Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Lucy Thomas Mayenga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu. Nimesimama hapa kwa heshima kubwa na taadhima kuomba kuhusu barabara yangu ya Kolandoto kwenda Mwang'ongo, maana dakika zenyewe ni chache.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii imekuwa ikiwekwa kwenye ilani tangu mwaka 2020. Vilevile tangu Mwaka 2020 imekuwa inatengewa fedha kidogo za bajeti, hata hivyo hakuna kitu chochote ambacho kimefanyika. Barabara hii ni ya muhimu sana kwa uchumi wa Jimbo langu la Kishapu na Wilaya yetu ya Kishapu, kwa ujumla ni barabara muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri. Yapo mambo mengine ambayo yako ndani ya uwezo wa Waziri na yako ndani ya uwezo wa TANROADS, lakini bado kuna mambo mengine ambayo kidogo yanakuwa yako nje ya uwezo wao. Ninamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, alikuja kwenye barabara ile akaitembelea, akaikagua na kuona hali halisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo ambalo lilikuwa halijawahi kutokea, hakuna Waziri ambaye ameshawahi kufika pale akafanya ukaguzi wa ile barabara akaona. Barabara hii inaunganisha wilaya kwa wilaya, lakini mpaka sasa, barabara ile ilikuwa haijawahi kuwekwa lami. Tuseme, kwa ujumla wake kwa historia, barabara ile haijawahi kuwekwa lami tangu uhuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana TANROADS, licha ya kazi nzuri ambazo inafanya, inafungua nchi, inasimamia barabara, hebu Mheshimiwa Waziri barabara yetu hii ya TANROADS ya kutoka Kolandoto, kupita Kishapu kwenda Mwangongo, ambayo ina kilometa 52.7 iweze kuwekwa lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wangu wamekuwa wakilalamika sana, wafanyabiashara wanabeba rangi zinamwagika, wafanyabiashara wa ujenzi wananunua gypsum, wanasafirisha kwenye barabara hii mbovu, gypsum zinavunjika. Hasara ambazo wamekuwa wakizipata, wafanyabiashara wengi wa aina mbalimbali, ni hasara kubwa sana. Ninaomba sana Wizara hii iichukulie barabara hii kwa uzito unaostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alipita kwenye jimbo langu mwaka 2025, tarehe 19 akasema, baada ya kusikiliza historia hii kwamba, barabara hii haijawahi kupata lami tangu uhuru, sasa hivi inakwenda kujengwa kwa lami. Ninaomba kwa heshima na taadhima, TANROADS, na Wizara hii ya Ujenzi, iweze kutimiza wajibu wake kwa kujenga barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara nyingine ambayo ni ya muhimu sana kwa uchumi wa Kanda ya Ziwa. Barabara hii inakwenda kuwa muhimu kwa mikoa zaidi ya sita kwenye Kanda ya Ziwa; hiyo ni Barabara ya Igunga – Igurubi – Manonga – Ukenenge, kupita Kolandoto, yenye urefu wa kilometa 90. Barabara hii, endapo kama ikitokea changamoto yoyote maeneo ya Igunga na Nzega, ndiyo alternative. Ninasikitika kwamba, barabara hii haipo kwenye mpango. Ninaomba Wizara iiweke barabara hii kwenye mpango ili iweze kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwa heshima zote na mapenzi yote tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya kwa kutenga fedha nyingi kwenye barabara. Nchi hizi za kimaskini, hasa za Kiafrika, ambazo zinakuwa na changamoto na priorities nyingi wakati, mwingine tunaweza tukalaumu kwamba, hiki hakijafanyika na hiki kimekwenda hivi. Mambo ni mengi, matatizo ni mengi na kila kitu ni cha muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tukizungumzia SGR, ni ya muhimu, tukizungumzia hiki ni cha muhimu. Tukizungumzia umuhimu wa barabara, kila mtu atasema Dodoma ni muhimu, mwingine atasema huku ni muhimu. Kwa hiyo, ninaomba Waheshimiwa Wabunge leo tumpitishie Mheshimiwa Ulega, mambo huwa yanakwenda na maendeleo huwa yanafanyika taratibu. Tupitishe hii bajeti, hata, hivyo kama ni kusikia Serikali imesikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana, kwa heshima zote na mapenzi yote, kama ni kusikia, kama ni kupigwa nondo wamepigwa za kutosha; kama ni kusemwa, wamesemwa vya kutosha na kwa kweli, ambaye atakuwa hajasikia atakuwa ana matatizo ya uziwi. Ahsante sana.

MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

MHE. LUCY T. MAYENGA: Sitaki taarifa zako na wewe! Hebu kaa chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kumalizia jambo moja kwa sababu, muda hautoshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ambalo ninapenda kuzungumzia.

MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lucy, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Sigrada Mligo.

TAARIFA

MHE. SIGRADA W. MLIGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba, yeye sio mamlaka ya kuizungumzia Serikali, itakuja itazungumza yenyewe. Yeye azungumze matatizo yake na asitushawishi.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lucy, Taarifa unaipokea?

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, huyu hajitambui, hata kumjibu nitapoteza muda. Ninataka nizungumzie jambo moja. [MANENO HAYA SIYO SEHEMU YA TAARIFA RASMI ZA BUNGE]

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lucy kwa kusimamia kanuni...

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei. Ni kwamba, jambo hili, sisi ni Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, hatuwezi kusema kwamba, hatuwezi kuizungumzia Serikali, pale ambapo inatakiwa kuzungumzwa lazima tuseme. Ni lazima tuseme, hatuwezi kunyamaza tu hivi hivi, kimyakimya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ninapenda kumalizia ni suala la ubora wa barabara. Wananchi wengi, hasa Wabunge, wamezungumza kwa machungu makubwa sana kwamba, ubora wa barabara kwa kweli unasikitisha. Lifespan ya barabara imekuwa ya muda mfupi, nadhani hili lingezingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja, bajeti itapita, mambo yatakwenda na kazi ziendelee. Ahsante sana. (Makofi)