mchangiaji wa mwisho dada yangu aliyemaliza kusema. Bunge hili ni chombo Tukufu sana na ni chombo ambacho tunategemea kukidhi matarajio ya Watanzania kwa kuisimamia Serikali. Tukifanya kama debate za shule za msingi, zile ambazo tulikuwa tunafanya wakati huo, si sawa. Mbunge unasimama kuanza kuchambua hotuba ya Mbunge mwenzako. Sidhani kama ni kazi ya Kibunge kuchambua, mpaka unajua alishiriki CC, unajua mkandarasi amelala guest, sasa sidhani kama hii ni kazi ya Kibunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilifikiri, chombo hiki kingetusaidia kushauri Serikali ili tutoke hapa tulipo. Baada ya kusema hayo, sasa nijikite kwenye hoja zinazohusu Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, Mheshimiwa Waziri ninamshukuru sana. Katika Jimbo letu la Hai umefanya kazi kubwa, amejenga culverts pale KIA akatuwekea na taa. Tunakushukuru sana na kwa kweli wananchi wa Hai wamenituma nimshukuru Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo tunasema tunashukuru au tunasifia tu, tunataja na vitu vilivyofanyika, imejengwa culvert na taa za barabarani zimefungwa. Hakuishia hapo, pale Bomang'ombe ameweka taa za kuongozea magari. Tangu tumepata uhuru, tangu dunia imeumbwa hazijawahi kuwepo, ndiyo zimekuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini, tusimsifie Mheshimiwa Rais? Ndiyo uungwana huo na niliwahi kusema humu jamani, wale Wakristo tulifundishwa kwamba, hata namna ya kusali, ombeni Baba yetu uliye Mbinguni, jina lako litukuzwe, utukufu wako, halafu baadaye ndiyo utupe leo riziki yetu. Kwa hiyo, ni formula tu ya kidunia na mtu akifanya jambo ashukuriwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hapa ninazungumza, Mheshimiwa Waziri amejenga Daraja la Makoa, japo halijakamilika, lakini tunamshukuru. Anajenga Daraja la Kitafu, kwenye bajeti hii nikisoma, ninaona miradi. Barabara ya Sadala kwenda Lemira kilometa 16, zimo humu. Daraja letu la kisasa la Kitafu limo humu. Sasa nimwombe Mheshimiwa, pamoja na mambo hayo mazuri ambayo ametuwekea huku, niweze kukushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, Mheshimiwa Waziri amalizane na mimi kuhusu viporo vilivyobaki. Kiporo cha kwanza ni pale Kwasadala. Wananchi wamekubali kuondoka, tunaomba, tunajua mchakato umeenda na kila wanapofanya kikao pale, bahati nzuri Naibu Waziri wake ni maarufu sana kule Hai, wanamjua. Wanasema yule baba mnene kila siku anakwambia tutalipwa, tutalipwa. Sasa ifike mahali, ile fidia iweze kulipwa na daraja lile lijengwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kiporo kingine kule Kitafu Juu, ambapo Kalali na Uswaa ilitakiwa iunganishwe. Juzi hapa Naibu Waziri ameniambia mkandarasi ameshalipwa. Tunamwomba nikitoka hapa akanikabidhi huyo mkandarasi, kwa sababu ameshachukua mzigo wa Mama Samia, nimfuatilie ili aweze kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwenye zile kalavati walizojenga, zinapeleka maji kwenye nyumba za watu kule KIA na Mheshimiwa Waziri alikuja pale aliona jambo hili. Nimwombe sana chonde, chonde, atusaidie namna ya kujenga mitaro ili maji yale yasifike kule. Bahati nzuri nilitembea na Meneja wa TANROADS, tukaenda kuona namna ambavyo wananchi wanapata tabu kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Waziri jambo lingine kubwa sana na kwa sababu ya AFCON inayokuja nchini kwetu; tuna Barabara ya Bomang'ombe - Chekimaji - TPC kwenda mpaka Tarakea. Barabara hii ni barabara muhimu sana na ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, lakini majuzi hapa Waziri Mkuu alikuja kuweka jiwe la msingi kilometa tatu, kuanzia Bomang'ombe kwenda kule Rundugai. Ninamwomba sana, Waziri Mkuu alisema washirikiane TANROADS na TARURA kujenga barabara hii. Ninamwomba washirikiane TANROADS ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana RAS wa Kilimanjaro ameandika barua kumkumbusha Mheshimiwa Waziri, kupitia Katibu wake Mkuu. Katibu Mkuu ninamwamini sana, mama mchapakazi yule. Niombe waifanyie kazi barua hiyo, ili barabara hii iweze kupitika. Hii ndiyo barabara ambayo ni diversion road.

