Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi ninashukuru kwa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii ya Ujenzi. Kwanza kabisa, nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake na dhamira yake ya kuendelea kuijenga na kuboresha Mkoa wa Dar es Salaam, kupitia uwekezaji wa miundombinu ya barabara zinazoendelea kwenye mkoa wetu. (Makof)
Mheshimiwa Naibu Spika, chini ya uongozi wake, tumeona ujenzi unaoendelea Dar es Salaam, umebadilisha mwonekano na umeendelea kuboresha ubora wa mkoa ule, kwa sababu Dar es Salaam ndiyo mkoa unaobeba sura ya Taifa letu la Tanzania, kazi kubwa imefanyika. Bado kuna upungufu, lakini kwa hiki kilichofanyika, hatuna budi kushukuru na kuipongeza Wizara na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nimpongeze Waziri wa Ujenzi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu nzima, kwani wanafanya kazi nzuri, sisi wananchi wa Dar es Salaam tumeona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi unaoendelea Dar es Salaam, umesaidia kupunguza foleni, kwa sababu barabara za ndani zimeboreshwa. Tumeona taa zimewekwa ambazo zinasaidia kuongeza uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam. Sasa hivi wananchi wa Dar es Salaam wanafanya biashara mpaka usiku. Kama tunavyofahamu, Mkoa wa Dar es Salaam, nature yake ni biashara. Kuna wanaofanya biashara asubuhi, lakini wengine wanafanya biashara usiku kwa sababu ya miundombinu iliyoboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ukishuka hata stendi ya Magufuli usiku, pembezoni mwa barabara utaona biashara zinaendelea, hususan wanawake wajasiriamali wamekuwa wakiuza pipi, karanga, na matunda usiku. Haya yote yamefanyika kutokana na ujenzi ulioendelea, miundombinu iliyoboreshwa ndani ya mkoa wetu wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi ule umeongeza hadhi ya mkoa wetu. Mtu aliyeondoka Dar es Salaam, miaka 10 iliyopita akirudi leo lazima anaona mabadiliko makubwa na anaweza hata akapotea. Kwa hili, hatuna budi kuishukuru Serikali na kuipongeza Wizara kwa kazi inayoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa miundombinu hii umesaidia pia kuongeza thamani ya maeneo ya Dar es Salaam. Leo hii watu wanapungua Dar es Salaam na kupunguza msongamano, wanakwenda pembezoni kununua viwanja, kujenga, lakini hata vile viwanja ambavyo watu walikuwa wanauza kwa bei rahisi, sasa hivi thamani imepanda kwa sababu ya miundombinu. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali iendelee kuboresha barabara za Dar es Salaam, kwa sababu Dar es Salaam ndiyo mkoa wenye wananchi wengi kuliko mikoa yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanaingia Dar es Salaam kila siku, ongezeko ni kubwa. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali, miundombinu iendelee kuboreshwa ili watu waendelee kuja, waendelee kutengeneza fedha, kwa sababu Dar es Salaam ndiyo mkoa unaoingiza uchumi mkubwa na unaongeza pato kubwa la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha shughuli za Uchumi, lakini tuna maombi ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam. Kazi kubwa imefanyika, lakini kuna vitu bado tunaomba. Tunaomba uboreshaji wa miundombinu ya barabara za ndani uongezeke kupunguza msongamano wa barabara kuu ambazo zinatumika na watu wanaoingia na kutoka mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dar es Salaam watu wote asubuhi wanatoka wanatawanyika kwenda kutafuta vipato, jioni watu wote wanarudi. Kwa hiyo, tena barabara nyingi za ndani ili kupunguza msongamano na watu wafanye shughuli zao kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba pia kufunguliwa kwa barabara ambazo ujenzi unaendelea, barabara zile nyingi zimefungwa. Kwa hiyo, zilizokuwa zimekamilika waruhusu watu wapite kupunguza msongamano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, tunaomba taa za barabarani. Ni kweli taa zimewekwa, lakini kuna maeneo mengine tumeona taa zimewekwa, lakini bado hazina ubora. Ukiangalia mfano barabara ya Chuo Kikuu kupita Makongo – Goba kumeanza kuwekwa taa. Taa zile zimewekwa mbalimbali sana ukilinganisha na maeneo mengine, lakini bado ni taa ambazo hazina mwanga wa kutosha, kwa hiyo, inakuwa kama hazisaidii. Tunaomba mkandarasi anayeweka taa zile aboreshe, ziwekwe taa zenye viwango ambazo kweli zilete thamani ya taa za barabarani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba pia uboreshaji wa mifereji katika ujenzi unaoendelea ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, kwa sababu Dar es Salaam, ikinyesha mvua ndogo tu mafuriko. Kukishakuwa na mafuriko ndani ya barabara zile tayari inaleta msongamano mkubwa sana. Inakuwa changamoto kubwa kwa watoto wanaokwenda shuleni na hata watu wanaokwenda maofisini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi unaoendelea Dar es Salaam kwenye barabara nyingi umeinua vipato vya wananchi wa Dar es Salaam. Mama Lishe na Baba Lishe waliokuwa wanapika kilo tano kwa siku, sasa hivi wanapika mpaka kilo 30. Vijana wanaouza vinywaji (maji, juisi, na soda) walikuwa wanauza katoni mbili, tatu, sasa hivi wanauza mpaka 10. Kwa hiyo, tunaomba ujenzi uendelee. Tunatamani ujenzi uendelee, huku tunatamani ujenzi uishe, kwa sababu unavyoendelea, uchumi unaongezeka, ukiisha pia utakuwa na faida kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Wizara, tuna Barabara ya Kimara Mwisho kupitia Bonyokwa hadi Kinyerezi. Barabara hii tunaomba ijengwe kwa viwango cha lami kama Serikali ilivyokuwa imetaka ifanye, kwa sababu toka mwaka 2024, mkandarasi ametoa vifaa pale, wananchi wale walikubali kupisha kwenye maeneo yale bila kulipwa fidia, kitu ambacho ni kikubwa na kizuri sana. Sasa hawaoni kinachoendelea, wanaacha kufanya shughuli zao za kiuchumi, hawaendelezi maendeleo yoyote na hawana taarifa yoyote nini kinaendelea, toka mwaka 2024 mpaka leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Serikali iangalie barabara hii, imekuwa na msaada mkubwa sana na ina tija sana kwa wananchi hawa na ndiyo maana kwa hiyari yao wakapisha bila fidia. Tunaomba Mheshimiwa Waziri, hili lifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tuna Barabara ya Msongola – Kivule – Kitunda - Banana na Barabara ya Majohe kwa Warioba na Majohe Ngozoma. Barabara hizi zimeharibika sana kutokana na mvua zinazoendelea ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Wizara, katika ukarabati unaoendelea, Mheshimiwa Waziri hapa alisema, ujenzi utaendelea baada ya mvua kwisha. Tunaomba hizi zifanyiwe haraka sana, zimekwamisha uchumi wa wananchi wa maeneo haya, watu hawafanyi shughuli zao, watoto wanashindwa kwenda shule na kufika kwa wakati. Mtoto anatoka nyumbani asubuhi saa moja, anafika shuleni saa nne, amepitwa na vipindi. Tunaomba hizi barabara ziangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna changamoto ya malori njia ya Bandari kwenda Kigamboni. Wananchi wanahama, wanaacha nyumba zao kwa sababu ya changamoto hii.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru, na ninaunga mkono hoja. (Makofi)