Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Sigrada Wilhem Mligo

Sex

Female

Party

CHAUMMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kidogo kwenye hii Wizara. Sisi Mkoa wa Njombe tuna barabara kubwa nne ambazo ni miaka 20 sasa zinaingizwa kwenye bajeti na zinawekwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa barabara ambayo imekuwa ndiyo changamoto kuliko barabara nyingine zote ni Barabara ya Ludewa – Njombe maarufu kama Itoni – Lusitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kuwapa picha ya hii barabara kwa sababu Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, kaka yangu Mheshimiwa Deodatus Mwanyika hataki mgogoro na Serikali, ndiyo maana hata alivyoizungumzia hakuweza kuingia kiundani zaidi. Mimi Sigrada Mligo sina cha kupoteza, ninataka niseme ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni mwaka wa tatu sasa, barabara imesimama. Mkataba unasema ilitakiwa barabara hiyo ikabidhiwe mwaka huu mwezi wa tano.

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutoa taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sigrada kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.

TAARIFA

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, haki lazima isemwe na isemwe wazi. Mheshimiwa Mwanyika, kwanza jana amechangia vizuri sana juu ya Barabara ya Itoni - Lusitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata juzi wakati tunaposhangilia Mei Mosi, Mheshimiwa Mwanyika akiwa na Mheshimiwa Villa na Mheshimiwa Kihenzile na wengine katika eneo hili la Iringa na Njombe, walinialika rasmi kabisa, akiwa na Mheshimiwa Sanga wa Makete. Walinialika rasmi nitembelee ikiwa ni pamoja na kuiona barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, kwa kuwa wananchi watakuwa wanafuatilia Bunge Tukufu, ninaomba nitoe taarifa ya kuwa Mheshimiwa Mwanyika, Mbunge wa Njombe ni kipaumbele chake namba moja, juu ya barabara hii na zingine nyingi katika Mkoa wa Njombe. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sigrada taarifa unaipokea?

MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipokea kwa sababu ameniunga mkono na anaungana na mimi kwamba Mheshimiwa Deo anaipambania hii barabara. Sasa kuna vitu ambavyo hawezi kuzungumza, nitazungumza mimi. Kwa hiyo, ninaipokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, iko hivi, kama nilivyosema, barabara hii ilitakiwa ikabidhiwe mwezi Mei mwaka huu. Mpaka ninavyozungumza hivi….

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sigrada kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Neema Mgaya, taarifa ya mwisho hiyo.

TAARIFA

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nilikuwa ninapenda kumpa taarifa, Mheshimiwa mzungumzaji kwamba, katika Wabunge ambao wamepambania barabara ile tangu mwanzo na ile barabara imeanza kujengwa kipindi ambacho Mheshimiwa Deo Mwanyika ameingia madarakani, ndiyo mwanzo wa kujengwa barabara ile na mpaka sasa hivi inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hakuna kitu chochote ambacho anaogopa kukiambia Serikali. Amezungumza mambo mengi na ndiyo maana barabara ile imeanza kujengwa ndani ya uongozi wake Mheshimiwa Deo Mwanyika. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Sigrada taarifa unaipokea?

MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo siipokei kwa sababu yeye ndiyo hana taarifa. Hatuna lami hata sekunde moja, hata nusu meta hakuna. Kwa hiyo na yeye hana taarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninataka kusema kitu kimoja, hii barabara ni mwaka wa nne sasa hatuna hata meta moja ya lami. Mkandarasi alipewa mradi, akafika site, akatifua ile barabara, halafu baada ya hapo akaondoka. Mpaka ninavyozungumza hivi, barabara ile imesimama, miaka minne sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tumerudi kwenye kampeni mwaka jana, mimi nilikuwa mgombea pia na Mheshimiwa mwenzangu Deo Mwanyika, tulikubaliana kwamba, Mungu akitujalia tukafika Bungeni, lazima tusimame wamoja. Msije mkafikiri mimi na Mheshimiwa Deo hatuzungumzi; poleni sana. Tusimame wamoja ila kila mtu aongee kwa mipaka yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza hivi, mhandisi mshauri ana miaka miwili analala guest. Kama mimi mwongo nishtakiwe. Ninavyozungumza hivi, mkandarasi aliondoka toka mwaka 2023 yuko Kigoma hajawahi rudi. Ninavyozungumza hivi, hii barabara ilivyoshindikana kupitika mwaka jana wakati wa kifuku, ikabidi Meneja wa TANROADS Mkoa wa Njombe atafute mkandarasi wa ziada ampeleke site. Ndipo mkaona kuna picha na waandishi wa habari wamesema Barabara ya Ludewa - Njombe mkandarasi yuko site.

Mheshimiwa Naibu Spika, yule siyo mkandarasi wa ile barabara, yule alichukuliwa kwa muda, kunusuru wakazi wa Njombe na Ludewa ambao kuna watu walijifungulia njiani. Ndiyo maana nikasema ninataka mpate picha pana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi nimehudhuria mkutano wa RCC ambao Mheshimiwa dada yangu Neema hajahudhuria. Nimesoma kabrasha la Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Njombe, anasema, mradi ule kwenye makabrasha yake ni wa shilingi 109,000,000,000. Mkandarasi alilipwa shilingi 21,000,000,000, anadai zaidi ya shilingi 70,000,000,000 na ndiyo maana mkandarasi yule, sasa hivi tunasingizia watu kwamba, mvua, mvua. Mvua Njombe ilishakwisha. Yule mkandarasi hawezi kurudi site, kwa sababu anachodai ni kikubwa kuliko kile ambacho tumemlipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kila atakayesimama anakwambia, tuliambiwa mvua. Kwani mwaka jana hatukuwa na mvua na kiangazi? Mwaka juzi hakukuwa na mvua na kiangazi? Mwaka 2022 hakukuwa na mvua na kiangazi? Kwa nini, tusiambizane ukweli?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mbunge mmoja alichangia hapa, sometime ni bora kuwaambia wananchi ukweli kwamba, hii barabara kwa sasa hatutajenga, kwa sababu hatuna bajeti na siyo kusingizia mvua na Mwenyezi Mungu anawaona. Wanasingizia mvua, wakati mwaka jana kulikuwa na kiangazi, mwaka juzi kulikuwa na kiangazi. Hivyo viangazi vya mwaka jana na mwaka juzi walijenga wapi? Ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea na hoja yangu nyingine. Hoja nyingine, kuna Mbunge mmoja hapa alitoa hoja ya msingi sana, ni namna gani tunaweza kwenda mbele. Akasema tunaweza kununua lami kwa bulk procurement. Hoja ya msingi sana. Sasa, kwa sababu sisi vitu kama hivyo hatutaki kusikia, niliona hakuna anayempigia makofi ila ukiongea mambo fulani ndiyo unapigiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ile laiti tungejua umuhimu wake sisi kama Wabunge na alitoa hesabu zake kwamba, tuna uwezo wa kununua lami na kujenga kilometa moja ya lami kwa shilingi 900,000,000 na akatoa namna gani tunaweza kujenga lami kwa shilingi 900,000,000. Mimi nilimpigia makofi, lakini mimi sitaki kupigiwa makofi kwa sababu, siku nitakayoanza kupigiwa makofi na CCM, ujue hali yangu ni mbaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia sitaki kupigiwa makofi kwa sababu mimi siyo hela. Anayependwa na kila mtu ni hela tu. Ahsante baba yangu. (Makofi/Kicheko)