Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FARAJI B. NANDALA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii ili nami niwe miongoni mwa wachangiaji wa hotuba hii ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia nichukue nafasi hii pia kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kuona kwamba barabara za Kitanzania zinapitika muda wote na zinakuwa rafiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tuliiona mapema tu tangu alivyoingia kuwa Rais Awamu ya Sita. Tumeona mchakamchaka mkubwa wa ujenzi wa barabara. Mimi ni Mbunge kutoka Mtwara kutoka Jimbo la Ndanda. Sisi kutoka Mtwara, tumeona maendeleo makubwa sana ya barabara. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitamshukuru yeye na Waziri mwenye dhamana hii ya ujenzi, kaka yangu Mheshimiwa Abdallah Ulega. Amefanya kazi kubwa sana Mtwara na Wanamtwara wanamkubali sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wanamtwara tumeshuhudia fedha nyingi zimemwagwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Tumeona fedha zaidi ya shilingi bilioni 268 kwenye ujenzi wa barabara kutoka Mtwara – Mnivata – Tandahimba – Newala kuja Masasi. Pia hawakutuacha hapo, wakatupatia fedha nyingine zaidi ya shilingi bilioni 400 kwenye ujenzi wa barabara kutoka Mtwara – Mingoyo – Ndanda kuja Masasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wananchi wa Mtwara tunakubali sana jitihada za Serikali na tunaona jitihada hizi ni za kuungwa mkono na za kupongezwa, kwa sababu asiyeshukuru kwa kidogo, hata ukimpa kwa kikubwa hawezi kushukuru kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mazuri hayo, bado kuna changamoto moja ambayo sisi wananchi wa Masasi, hasa Jimbo la Ndanda, tumekuwa tukilalamikia sana kuhusu barabara ya kutoka Masasi – Nachingwea – Liwale. Barabara hii imekuwa na changamoto nyingi, kwa sababu iliwekwa katika mpango wa bajeti ya EPC+F.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kufanya analysis ya barabara zote zile saba ambazo ziliwekwa katika mkataba huu, ufanisi wake umekuwa siyo mzuri. Sisi kule hii barabara moja ya kutoka Masasi – Nachingwea – Liwale imekuwa ikipigwa danadana sana, na kwa muda mrefu sana na kuwafanya wananchi kuwa na malalamiko.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii wananchi walifanyiwa uthamini na tathmini tangu mwaka 2013, Serikali iliwaahidi kuwalipa fidia. Cha kustahajabisha, hadi leo hii wananchi hawajalipwa fidia, lakini pia hata ujenzi wa ile barabara bado haujaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Ndanda, Masasi, Nachingwea na Liwale wameniagiza nije nimwulize Waziri na Serikali, ni lini hasa ujenzi wa barabara hii kutoka Masasi – Nachingwea – Liwale utaanza ujenzi wake? Pia wameniomba niiulize Serikali ni lini fidia itakwenda kulipwa kwa wananchi? Hawa wananchi watalipwa fidia kwa rate ipi? Kwa rate ya mwaka 2013 au kwa rate ya mwaka huu wa 2026. Kwa sababu gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Ardhi inasema, ukitoa ardhi ya mwananchi, lazima ulipe fidia na ulipe fidia kulingana na current price ya ile ardhi. Leo hii ni zaidi ya miaka 15, wananchi hawajalipwa fidia kwenye ile barabara na barabara haijaanza. Kwa hiyo, wameniagiza nije kuuliza, ni lini hasa hawa wananchi watalipwa fidia ili waweze kuendeleza yale maeneo?
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wale wamekaa zaidi ya miaka 15, na msingi mkubwa kwao ni ardhi. Leo hii wameshindwa kuendeleza ile ardhi kwa sababu Serikali imewazuia wasifanye chochote kwenye ile ardhi kwa kuwaahidi kwamba watawalipa fidia. Miaka mingi imepita, wazee wengine wanafariki, vitukuu pia vinakufa, lakini bado fidia kutoka kwa Serikali haijalipwa na hata barabara bado haijaanza kutengenezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe kaka yangu Mheshimiwa Abdallah Ulega atakapokuja kufanya hitimisho ya hotuba yake hii atuambie, ni lini wananchi wa Masasi, hasa kata ya Lukuledi watalipwa fidia zao na wananchi wote mpaka kuelekea Jimbo la Masasi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)