Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiwani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HIJA HASSAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, na ninaomba nichangie kwa ufupi sana kwenye hoja hii ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu. Kwanza ninaomba niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri, na niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu tumuunge mkono Mheshimiwa Waziri ili bajeti yake ipite ikafanye kazi ya kuwatetea wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamezungumza hapa, tutaendelea kulalamika na kumlaumu Mheshimiwa Waziri, lakini hoja ni kwamba Wizara hii ina tatizo la ukosefu wa fedha. Hoja ya pili, Wizara hii ina tatizo la kundi kubwa la madeni ya wakandarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niendelee kuiomba Serikali kwamba kama tunahitaji Wizara hii ifanye vizuri na Watanzania wapate barabara kama inavyohitajika, basi tulinde fedha za Mfuko wa Barabara kama ambavyo wenzangu wamezungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali ikubali sasa kubeba madeni yote ya wakandarasi chini ya Wizara hii. Laiti kama Serikali itabeba madeni yote, nina uhakika kwamba Wizara hii itafanya vizuri na malalamiko ya Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa Tanzania yataondoka kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, Serikali ikubali tu kubeba madeni ili kupunguza mzigo kwa Wizara hii ili Mheshimiwa Waziri na Wizara yetu ifanye kazi vizuri kwa ajili ya kuwatetea wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisikiliza malalamiko ya Waheshimiwa Wabunge wote, sisi ambao hatuna barabara; mimi ninaishi Zanzibar, lakini ninaiona hisia ya wenzangu wa Tanzania Bara. Ukweli ulivyo, siyo kwamba Waheshimiwa Wabunge wana nia mbaya, ni kwa sababu wanayabeba maono ya wananchi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, njia ya pekee ya kuwasaidia wananchi wa Tanzania ni kuongeza fedha kwenye Wizara hii na kulinda fedha za Mfuko wa Barabara ili Watanzania wapate barabara kama ambavyo Serikali na Mheshimiwa Rais amedhamiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili njia pekee ninaomba nikumbushe kwamba ni njia nne tu. Ya kwanza ni kulinda fedha ya Mfuko wa Barabara. Njia ya pili ni kubeba madeni ya Wizara ya Miundombinu ili Serikali ibebe madeni haya na fedha ya maendeleo ya Wizara hii, ibakie kwa ajili ya ujenzi wa barabara zetu. Njia ya tatu ni kutafuta vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitaangalia maslahi ya wananchi na havitaumiza wananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu wa mikoa yote, wa kanda zote tumsaidie Mheshimiwa Waziri, hii bajeti yake ipite. Mheshimiwa Waziri ni msikivu mbele ya Kamati, amekuwa akitusikiliza na Kamati yetu imebeba maoni ya Wabunge wote kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Tanzania. Kwa hiyo, ninaunga mkono hoja hii, ninaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuunge mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)