Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbagala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KAKULU B. KAKULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa nafasi hii. Nianze kwa kuipongeza Serikali kwa mageuzi makubwa ya miundombinu ya barabara hasa Barabara Kuu ya Kilwa katika Jimbo la Mbagara na kwa ukamilikaji na kuanza kwa shughuli za mwendokasi kuanzia mjini kwenda Rangi Tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi pia kwa Serikali yetu na kwa Rais wetu na wanaomsaidia katika upanuzi wa barabara ya kutokea Rangi Tatu kuelekea Kongowe na ujenzi wa daraja kubwa katika Mto Mzinga, ambao tunaamini utaenda kumaliza tatizo la mafuriko pale Mto Mzinga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo, nijielekeze kwenye jambo moja mahususi lililoko jimboni kwangu, ambalo ninafikiri pia linahusu Jimbo jirani la Kigamboni, kuhusu Barabara itokayo Kongowe kwenda Kivukoni kule Kigamboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi na upanuzi wa Barabara ya Kongowe kuja mpaka Rangi Tatu utakuwa na maana sana kama ile barabara inayotokea Kongowe kwenda Feri itafanyiwa upanuzi au kufanyiwa marekebisho makubwa. Ni muhimu tukubaliane, Mheshimiwa Waziri yuko hapa ni jirani yangu pale tunapakana mipaka Jimbo la Mkuranga na Jimbo la Mbagala. Barabara ya Kongowe kwenda Feri ni barabara ambayo imeharibika vibaya mno. Ninafikiri ujenzi wake sasa hivi ni kama miaka 40 tangu kujengwa. Imekuwa ikifanyiwa ukarabati kwa muda mrefu, lakini hali ni mbaya zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kiwango cha upanuzi wa viwanda na ujenzi wa viwanda unaotokea kwenye eneo la Kisarawe II kule Kigamboni na viwanda vinavyoendelea kuongezeka kule eneo la Mkuranga ambako ndiko Mheshimiwa Waziri anapotokea, barabara ile haiwezi kuhimili tena kiwango cha mizigo inayopita kwenye ile barabara. Kwa hiyo, imeharibika kiasi kwamba usumbufu kwa wananchi ni mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwenye hili la barabara ya Kongowe kwenda Feri, inabidi tuzungumze zaidi na Mheshimiwa Waziri, kwa sababu vinginevyo wakati wa kupitisha kifungu kwa kifungu tunaweza tukatofautiana, pamoja kwamba ni jirani yangu mwema.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba kusisitiza kwamba barabara hii ifanyiwe na kupewa kipaumbele mahususi kwa sababu ni barabara muhimu kiuchumi na kwa matumizi ya wananchi. Pia ni barabara ya mchepuko kwa wananchi wanaoenda kusini, wanaoenda Mikoa ya Mtwara na Lindi. Kwa hiyo, ni muhimu sana hili jambo nilisisitize mbele yako na Mheshimiwa Waziri ambaye ni jirani yangu ninafikiri ananisikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nitazungumza, ni la kisera kidogo, lakini pia ni jambo la miundombinu. Dar es Salaam kwa sasa hivi ilipofikia inaelekea ku-jam. Pamoja na upanuzi mkubwa wa barabara inayofanyika kwenye maeneo makubwa na mengi pale, lakini bado kuna tatizo kubwa sana la foleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kama tukitaka Bandari yetu ya Dar es Salaam ambayo tumeifanyia mageuzi makubwa sana; makadirio ya bandari yetu kati ya sasa na 2030 inatarajiwa kuwa ita-handle mizigo ya zaidi ya tani milioni 58. Katika hali ya kawaida kwa hali ya foleni iliyoko Dar es Salaam, bandari yetu tunaweza tusiifaidi kama hatutafanya upanuzi wa kutosha wa barabara. Hatutafaidi matunda yanayotokana na bandari.
Mheshimiwa Naibu Spika, upanuzi wa barabara inayotokea bandari kwenda Ubungo na kutoka nje ya Dar es Salaam unatarajiwa kuwa wa njia sita. Katikati mwendokasi, na njia nne, mbili upande mmoja na mbili upande mwingine; lakini ukiniuliza mimi nitakwambia Dar es Salaam ilipofikia hata upanuzi huo hautatutosheleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninafikiri mtazamo sasa ubadilike. Mheshimiwa Waziri ananisikiliza, kwamba zile barabara sasa hivi inabidi tufikirie kuzijenga kwa upana zaidi kuliko kubaki na njia nne zile ambazo bado haziwezi kutusaidia sana kuondoa msongamano pale bandarini na kwenye Mji wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya miundombinu ya Dar es Salaam kama tukiendelea kuitazama kama ilivyo bila kufikiria upanuzi mkubwa, bado tutaendelea kuwa na tatizo kubwa zaidi. Kwa mfano, upanuzi wa barabara inayotokea mjini kwenda mpaka Bunju wa njia sita. Njia mbili za kawaida na njia mbili za katikati za mwendokasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafikiri kwa sababu bado barabara ina nafasi ya kutosha tungeweza kupanua zaidi ya hapo ili barabara sasa tusiende kulazimika tena miaka mingine 10 kufanya mageuzi makubwa tena ya ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dar es Salaam, kwa uzoefu wangu, kwa mfano barabara ile ya Kilwa tuliipanua wakati wa Mheshimiwa Rais Kikwete kuwa njia nne. Imetutumia miaka 15 kwenda kurudi tena pale kuipanua tena kwa mara nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninafikiri mtatazamo uwe mkubwa zaidi, tupanue zile barabara ili bandari iweze kuwa na manufaa zaidi, kwa sababu vinginevyo kama hali ndiyo ile hatutaondoa tatizo. Kwa mfano leo tunapozungumza eneo la Jimbo la Mbagara foleni imekuwa mbaya zaidi kuliko ilipokuwa kabla. Kwa nini? Kwa sababu ongezeko la ICDs na ongezeko la shughuli za bandari zimefanya ile barabara sasa hivi inapata usumbufu mkubwa sana. Kwa hiyo, unakuta malori yame-pack kandokando ya barabara, hali ya usumbufu ni kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi lori lilianguka pale Mto Kizinga kabla ya kufika Mbagala, magari yamesimama pale na wananchi wametembea kwa mguu kwa zaidi ya masaa sita. Kwa hiyo, huu ni msisitizo. Mheshimiwa Waziri yuko hapa, kwamba tukubaliane kwamba kuna haja ya kufanya mageuzi makubwa katika ukubwa wa barabara zinazotoka Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia jambo moja la mwisho kuhusu fidia za wananchi wangu pale Mbagala. Zaidi ya wananchi 536, wanadai zaidi ya shilingi bilioni 21. Walibomolewa nyumba tangu mwaka 2002 hadi leo wanadai, na hatujapata majibu ya kuridhisha kutoka kwa Serikali kuhusu ni lini wananchi hawa watafidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili ninaomba tupate majibu ya kuridhisha ili tuweze kumuunga mkono Mheshimiwa Waziri. Nitaunga mkono hoja hii kama nitapata majibu ya kuridhisha kuhusu hizo hoja nilizozitoa hasa kuhusu barabara ya Kongowe – Feri na fidia kwa wananchi wetu wa Mbagala.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)