Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kuwashawishi wenzangu kwamba tumpitishie Mheshimiwa Waziri Ulega bajeti hii kwa sababu kwanza amekuwa ni Waziri wa kwanza ambaye anajituma, anakwenda Wilaya kwa Wilaya, Jimbo kwa Jimbo na anapambana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tunatakiwa tujue kwamba haya mambo ameyarithi tu, ameyakuta na kikubwa ni kwamba hapewi fedha za kutosha. Kwa hiyo, niseme tu viboko wamekutandika sana Mheshimiwa Ulega na wewe ukiingia kwenye vikao, basi nenda ukawe mkali. Wamekuchapa sana, wamekutandika sana, lakini hata tukikutundika, haina maana. Maana yake ni kwamba tusipokupitishia, na hizi ndogo au chache zilizopo, basi kazi zisifanyike.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niende moja kwa moja kwa kusema, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge wangu wa Musoma Mjini Mheshimiwa Muhongo, ameiongelea sana jamani barabara yake ya Musoma - Makojo - Busekera, hadi imefika hatua yaani sasa, ninaona kama anaona huzuni hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama Mbunge wake, na mwananchi wake wa Musoma, ninaomba sana Serikali iiangalie hii barabara kwa jicho la huruma. Kati ya barabara zote nchi nzima, Mheshimiwa Rais alizosema kwamba ziunganishwe Wilaya kwa Wilaya, imebakia Wilaya ya Musoma Vijijini na Wilaya ya Musoma Mjini peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ndiyo ambao hazijaunganishwa barabara na barabara, pamoja na kuwa Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri sana na baadhi ya maeneo mkoani kwetu Mara kwa kweli, amefanya mambo mazuri sana tunampongeza na barabara zipo baadhi ya maeneo, lakini kwa eneo hili la Musoma Vijijini basi tuonewe huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hizi kilometa 92 jamani kilometa tano tu! Ni kweli kwamba wengine wanapata mpaka barabara za vichochoro, wanapata barabara za kuunganisha mpaka barabara hizi zinazotoka Benki ya Dunia. Jamani, sisi hii barabara moja tu basi angalau tujaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Rais huko aliko, aniangalie mtoto wake, binti yake Bungeni pekee, mtoto wa Chifu Hangaya, barabara inayokwenda nyumbani kwetu Musoma Vijijini Majita, Mheshimiwa Rais, ninaomba angalia mama, kwenye mfuko tu wa ziada, basi angalau na mimi binti yako niwe ninaenda kwetu ninajitapa au ninatamba kwamba mtoto wa Rais nimekuja Musoma Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hili daraja la Nyasahungu na daraja la Suguti. Juzi Mkuu wetu wa Mkoa imebidi ashuke atembee kwa miguu, bahati nzuri Mheshimiwa Mtambi, Mkuu wetu wa Mkoa ni Mwanajeshi, yuko vizuri, ikabidi apite pale. Hili daraja limeleta maafa mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwomba sana Waziri, rafiki yangu Mheshimiwa Ulega, ndugu yangu, yeye ni mchapakazi, basi angalie. Ninaamini kabisa bajeti siyo msahafu, inaweza ikarekebishwa na baadhi ya maeneo, wakatuongezea fedha basi na sisi tukajengewa hata madaraja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Waziri Ulega anakumbuka juzi juzi amekuja Tarime, katika msafara wake kuna gari yake ilipata pancha katika barabara zetu, angalia hii barabara ya Tarime - Mugumu. Hii barabara kwetu sisi ni barabara ya kiuchumi, pia inaleta watalii, inapitisha watalii, lakini ni barabara mbovu. Hii ndiyo barabara ambayo hata Mheshimiwa Musukuma juzi alitucheka. Imagine, mpaka Wabunge wenzetu wanatucheka jamani Mkoa wa Mara! Kwani sisi tuna matatizo gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika kwetu ndiyo ametoka Mwasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa kweli najisikia uchungu, nataka hata kulia. Roho inaniuma sana kuona kwamba sisi tulimtoa Mwasisi wa Taifa hili, lakini pia bado miundombinu kwetu inakuwa ni migumu. Jamani, Mkoa wetu wa Mara ndiyo ungekuwa kivutio, Mkoa wetu wa Mara ndiyo ungekuwa wanasema kwamba jamani, tunataka kwenda kuangalia Mkoa wa Mwasisi wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Wizara zituangalie, tunaomba na sisi pia tuangaliwe ndugu zetu, basi na sisi angalau tuonekane tumetoka Mkoa wa Mara. Tunajitahidi sana kama mnavyotuona angalau kupambana kuogaoga hivi, lakini kwetu kule tunaoga vumbi. Barabara bado ni vumbi jamani. Sisi tutajitapia nini tuliotoka kwa Mwasisi wa Taifa hili? Kwa hiyo, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri Ulega nenda kaangalie na Wizara yako basi mrekebishe hizi barabara angalau zipitike.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Wabunge wenzetu wanatucheka, tunajisikia vibaya. Juzi ilibidi twende tukajifungie pamoja Wabunge wa Mkoa wa Mara tulie, kwa sababu haya mambo kwa kweli tulikuwa tunaongea kwa uchungu sana. Kwa hiyo, niwaombe sana ndugu zangu mtusaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kuna hospitali yetu ya Kwangwa, ile ni hospitali ya rufaa. Hospitali ambayo Mama yetu Samia Suluhu Hassan katenga fedha nyingi sana, lakini ndiyo hospitali ambayo haipitiki. Ukienda pale hospitalini, juzi mwenezi CCM wa Taifa Ndugu Kihongosi alikuwa na ziara, akiwa na ziara hata hajafika mwisho, gari ya mwisho ikapata pancha katika gari zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba Mheshimiwa Waziri aangalie jinsi ya kurekebisha mambo haya kwa sababu bajeti siyo msahafu, inaweza ikarekebishwa na sisi Mkoa wa Mara tunatamani kujulikana kwamba Mwasisi wa Taifa hili ametoka Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)