Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Christina Solomon Mndeme

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuboresha miundombinu nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za miundombinu ni nyingi na mahitaji ni mengi, lakini Mheshimiwa Rais wetu anafanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa barabara, madaraja, makalvati, mifereji na kila kitu kinakuwa sawa kulingana na uwezo. Tunampongeza sana Rais wetu. Tanzania ya leo siyo Tanzania ya jana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi kubwa kwa Mheshimiwa Waziri Ulega pamoja na timu yake yote. Ninampongeza sana kwa kazi kubwa anayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais wetu kipenzi na chaguo la Watanzania. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru sana Serikali yetu pendwa kwa kutuboreshea miundombinu Mkoa wa Tabora, kwani Tabora ya leo siyo Tabora ya jana. Sasa Tabora inafikika kwa urahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miaka mingi Mkoa wa Tabora ulikuwa haujaunganishwa na barabara za lami, ilikuwa ni vigumu kuufikia mkoa wetu, lakini sasa hivi kwa siku moja unaweza ukafika ndani ya Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Tabora haukuwa na hata taa za barabarani. Sasa hivi taa za barabarani tunazo. Tabora tulikuwa tuna matatizo sana ya barabara ambazo zilikuwa hazipitiki kwa mwaka. Sasa hivi kiwango kimeongezeka. Zipo ambazo tumeongezewa, zinapitika kwa mwaka mzima. Tumeongezewa madaraja, tumeongezewa makalvati, tumeongezewa mtandao wa barabara ya lami ndani ya Mkoa wetu wa Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, palipo na mafanikio hapakosi changamoto. Ninaomba kuishauri Serikali kufanya mambo yafuatayo. Pale ambapo hali itaruhusu ili kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara ndani ya Mkoa wa Tabora na kurahisisha usafiri na usafirishaji, nami kwa namna ya pekee ninawashawishi Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuipitishe bajeti hii ili yale ambayo tunayaomba yakatekelezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba tuweze kujengewa barabara ya lami ya mchepuo (bypass) kutoka Kigwa – Ibili ambayo ni Wilaya ya Uyui, ili kupunguza msongamano wa malori na magari mengine yanayokwenda mikoa mingine na nchi jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, tunaomba kuzibiwa mashimo yaliyochimbika katikati ya barabara yaliyosababishwa aidha na mvua na changamoto nyingine ili kupunguza ajali na kuharibika kwa vyombo vya moto. Vilevile, tunaomba kurudishiwa taa za barabarani na alama za barabarani maeneo ambayo zimetoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tunaomba ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Ipole mpaka Lungwa kupitia Kata ya Ngoywa – Kitunda – Kiloli - Kilumbi na Kipili. Pia ni barabara muhimu sana kwa utalii wa Mbuga ya Mpemba Mpazi, ipo wilaya ya Sikonge na pia inaunganisha Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Mbeya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kujengewa barabara kwa kiwango cha lami ili kuunganisha Mkoa wa Tabora na Singida kutoka Tura - Maguliati na Iyumbu. Tunaomba kujengewa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Tabora – Mambali kupita Bukumbi – Shitage - Ushetu na Kahama. Hii itasaidia kuunganisha Mikoa ya Kagera – Shinyanga - Tabora, Katavi na Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kujengewa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Nzega – Itobo – Igusule – Gongwa, Mkoa wa Shinyanga. Tunaomba barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kahama – Ushetu – Ulyankulu – Kaliua na Ugala, Mkoa wa Katavi. Tunaomba kujengewa barabara kutoka Tabora – Ibili – Ulyankulu ambapo upembuzi yakinifu umekamilika; tunaomba ujenzi uanze.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba barabara kwa kiwango cha lami kutoka Puge – Ziba – Choma kwa kiwango cha lami ambapo kuna Hospitali ya Rufaa ya Nkinga. Hii ni hospitali ambayo barabara inapokuwa imeharibika wanaopata changamoto kubwa ni akina mama na watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba maombi haya yote. Ujenzi huu wa barabara uwe wa ubora wa hali ya juu ili ziweze kudumu kwa muda mrefu. Ninapomalizia maombi haya, niwashawishi wenzangu tuiunge mkono hotuba hii, ili maombi haya sasa yaweze kufanyiwa kazi kwa kuwa changamoto ni nyingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)