Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Mgore Miraji Kigera

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MGORE M. KIGERA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Ninapenda dakika chache hizi, kwanza nitoe pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya kuhakikisha miundombinu ya barabara inaendelea kuimarika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana tumesikia hapa kilometa 1,495 zimeweza kujengwa kwa kipindi cha Awamu ya Sita, na hapa bado ana miaka mingine minne mbele. Ninaona Mheshimiwa Rais anakwenda kuvunja rekodi katika ujenzi wa barabara za lami nchini Tanzania. Tumesaini juzi mkataba wa kujenga barabara ya njia sita kutoka Dodoma kwenda mpaka Chamwino. Hiyo ni kazi nzuri inayofanywa na MheshimIwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninawapongeza Wizara ya Ujenzi, chini ya Waziri wetu Mheshimiwa Ulega, pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Kasekenya, Katibu Mkuu na Naibu wake na watendaji wote wa TANROADS Tanzania nzima wakiongozwa na Mtendaji Mkuu, kaka yangu Besta.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamesimama hapa wakiongea kuhusu barabara. Ni kweli kitovu cha uchumi wa nchi yetu ya Tanzania ni barabara. Wakulima wanatumia barabara ambazo ni gravel na tunazo barabara za lami, hata hivyo barabara zote, ili ziweze kuendelea kuimarika, tunahitaji tupate fedha. Huyu Mheshimiwa Ulega huyu, watashika shilingi, watamkata masikio, lakini bila fedha kwenda Wizara ya Ujenzi, hakuna kitakachoweza kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mwaka 2025/2026 shilingi bilioni 945 zilitakiwa zitoke kwenye Mfuko wa Barabara, zimetoka shilingi bilioni 418, sawa na 44% tu, 56% fedha hazijaenda. Utekelezaji wa miundombinu utafanyikaje? Siyo ujenzi wa barabara mpya, wala siyo kufanya maintenance ya barabara zetu; ni kweli barabara ni mbovu sana, tunahitaji fedha. Ninaomba Serikali ipeleke fedha Wizara ya Ujenzi, fedha zinavyokusanywa ziende zilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wamekuja na mpango wa kusema kwamba, inatakiwa asilimia tano iende kwenye maeneo mengine. Mimi sijawahi kuona mtu anaenda kuomba jamvi msibani; yaani wewe una msiba, mtu anakuja kukuomba jamvi! Wizara ya Ujenzi hapa inapumulia mashine, tena itolewe asilimia tano iende maeneo mengine. Sidhani kama hii ni sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itafute maeneo mengine ya kutoa fund iende kusaidia maendeleo mengine na fedha za Mfuko wa Barabara ziachwe kama zilivyo, ili ziendelee kutengeneza barabara zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ametoka kuongea hapa Mheshimiwa Musukuma, ni kweli, kutoka Dodoma mpaka ufike Jimboni kwangu Musoma, kama haujapasua tairi mbili, una Mungu ndani yako. Ni kwa sababu, Wizara ya Ujenzi haina fedha, wanashindwa kufanya chochote. Ninaomba Serikali ipeleke fedha Wizara ya Ujenzi, na hili ninalisisitiza, tunaomba fedha ziende Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niongee kuhusiana na madeni ya wakandarasi. Katika watu wenye matatizo dunia hii, hasa nchini Tanzania, ni wakandarasi tena wa ndani. Wakandarasi wa ndani wanadai fedha nyingi sana, na yote inatokana na fedha kutokwenda kwa wakati, ndiyo maana wakandarasi wanakuwa wanadai.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisikia depression, wakandarasi; pressure, wakandarasi; sukari, wakandarasi; vifo, wakandarasi; watu kuuziwa mali zao, wakandarasi; kwa sababu, wanafanya kazi hawalipwi. Ninaomba Serikali ije na mpango mzuri wa kuona ni wapi itaenda kupata fedha, na Serikali yetu inaaminika, hata kama ni kwa kukopa waweze kuwalipa wakandarasi madeni yao yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ujenzi inashindwa ku-perform kwa sababu, fedha inaingia for instance shilingi trilioni moja, katika trilioni moja inayoenda kufanya projects ambazo ni current, unakuta ni shilingi bilioni 300, 400; shilingi bilioni 600, 700 inaenda kulipa madeni. Tutawezaje ku-execute kazi vizuri?

Mheshimiwa Naibu Spika, madeni ya wakandarasi yaje na mpango mzuri waweze kulipwa, tuokoe maisha ya wakandarasi. Tunapoteza dignity ya wakandarasi wetu wa ndani kwa sababu yao, leo mkandarasi haaminiki, huwezi kwenda sehemu kukopa akakubalika. Wanajua hata wakimkopesha, kuja kulipa ni changamoto. Serikali ilizingatie hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niweze kuchangia kwenye upande wa Jimbo langu la Musoma Mjini. Mimi kwanza ninaishukuru Serikali, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutuletea shilingi bilioni 35 ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma, ujenzi wetu umefika 67%. Ninaomba sasa Waziri atusaidie, huyu mkandarasi ana certificate yake ya shilingi bilioni 1.9, amlipwe, ili hizi 33% zilizobaki zikamilike na uwanja huo uweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea pia kuomba kuhusiana na Jimbo langu la Musoma Mjini. Barabara ya lami ninayo kutoka Nyabange mpaka Musoma Mjini, ila kwenye Kona ya Nyasho tuna changamoto ya mafuriko. Kila mvua ikinyesha wananchi wa Musoma Mjini wanateseka na mafuriko makubwa pale Kona ya Nyasho.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Daraja la Kona ya Nyasho liweze kufanyiwa ufumbuzi, watujengee daraja pale ili tuepukane na mafuriko katika eneo hilo. Ninaomba pia, hili lielekee upande wa TEMESA. Mheshimiwa Waziri tuna Kivuko chetu pale cha Kinesi, kile kivuko kwanza kina injini moja, anytime mnaweza mkasikia maafa yametokea katika Jimbo la Musoma Mjini na Rorya kwa sababu, kivuko kile siyo rafiki. Tumeshaomba na tuliahidiwa kwamba, tutaletewa kivuko kingine, mpaka leo kivuko hakijaja. Wananchi wanapata changamoto kubwa kuhusiana na kuvuka kutoka ng’ambo ya Musoma kwenda Kinesi na kutoka Kinesi kuja Musoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri, kaka yangu, nina imani bajeti yake itapita vizuri kwa sababu, changamoto ni fedha huletewi, ila ninachoomba akija ku-wind up hapa, atuambie maafa yanayoweza kutokea anytime pale Kinesi, anakuja kuya-rescue vipi, kwa sababu, tunahitaji kivuko, kwa ajili ya wananchi hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja. (Makofi)