Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu na afya njema, mpaka leo nasimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia hotuba hii ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, kama ambavyo wengi wetu wametangulia, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika Taifa hili na kutuongoza kwa umaridadi mkubwa sana. Pia, ninachukua fursa hii kumpongeza kwa dhati kabisa kaka yangu, Mheshimiwa Ulega, Waziri wa Ujenzi, kwa hotuba yake nzuri iliyosheheni mambo mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pekee nimefurahishwa sana na Hotuba ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi mimi pamoja na wananchi wangu wa Wilaya ya Mkalama, Jimbo la Iramba Mashariki, baada ya kuona barabara yetu kilometa 89 kutoka Iguguno kupitia Nduguti na kuendelea imetajwa kwenye bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara yetu ile ndiyo moyo wa wananchi wa Mkalama. Barabara ile ndiyo uti wa mgongo wa wananchi wa Mkalama. Nimefurahi sana kuona imetajwa, na ninasema tu, hivi karibuni nimepata ujumbe kutoka kwa Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Singida, ambaye ni mchapakazi kweli kweli. Amenijulisha kwamba, siku chache zijazo anakwenda kutangaza upya tenda za kilometa 10 ambazo zinakwenda kuvuruga kwa mkeka mweusi centre ya Nduguti, Wilaya ya Mkalama. Naishukuru sana Serikali, naishukuru sana Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu ni moja tu. Tunaomba jambo hili, mchakato huu, uwe kwa haraka, usisuesue kwa sababu, tunahitaji sana barabara hizi. Sina wasiwasi kabisa na Mheshimiwa Waziri; sina wasiwasi na watendaji wake wote akiwepo Mkurugenzi wa TANROADS Tanzania; ninaamini kabisa mambo haya yatakwenda kufanyika, ujenzi huu utakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutumia fursa hii kuipongeza sana Kamati ya Miundombinu. Hotuba hii ni nzuri na imetupa mwanga sisi Wabunge kuweza kuishauri Serikali ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja ya Kamati inayotaka mfuko. Inapendekeza fedha za mfuko wa barabara zielekezwe kwenye matumizi yaliyokusudiwa kwenye barabara, yaani tusiwe na reallocation.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiruhusu reallocation kwenye fedha hizi, hiyo asilimia tano ni wazi kabisa TANROADS itakufa na haitaweza kujisimamia. Ni muhimu sasa Serikali ikaona umuhimu wa kuifanya TANROADS kuwa na full financial autonomy, ikawa na mamlaka kamili ya kifedha, ili kuweza kuiwezesha kutekeleza shughuli zake za ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili sisi hatutakuwa wa kwanza. Nimetazama nchi mbalimbali, ziko nyingi, lakini kwa sababu ya muda, nitataja nchi mbili. Mfano, South Africa wana shirika lao linaitwa SANRAL, yaani South African National Roads Agency Limited. Shirika hili lina full authority, lina uhuru kamili wa kifedha. Shirika hili linakusanya ushuru na kupokea fungu la matengenezo bila kupitia urasimu wa hazina yake. Hii ndiyo imesababisha barabara nyingi za South Africa zinakuwa na ubora zaidi Afrika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi hatutakuwa wa kwanza, kuna nchi ya New Zealand, hii inaitwa 'The Gold Standard'. Wao wanatumia mfumo unaitwa NLTF, yaani National Land Transport Fund. Sheria yao waliyoitunga inakataza kabisa Wizara ya Fedha, pamoja na Hazina kuingilia kwa vyovyote vile makusanyo yanayogusa fedha za barabara. Wanakusanya kwenye kodi ya mafuta na wanapeleka moja kwa moja kwenye mfuko wao, hawataki kabisa mfuko ule uguswe. Kwa nini sisi tusifanye hivyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, nimeangalia ripoti, inaonesha Tanzania imewahi kuwa kwenye rekodi kubwa miaka 20 iliyopita kwa kupeleka makusanyo ya bajeti kwa kiwango kile kile kilichokusanywa kikapelekwa kwenye Mfuko wa Barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma ripoti ya Road Fund Board Secretariat ya Mwaka 2005 na ninayo. Ripoti hii ilikuwa ina lengo la kuonesha mwenendo wa kibajeti wa kifedha toka mwaka 1997 mpaka 2004. Ripoti inaonesha kwa miaka mitatu ya fedha, mfululizo, kuanzia mwaka 2001/2022 bajeti, mwaka 2022/2003, 2003/2004 Wizara ilipeleka kiasi chote, 100% ya kiasi kilichokuwa kinatengwa kwa ajili ya barabara. Sasa ni kwa nini sasa hivi tunashindwa kufanya hivyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi zinakusanywa...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, muda umeisha, malizia.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja, lakini ninaiomba Serikali, fedha zote za Mfuko wa Barabara zipelekwe kwenye vipaumbele, zisipelekwe kwenye vipaumbele vingine. (Makofi)