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Arusha - Moshi imeshajaa, kipindi cha AFCON hapo tutashindwa, alisema Mheshimiwa Nassari hapo. Nimwombe pia, kiko kipande kidogo cha barabara kutoka kwa Mengi kwenda Kiaria. Hili Katibu Mkuu wa Wizara analifahamu vizuri, kupitia kwa Askofu Shoo pale. Ninaomba kipande hiki tumeshaahidiwa sasa asukume kiweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nishauri jambo moja hapa kabla sijagongewa kengele. Amezungumza Profesa Muhongo hapa, mambo mazuri kabisa, kwamba tuna mikataba ya madini iliyosainiwa kipindi cha Mheshimiwa Benjamin William Mkapa kwenye uongozi wake. Mikataba hii haijafanyiwa review, kama tukiweza wao wenyewe ingekuwa hii mikataba inawapa hasara, wangekuja Serikalini kuomba kufanyiwa review. Sasa sisi kwa kuwa wanapata faida na bei ya dhahabu imeongezeka, ifanyiwe review iwe ndiyo eneo ambalo tunaweza tukapata pesa ya kuongeza kwenye ujenzi wa barabara. Niombe sana hayo wayafanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, Tume yetu ya Mipango ifanye utafiti, aina ya barabara ambazo tunapaswa kujenga kwa mazingira yetu. Mheshimiwa Waziri ni mjanja, mtoto wa mjini. Ninasikitika sana kila akitembea barabara kuu hizi anakuta watu wana vitoroli na mchanga, wanafukia mashimo, kesho wanarudi pale pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini, tusijenge barabara ambazo ni za kiwango, tukijua tumejenga, tuondoke hapo. Kama kuna barabara kama alivyosema Mheshimiwa Kadogosa hapa, zimeshapitwa na wakati tuweke bajeti, kuliko hiki tunachoendelea. Ukisoma kitabu cha Waziri, utaona pesa za maintenance ni nyingi kuliko za kujenga barabara mpya. Kwa hiyo, Tume ya Mipango ikae chini, ije na draft ya kwamba, barabara zetu suluhu ni nini kuliko hivi tunavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe pia, kuna Barabara ya Machame kwenda Kiaria. Barabara hii kumekuwa na mgogoro, ninajua kuna kesi za Mahakama, lakini wananchi wanashindwa kujenga kwa sababu kuna wakati walipewa stop order ya kuendelea. Hebu wafike mwisho watuambie, wananchi waendeleze barabara zao? Serikali itoe tamko, kuliko sasa hivi watu hawajui wajenge au wasijenge.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na kumalizia kiporo kingine cha taa za barabarani, pale mjini ametuwekea taa vizuri kabisa. Ninajua na eneo la Kwasadala atatuletea, lakini yeye mwenyewe alivyokuja kwenye ziara yake alituahidi kutuwekea barabara hii na yeye anaijua ni ya kimkakati. Nimwombe kaka yangu amalize jambo hilo ili tuweze kufikia malengo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na ninaunga mkono bajeti hii kwa 100% na haya tuliyomshauri Waziri akayafanyie kazi. Mungu ambariki sana. (Makofi)