Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara yetu hii ya ujenzi. Awali ya yote nianze kumshukuru Mungu kwa kutupa uhai sisi sote humu ili basi tuweze kutimiza hili jukumu ambalo tumepewa na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee sana nimpongeze na nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo ameendelea kusimama na kutuongoza Tanzania na hata hizi barabara ambazo tunaziongelea leo zimeendelea kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote humu ndani wamezungumzia barabara; na kilio cha Watanzania walio wengi ni barabara. Siyo TANROADS na siyo TARURA, kote huko ni barabara zimetenganishwa tu, lakini ukiangalia Tanzania kilio kikubwa ni barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatambua kwamba mkate wa Taifa ni mdogo na kwa sababu mkate ule tunagawana kidogo kidogo, wakati mwingine hautoshi. Hautoshi kufikia malengo yale ambayo kila mbunge aliyeko humu ndani angetamani kwenye Jimbo lake kiweze kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane sana na Kamati na niipongeze Kamati kwa kazi kubwa ambayo imeifanya. Hamna muujiza utakaotendeka kutengeneza barabara zote zile kama hatuna fedha. Hatuwezi tukapiga magoti tukaomba kesho yake barabara zikawa zimetengenezwa; tutatengeneza barabara hizi iwapo tu tutakuwa na fedha za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa nini ninaungana na Kamati? Kamati ushauri mmojawapo ilioutoa ni kufikiria na kugundua vyanzo ambavyo vitaongeza mapato ili barabara zetu ziweze kutengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Sisi ni Watanzania, lakini pia ni Wabunge. Tukubaliane kwamba, ni lazima tutafute vyanzo, na vyanzo hivyo wakati mwingine vitaumiza, wakati mwingine vitaongeza gharama, lakini tutaangalia kipaumbele tunataka nini? Tunayo bandari, tunakusanya fedha huko kwenye bandari, tunazo sehemu nyingi ambazo tunaweza tuka-adjust kidogo tu, changamoto zikipatikana, lakini tuta-solve tatizo. Hatuna mtu wa kutusaidia, ni sisi Watanzania tunatakiwa tujisaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kupata vyanzo vya mapato na kuongeza, hizo fedha tukizipata na kwa sababu ni kwa ajili ya barabara, tuweze kuzilinda ili ziweze kwenda kufanya kazi iliyokusudiwa. Kama tutakusanya na tukalinda zikafanya kazi iliyokusudiwa, kiukweli tutapiga hatua kiasi; tunaweza tusimalize leo, lakini kesho na keshokutwa tukamaliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, tunashauri na Kamati nayo imeshauri kwamba tuwe na uwezekano, miradi ambayo imeshaanza tusikusanye mingi. Tunakusanya halafu mwisho wa siku hatuna bajeti. Tutengeneze ile ambayo imeshaanza, tutengeneze ile ambayo tulishasaini mikataba, ili basi ikamilike hata kitu kionekane, kuliko kuwa tunafanya vipande tunaachia njiani, vipande tunaachia njiani, matokeo yake kila sehemu ni kelele na hakuna kilichofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nchi nyingine kuna barabara zipo za kulipia. Hii PPP ambayo tunasema tuiitekeleze kwa vitendo, ili mwisho wa siku tusiwe tunasema tu. Tukija hapa tunasema, lakini hakuna mradi ambao tunaufanya wa hizi PPP. Tutafute watu wenye fedha ambao wanaweza kushirikiana na Serikali. Sehemu zile ambazo kunaweza kufanyika kibiashara hizi barabara tujenge kwa PPP ili mwisho wa siku, tuweze kuipunguzia mzigo Serikali na tuweze kupata barabara nyingi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali watakapokuwa wanakuja kuhitimisha, watupe commitment ya kutafuta vyanzo ambavyo aidha vinaumiza kidogo au haviumizi ambavyo vitaongeza mapato twende tukatengeneze barabara. Vilevile Mheshimiwa Waziri atupe commitment ya kulinda hizi fedha ambazo zinakusanywa kwa ajili ya Mfuko wa Barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kidogo kuhusu Geita. Nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa daraja kubwa ambalo alilikamilisha la Kigongo – Busisi, angalau sasa hivi una uhakika wa kutopanga foleni sana unapokwenda Mwanza, lakini sisi Geita hatujawahi kuunganishwa na Mkoa wa Shinyanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo barabara ambayo toka mimi nakua, tumekuwa tukiambiwa inatengenezwa kwa kiwango cha lami, lakini mpaka sasa hivi tunavyozungumza haijatengenezwa. Tarehe 1/10/2025 ulisainiwa mkataba wa kuitengeneza ile barabara. Ukiangalia kutoka Kahama mpaka Kakola, mwekezaji ametengeneza, lakini kutoka Kakola mpaka Geita hiyo barabara haijatengenezwa. Mkataba umesainiwa, fedha za kumlipa mkandarasi advance imekosekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba commitment ya Serikali, hizi fedha ni lini zitaenda kulipwa ili ile barabara kiukweli itengenezwe ili na watu wa Geita waweze kunufaika na hizi barabara zinazounganisha Mkoa na Mkoa.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mwambura muda umeisha.
MHE. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana, kwa kunipa nafasi, ninaunga mkono hoja na ninaomba commitment ya Serikali kwenye hayo ambayo nimeyaongea.