Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiteto
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa nafasi, na kwa sababu ya muda tutapongezana baadaye. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Manyara ni mkoa wa nane Tanzania Bara kwa ukubwa na barabara za TANROADS ni kilometa 1,657. Zenye lami peke yake ni 259, na barabara kuu kati ya hizo ni 207, barabara za mkoa ni kilometa 52 peke yake ndiyo zenye lami. Sasa rafiki yangu Mheshimiwa Waziri Ulega, haiwezekani Mkoa wa Manyara, mkoa wa nane kwa ukubwa iwe na kilometa 52 peke yake, haiwezekani! It is a big job. Kwa hiyo, kwa kweli Wizara ikakae vizuri ilete fedha kwa ajili ya barabara za Mkoa wa Manyara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara za EPC+F tulisaini mikataba tarehe 16/6/2023. Barabara ya Kongwa – Kiteto – Simanjiro - Arusha ilikuwepo kati ya barabara ambazo tulisaini mikataba na sifa zake mnafahamu. Barabara ya Kongwa inaunganisha Mkoa wa Dodoma, Manyara na Arusha. Sisi tumekubaliana hapa kwamba sera yetu, tuunganishe barabara za mikoa kwa mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Handeni – Kiberashi – Kibaya – Njoro – Chemba - Singida ilikuwepo kwenye barabara hii ya EPC+F, tulisaini mikataba tangu tarehe 16/6/2023. Tulifahamishwa kwamba kulikuwa na tatizo kwenye EPC+F na tukaelewa, lakini bajeti iliyopita walisema wameyeyusha mikataba na kwamba barabara hizi zitajengwa. Kwa ushauri wa kisheria wa bure kabisa, unaposaini mikataba, ni sharti uzijenge barabara hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka historia kuwa Rais wa kwanza aliyeweka fedha nyingi sana kwenye kilimo. Ni shilingi trilioni 1.2 bajeti ya mwaka 2025 na shilingi trilioni 1.1. Sasa hii maana yake nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka kuacha legacy kwenye kilimo, lakini bila barabara inayotoa mazao hatutaweza kuwa tumemtendea haki Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuacha legacy ya barabara hiyo. Kwa hiyo, hizi barabara mbili za Tanga - Manyara mpaka Singida ni barabara za wakulima, ni barabara zitakazochochea kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wale Mawaziri kama hawataki kuelewa na ninaomba nimnukuu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hapa alipokuwa Tanga, akizungumzia Barabara ya Kiberashi – Kiteto - Chemba mpaka Singida ninanukuu: “Barabara hii ni muhimu sana kwa maendeleo yetu ya bandari. Nimezungumza na Waziri, hii barabara tuifanye kwa PPP, tusiwaachie Wizara ya Ujenzi, hii barabara haitakwenda haraka.” Sasa kitu gani hakieleweki hapa, nukuu nzito sana, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan analifahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, anataka barabara hii ijengwe kwa haraka na kaagiza Wizara mbili: Ujenzi na Uchukuzi sasa kwenye bajeti ukurasa wa 217, Mheshimiwa Ulega bado anatuambia eti hii barabara ipo kwenye PPP, it is not enough. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alishatoa na hii kauli ni ya maelekezo. Rafiki yangu, huo ni ushauri mwingine wa kisheria. Tofauti ya ahadi na maelekezo, ushauri wa kisheria huo, take it or leave it, lakini ni ushauri. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, alivyokuja Mheshimiwa Waziri Mkuu na tumpongeze sana, alitumia barabara hii ya Kongwa mpaka Arusha karibu kilometa 453. Mwenyezi Mungu alitusaidia na mvua ikanyesha vizuri sana, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema hivi: “Nikirudi Dodoma nitaitisha kikao cha dharura haraka sana kwa ajili ya hii barabara.” Mheshimiwa Ulega, hata hii kauli huielewi? Haya ni maelekezo, sawasawa! Yaani hapa leo ningesema tutakamata shilingi, ninadhani hata Waziri Mkuu ataniunga mkono kwa sababu ya kauli hii. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua sisi ni waungwana sana, sasa msitake tuwe wakorofi. Jambo lingine la kisheria, unajua mimi na Mheshimiwa Ulega ni marafiki, sasa na kisheria huwa urafiki pia unakuwa reviewed ikiwa kama haueleweki eleweki hivi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunataka sana baadaye utupe kauli kuhusu barabara hizi mbili. Kwa hiyo, kwa kweli ninaunga mkono with condition kwamba utatupa baadaye kauli nzuri ya kuridhisha, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)