Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Mecktridis Fratern Mdaku

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti wa Wizara ya Ujenzi ya Mwaka huu wa Fedha 2026/2027.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Morogoro ni mkoa unaochangia kwa asilimia kubwa sana pato la Taifa, lakini mkoa huu umekuwa na changamoto kubwa za barabara. Waheshimiwa Wabunge wenzangu jana walikuwa wametangulia kusema na kuongelea barabara zote za Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nami nimeona nianze na hili kwa Serikali iweze kutupa kipaumbele Mkoa wa Morogoro ili zile barabara ziweze kurekebishwa na nyingine kujengwa, ili Morogoro iendelee kuwa kitovu cha uchumi wa Taifa hili kwa sababu pato la Taifa linachangiwa kupitia sekta ya kilimo, lakini pia utalii, madini, lakini pamoja na maliasili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuongelea Jimbo langu la Malinyi. Jimbo la Malinyi limekuwa kisiwani, tuseme pembezoni, lakini ni kama bakuli, linapokea maji kutoka maeneo mbalimbali ya miinuko. Mvua zinanyesha kwingine, Malinyi tunapata mafuriko. Hali hii imeathiri sana barabara zetu za TARURA na TANROAD kule Malinyi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ni shahidi, alikuja kule Malinyi mwaka 2025 mwezi wa Nne akaona hali halisi ya mafuriko, lakini akaona Madaraja ya Namhanga pamoja na la Mto Fuluwa likiwa limesombwa na maji. Aliahidi kuwa mwezi wa Saba mwaka 2025 lile daraja lingekuwa limeanza ujenzi, lakini mpaka leo ni mwaka sasa na miezi minne, ujenzi wa Daraja la Mto Fuluwa haujaanza, wala pale Namhanga, walianza kidogo lakini wamekwama. Mkandarasi haonekani site, hamna kingine chochote kinachoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, madaraja haya yamekuwa ni changamoto kubwa sana kwa usafiri na usafirishaji wa mazao, na pindi tunapopata misiba, wananchi wamekuwa wakipata shida sana, kwa sababu Daraja la Mto Fuluwa linaunganisha kata nne; Kata ya Sofi, Kata ya Mtimbila, Kata ya Igawa pamoja na Kata ya Biro. Wananchi wanapata misiba, lakini wanashindwa jinsi ya kwenda kuzika, inabidi wengine wazikwe huko huko upande mwingine, ng’ambo nyingine, wengine wazikwe huku.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Serikali iangalie suala hili la haya madaraja. Ninashukuru Mheshimiwa Waziri ameniahidi, amesema kuwa akimaliza bajeti hii atafika kule Malinyi na kusema ule ujenzi utaanza lini na kuzungumza na wananchi wa pale Malinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuongelea na barabara ya lami kilometa 112 kutoka Ifakara – Lupiro – Mtimbira. Hii barabara imekuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, zaidi ya ilani sita. Pia bado kwenye kitabu cha bajeti cha Wizara ya ujenzi imekuwa ikitajwa kila mwaka. Leo tena nimeona kwenye page ukurasa wa 26 imeelezwa kuwa wanaenda kujenga barabara ya lami kilometa 112 kutoka Ifakara – Lupiro – Malinyi na mkandarasi yupo anajipanga ili kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, haya yanakuwa ni maneno tu. Nami ninaiomba Serikali, kwa wananchi wa Malinyi ambao ni wilaya inayozalisha kwa kiasi kikubwa mazao ya ufuta, mpunga, korosho, pamoja na mazao mengine, na bado yana mazao mengine ya kimkakati, barabara hii ni muhimu sana. Kujengwa kwa barabara hii kutafungua fursa nyingi katika Wilaya ile ya Malinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba barabara hii ipewe kipaumbele cha aina yake. Katika Mkoa wa Morogoro, Wilaya ya Malinyi ndiyo wilaya ya kwanza inayozalisha chakula kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda pia kuongelea barabara ya kutoka Malinyi – Luchemba – Londo – Namtumbo. Barabara hii ni miaka mingi inawekwa kwenye ilani, na barabara hii pia ni miaka mingi inazungumziwa. Barabara hii inaenda kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Ruvuma, lakini bado haipewi kipaumbele kinachostahili. Barabara hii itakapokwenda kufunguliwa fursa nyingi zitafunguka. Tutafungua fursa za biashara, uwekezaji, utalii, madini, kilimo, pamoja na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa katika pande hizi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba sana Serikali yetu iweze kwenda kufungua hii barabara, kwani ni muhimu kwa mikoa yote miwili pamoja na watu wengine watakaotumia barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, bado Malinyi tuna tatizo la kivuko ambacho ni barabara ile inayounganisha Malinyi kwenda Wilaya ya Mlimba, Kivuko cha Kikove. Huu mradi umeanza mpaka sasa ni miaka tisa, lakini haujakamilika mpaka sasa. Kila siku kunakuwa na changamoto hizi na zile. Gutter zinajengwa miaka minne, mitano, wanajenga gutter tu. Kivuko nacho mara kimekamilika mara bado hakijakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Wizara ya Ujenzi kufanya tathmini ya kina kujua tatizo la huu mradi, kwa nini unakwamba mpaka leo unaenda mwaka wa 10 na kitu? Kilichobaki ni kidogo tu. Sidhani kama hata shilingi milioni 400 inafika kukamilisha ule mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali pia kupitia Wizara ya Ujenzi kwenda kukamilisha huu mradi wa Kivuko cha Kikove pamoja na kinachounganisha Wilaya ya Malinyi pamoja na Mlimba.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi anapohitimisha bajeti yake hapa, atuambie, ni lini barabara hii ya kilometa 112 na barabara ya kuunganisha Malinyi – Namtumbo zinakwenda kujengwa? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)