Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Kwanza ninakupongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa ujenzi unaoendelea kwenye jimbo langu, kilometa 20, tunashukuru sana kwa sababu mkandarasi yupo site.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nimejaribu kusikiliza wachangiaji toka jana, kwa kweli kuna tatizo. Mimi ni Mbunge wa awamu ya tatu, Sheria hii ya Road Fund tulikuwemo mwaka 2019, ya ulinzi wa zile fedha za Road Fund. Sasa mara nyingi huwa tukisema tunaonekana kama hatueleweki, kwamba yalikuwa ni mawazo mazuri sana, watu walifanya research na sisi wengine wenye elimu za kawaida tukaungana na Mawazo, tukaweka ile sheria ya kulinda fedha zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kujiuliza, ikiwa mimi sijatoka Bungeni toka mwaka 2019, nimetoka tu kipindi cha uchaguzi 2020 na cha juzi, ni lini Bunge lilikaa likabadilisha hiyo Sheria ya Road Fund? Kama kweli huu mhimili tunauheshimu? Tulitunga wenyewe, tunaweza kubadilisha wenyewe. Ni nani ameingilia mamlaka ya kwenda kutoa Mfuko wa Road Fund kutokupeleka fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunatoka vijijini na ninataka niwape stori moja. Samahani sana mdogo wangu Mheshimiwa Makonda, nina message hapa Mheshimiwa nitakufowadia. Jana kuna gari imepasua matairi pale kwenye mlima Saranda, mtu mmoja nadhani ni fan wangu, akanitumia message ile gari ilivyo na matairi yake michelin yalivyopasuka. Halafu akaniambia ninyi Wabunge, yaani sisi tunahangaika na mashimo, ninyi mnatuletea Rio Ferdinand, ndiyo nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kujiuliza, hivi vitu, ndugu zangu leo hii hebu ondoka hapa nenda Mwanza uone hii barabara, ukitoka tu hapa kwenda kupata kwao Waziri Mkuu, ukisalimika kupasua tairi una bahati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ondoka Singida nenda Arusha; ondoka Arusha nenda Tanga; ondoka Dodoma nenda Morogoro; ondoka Dodoma nenda Mbeya, nenda Songea. Ndugu zangu kama tulikaa wenyewe humu ndani tukapitisha shilingi bilioni 956 mpaka leo tunaenda kumaliza mwaka mmepeleka shilingi bilioni 212 na fedha mmeshakusanya zote. Sasa tuzungumze nini sisi Wabunge? Tuzungumze nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Rais, kama anatusikiliza, apange ziara ya kupita kwa mguu pengine labda wanampitisha kwenye ndege haoni huku chini. Mimi ningekuwa ninaweza kuwa-convince Wabunge, tunge-cancel mipango yote ya mwaka huu tukarabati kwanza hizi barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, mimi nimekuwa dereva miaka sita, ninaendesha basi kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam, wakati huo wa rough road. Sasa hivi kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam ni sawa na rough road. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais, kafanya kazi nzuri ya kuifungua bandari yetu, tuna mizigo, tuna kila kitu, watu wote wanajua barabara za Tanzania ni nzuri. Ninataka niwaambie Watanzania na ndugu zangu Wabunge, ikiwa hizi nchi jirani zitatulia vurugu zilizonazo, watu wengi sana watatukimbia kwa sababu ya ubovu wa barabara kwenye bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni vizuri sisi kama Bunge, tuna uwezo, na tuna maamuzi, hatumshikii shilingi Mheshimiwa Ulega, maana hizi shilingi mwisho tutammalizia zote. Ningeshauri Wabunge, sisi kama Bunge, leo tukipumzika saa saba, Waziri Mkuu ni wa kwetu humu ndani, Waziri wa Fedha yupo humu, wakakae waje hapa wakati wa ku-wind up Waziri atatuambia fedha zinaenda lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa fedha wameshakusanya, wanazo shilingi bilioni 956, wanapeleka shilingi bilioni 211, haiwezekani. Haiwezekani, mtuhurumie! Tunaenda kujimwaga wote kutengeneza treni, ni jambo zuri sana, lakini wamefanya tathmini watu wangapi wanapita kwenye treni na watu wangapi wanapita barabarani?