Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Hatimaye ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumpongeza kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika maeneo yote, na hasa kwenye eneo hili la sekta ya barabara. Hongera sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, ninampongeza Waziri na Katibu Mkuu na viongozi wale wote. Ninampongeza Waziri kwa uwasilishaji wake ambao umegusa maeneo yote katika Wizara yake. Sambamba na hili, wakati anaeleza, ameeleza vipaumbele sita katika kuwasilisha hii bajeti ya Wizara yake ya Ujenzi. Vipaumbele hivyo ni kama vifuatavyo:- (Makofi)

(i) Kuendelea na ujenzi wa barabara;
(ii) Kuendelea na barabara zinazounganisha mikoa; na
(iii) Kuendelea na kuimarisha usafiri wa miundombinu pamoja na vivuko na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, nikianzia na suala zima la barabara, ni kama ambavyo wachangiaji wengi wamezungumza kuhusu barabara za mikoa na barabara zinazounganisha mkoa mmoja na mkoa mwingine na barabara zile za kimkakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi ninataka nieleze kwamba, kipaumbele chetu au kipaumbele ukienda ndani ya Mkoa wetu wa Lindi, hii ni barabara inayounganisha mikoa zaidi ya minne. Ni barabara inayounganisha Taifa hili na Taifa lingine. Hii ni barabara ya Lindi – Kibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara hii ya Lindi – Kibiti ni muhimu sana katika uchumi na ustawi wa maisha ya watu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, tulipata kadhia kubwa ambayo haijawahi kutokea katika maisha tunayoyafahamu kwa karne nyingi. Ikatokea mafuriko, mafuriko yale yakaharibu miundombinu ya barabara hii yote kuanzia Dar es Salaam mpaka unafika kule Lindi. Kilwa ndiyo ilikuwa usiseme, iliharibika yote na watu walikaa njiani kwa muda kadhaa. Hawavuki kutoka Pwani kuelekea Lindi hatimaye kuelekea Mtwara, hatimaye kuelekea Ruvuma hatimaye hata wale wanaoelekea Mozambique hawakuweza kuvuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, alitoa fedha nyingi, na yale madaraja yote yakajengwa. Baada ya ujenzi wa madaraja yale, hawakumaliza tu kujenga madaraja, halikadhalika hata taa za barabarani zilifanyaje? Ziliwekwa katika madaraja yale isipokuwa daraja moja tu. Wamejenga hatimaye taa za barabarani hazikuwekwa. Hili ni Daraja la Mbwemkuru. Sasa sijui hakukuwa na bajeti au hakukuwa na nini sijui! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri atambue na ajue ya kwamba, barabara hii ya Lindi – Kibiti ndiyo barabara pekee ya tumaini, na ndiyo barabara pekee ya uchumi, na sisi hatuna njia nyingine yoyote ya usafiri zaidi ya barabara hii ya Lindi – Kibiti. Ukitaka kwenda Lindi, kama daraja moja likiharibika ina maana hufiki Lindi, na haufiki sehemu yoyote ndani ya Mkoa wa Lindi, hata Mkoa wa Mtwara hata Mkoa wa Ruvuma hata huko Mozambique huwezi kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nini tunachohitaji? Tunachohitaji pamoja na yote, barabara imejengwa, madaraja yamejengwa vizuri, basi kuwe na njia mbadala, tusiwe na barabara moja tu. Tunahitaji hata kama isipokuwa kesho au keshokutwa, tunahitaji Mkoa wa Lindi na mikoa yetu ya Kusini kuwe na SGR. SGR ni muhimu sana kwetu. Mtengeneze mazingira, ama sivyo! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumzia asubuhi kwenye swali kuhusu suala la uwanja wa ndege. Ule uwanja wa ndege upo miaka mingi, lakini mpaka leo umeachwa. Tunazungumzia suala la LNG; LNG haiwezi kuwepo bila kuwa na uwanja wa ndege wa Mkoa wa Lindi. Ninaomba Mheshimiwa atakapokuja kuhitimisha, hili ni muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, ninaenda kwenye jimbo langu la Mchinga.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba univumilie kwa dakika moja. (Kicheko/Makofi)
NAIBU SPIKA: Ninakuongeza dakika moja.

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninakushukuru kwa hiyo dakika moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye Jimbo langu la Mchinga kama siku zote ambavyo ninasema, Jimbo la Mchinga ni jimbo pekee ambalo nikisema, hatimaye huko wataandika. Waandike tu, nami nimechaguliwa kwa ajili ya kuwatetea wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mchinga halina lami hata kidogo. Hata pale kilometa moja sijui nukta mbili kwenda kwenye shule ya wasichana imejengwa hivi karibuni. Leo ninapata taarifa daraja lile lime-sink. Sasa, huu ni ujenzi wa aina gani? Ninataka hii barabara ijengwe, lakini ninataka lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia kuunganisha makao makuu ya mkoa, hatuunganiki sisi. Jimbo la Mchinga limejifunga. Ninataka Mheshimiwa Waziri akija hapa anipe uhakika jinsi ya kuliendeleza Jimbo la Mchinga ambalo halina lami hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha tumepatiwa. Baada ya kupatiwa fedha hizo, sijui wanasema kuna mikataba gani haijaenda vipi! Ninataka nielezwe, aidha anieleze hapa au nitamtafuta huko aniambie kitu gani kinachokwamisha fedha zile zilizotolewa na Serikali, mikataba ile isiwe sawasawa na wakaanza kujenga? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kwa kweli ninachohitaji, Barabara yetu ya Lindi ijengwe kwa kiwango, ifumuliwe yote, hatimaye ijengwe upya. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)