Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Jonas William Mbunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika bajeti hii ya ujenzi. Awali ya yote, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na afya njema, na leo nimepata nafasi ya kuchangia bajeti hii ya ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana mtani wangu, Mheshimiwa Ulega kwa hotuba nzuri ambayo ameiandaa pamoja na wasaidizi wake na ina mambo mengi, lakini changamoto ninayoiona kubwa ni namna gani anawezeshwa ili kuhakikisha kwamba anaitekeleza hiyo bajeti yake? Kwa hiyo, niwaombe Wabunge wenzangu tushirikiane tuiagize Serikali itoe fedha ziende katika Wizara ya Ujenzi ili Mheshimiwa Ulega aweze kutekeleza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu kuna barabara ya kutoka Mbinga - Myangayanga – Litembo. Barabara hiyo ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Barabara hiyo ni barabara muhimu sana kwa sababu wakulima wa maeneo ya Litembo na maeneo mengine wanalima kahawa na hiyo barabara ni kama barabara inayosaidia sana kuhakikisha kwamba mazao haya yanafika katika eneo la Mji wa Mbinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri katika mikakati yake na mipango yake yote kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa na itakuwa imekidhi na kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kuna barabara ya kutoka Mbinga - Pachani – Longa kilometa 10. Kipande hicho kinaleta changamoto kwa sababu ukitoka Longa kwenda Rundumato, barabara hiyo imejengwa kwa kiwango cha lami, lakini kutoka Pachani mpaka Longa barabara hiyo ni ya vumbi na inasumbua sana wakati wa kipindi cha mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi wa Mbinga wamenituma nimwombe Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba barabara ile inajengwa ili wananchi wale waweze kupata neema na matunda ya uhuru wa nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2025 nilipata bahati nikawekewa baadhi ya taa za barabarani pale Mbinga Mjini. Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri katika mikakati yake ahakikishe kwamba Mji wa Mbinga unaendelea kumeremeta kwa kuwekewa taa za barabarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ni muhimu sana kwa Wananchi wa Mkoa wa Ruvuma ni Barabara ya kutoka Songea - Njombe hadi Makambako. Barabara hiyo ilijengwa mwaka 1984 na kampuni ya Balfour Beatty na ina umri wa miaka zaidi ya 30 inaelekea 40, lakini barabara hiyo inatumika kwa ajili ya kusafirisha makaa ya mawe, mazao mbalimbali ya kahawa na mahindi, na sasa hivi imeharibika na inaleta ajali nyingi sana katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Ulega katika mikakati ambayo imewekwa, tunajua kuna mpango wa kuanza kujenga kilometa 100, lakini mpaka sasa hivi, kazi hiyo haijaanza. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali, kuweka msisitizo kwa kuhakikisha kwamba barabara hiyo inaanza kujengwa ili wananchi wa Mkoa wa Ruvuma waweze kuitumia kwa kusafirisha makaa ya mawe, kusafirisha kahawa, mahindi na mazao mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ambayo ipo kwenye Wizara hii ya ujenzi ni Taasisi yetu ya TEMESA huwa inashindwa kulipa wazabuni. Kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, pamoja na mikakati yote aliyonayo, ahakikishe kwamba wazabuni wanalipwa ili waendelee kutuhudumia na kutoa huduma nyingi katika maeneo yetu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja. (Makofi)