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajivuna tuna ndege, tunajenga airport, sawa. Watanzania wangapi wana-afford kupanda ndege? Wengi wapeni ambao wanapita kwenye barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba sana kwenye hili tusichukulie kama michango ya kawaida. Bunge tuna uwezo wa kusema tunahitaji majibu ya Serikali. Huyu Mheshimiwa Ulega hana fedha. Mwenyekiti, kasema jana tutamgawana, mpelekeeni fedha halafu tum-sue humu ndani. Mimi ni mwaka wa 15 sijawahi kuona Wizara ya Ujenzi inasulubiwa kama kipindi hiki tulichonacho kwa leo. Kwa nini hampeleki fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha wanakusanya, sheria tumetunga, halafu fedha haziendi! Ukienda kwenye akaunti ya Road Fund, leo kuna shilingi bilioni 56 mwezi wa Sita, mnatoboa tu kidogo mnataka kuzipiga au mnataka kufanya nini? Achieni pesa tukatengeneze barabara za wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri, tusikubali kabisa kuipitisha hii bajeti kabisa, kwa sababu najiuliza, mimi ni mwana CCM, wapi tumefungwa kusema ukweli? Lazima tuwaombe kama mnamshauri vibaya Mkuu wa Nchi, basi mshaurini tunahitaji fedha. Sisi tunaoishi maisha ya barabarani tunajua shida tulizonazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ukisoma ukurasa wa 50 nimeona Mheshimiwa Ulega amekuja na hati fungani. Mimi ninamshauri siyo suluhisho. Tulikuwa na Bond ya Mama Samia, ilifanya vizuri kwa 170%. Ipo wapi performance yake? Leo tena amekuja na karatasi nyingine; niwashauri sana Waheshimiwa Wabunge, Serikali itusikilize; na Mheshimiwa Waziri Mkuu, saa saba mkakae hili ni suala ambalo linaumiza watu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jaribu kutoka hapa leo kwenda kwako kule Babati Mzee Sillo uone barabara zilivyo. Tumetoka kwenye milima inayoua watu, tukaweka lami tukajisifu, tuziache tena jamani ziharibike hizi barabara! Tuliweka Sheria ya Road Fund ya kazi gani? Niwaombe sana Wabunge, tukaze ili leo tupate majibu kabla ya kumsulubu ndugu yetu Mheshimiwa Ulega hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, ninataka kutoa ushauri wa kitaalamu, mimi nimebobea kwenye usafirishaji. Mheshimiwa Waziri ...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba dakika moja kama Profesa maana mimi ni daktari.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, malizia sekunde 30.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninafanya kazi ya transport, ninauliza kwenye mizani tunaongoza Tanzania kwa foleni, lakini nimepita juzi ninafanya tathmini tu kwamba, wenzetu mlifikiria nini? Ninachukua mfano, gari za mafuta; ukinunua gari ya mafuta, lazima upeleke kupima calibration na Serikali ndiyo inapima. Huwezi kupakia zaidi ya calibration iliyoandikwa pale kwenye depot yenyewe ina mashine yake ambayo inapakia kufuata calibration. Imepimwa na Serikali, ina kibali cha Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu unaenda tena kwenye foleni, unaenda unapanga tena foleni masaa sita. Vile ni vitu vya mlipuko na ukijiuliza, nimekaa jana mzani mmoja ninajiuliza ngoja nione leo zinazozidi kama watashusha mafuta. Hakuna tanki, hakuna madramu, mnaweka foleni, jamani, mnahitaji akili ya ziada!

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Musukuma, tunashukuru.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama wanashindwa, waniazime mimi niwarekebishie haya mambo ili tuweze kwenda sawa. Ninakushukuru sana. (Makofi)