Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Mhe. Dickson Nathan Lutevele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangie kwenye Wizara hii muhimu. Kusema ukweli ninaomba nielekee moja kwa moja kwenye uchangiaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kwa kuzungumzia barabara tatu na nitatumia muda wangu vizuri sana. Sisi katika Wilaya yetu ya Mufindi tunayo barabara ya kimkakati, barabara inayotoka kwenye Jimbo langu la Mafinga kwenda Mgololo. Barabara hii ina kilometa 81.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii Wabunge wenzetu kwa kipindi cha miaka 20 humu ndani wameshiriki kupitisha bajeti za barabara za nchi hii ikiwemo barabara yetu ya Mgololo, lakini hivi ninavyozungumza barabara ya Mgololo hata kilometa moja haijawahi kujengwa. Jambo hili linatufedhehesha na linatusikitisha sana sisi Wanamufindi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, alipokuja tarehe mbili kwenye ziara wilayani kwetu alitoa maagizo kwa Wizara kwamba anatoa wiki mbili awe mkandarasi amepewa advance payment kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii, pamoja na barabara ya Nyololo, Igowole kwenda Mtwango. Hayo ni maelekezo ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, barabara hii ilikuwa na maagizo ya Mheshimiwa Rais. Sasa kwa sababu wiki mbili zimeshaisha tangu tarehe mbili, ninaomba Waziri atakapokuja atuambie je, huyu mkandarasi tayari yuko site, ama amepuuza maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu? Jambo hili Mheshimiwa Ulega atakapokuja ninaomba atuambie. Sisi Wanamufindi kusema ukweli jambo hili halitupi furaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni barabara ya kutoka Kinyanambo kwenda Madibila. Hii barabara ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwamba tutengenezewe kiwango cha lami kilometa 20. Tuliishukuru na kuipongeza Wizara, walianza kwa kutengeneza kilometa 1.2, maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kilometa 20, lakini wakaanza kilometa 1.2. Nayo kilometa 1.2. ninavyoongea leo, mimi tangu nimeingia humu Bungeni, nimeanza kudai hii barabara kwa sababu imefumuliwa, watu wanapata vumbi wakati wa jua, wanapata tope wakati wa mvua. Kilometa 1.2 mpaka leo haijafanyiwa chochote na mkandarasi hayupo site.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu Mheshimiwa Waziri aniambie, furaha ya kuunga mkono bajeti hii inatoka wapi kama kilometa 1.2 nalo limekuwa tatizo? Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie tatizo ni nini? Sisi watu wa Nyanda za Juu Kusini tuna shida gani, kama barabara ya kilometa 1.2 nayo inakuwa shida? Ninaomba sana mambo haya atakapokuja Waziri atuambie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, sisi tunaamini kwamba kauli ya Mheshimiwa Rais ni kauli ya mwisho. Mheshimiwa Rais akitoa kauli ni kauli ya mwisho, na wananchi wanashangilia kweli kweli. Kwa nini Wizara inakuwa haitekelezi barabara hizi za kimkakati?

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Mafinga kwenda Madibila ni barabara ambayo ndiyo sehemu ya skimu ya chakula inayolisha Mji wa Mafinga. Mpaka leo barabara ile siyo nzuri, wakati wa mvua haipitiki kabisa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, iko barabara inayotoka Kinyanambo kwenda Itimbo, inapita mpaka kwenda Kisusa mpaka Mlimba. Barabara hii tumeambiwa imefanyiwa upembuzi ya kinifu. Sasa, umeanza upembuzi yakinifu, ndizo lugha alizotoka kuongea Mheshimiwa Kunti hapa. Itakuwa upembuzi yakinifu, sijui mtaala elekezi, sijui hali ya hewa, miaka 20 inaisha. Tunaomba Wizara hii pamoja na kazi wanazozifanya, wawe na kauli ambazo zinatekelezeka. Vinginevyo Wabunge tutalaumiwa, lakini ukweli ni kwamba kule majimboni hali ni mbaya na tunashindwa kufanya ziara wakati wa masika kwa sababu unaweza ukapigwa mawe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ni mbaya, hata hizo zilizotengenezwa kwa kiwango cha changalawe hazipitiki. Ametoka kuzungumza Mheshimiwa Paresso hapa, ubora wa barabara ni kitu muhimu sana, barabara zetu hata hizo za changarawe hazitengenezwi kwa ubora. Wewe mtu culvert anakwenda kuweka mlimani wakati maji yanajaa bondeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana barabara zitengenezwe kwa ubora. Hapa ndani hata kama tutapongezana vipi, kama hali halisi kule haiwezi kuwa nzuri tutakuwa tunadanganyana. Tunaiomba hii Wizara kwa sababu ndiyo inayobeba uchumi wa nchi, wakandarasi na watu wetu wanaofanya kazi kule wafanye kazi kwa kutumia weledi na uzoefu walionao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kaka yangu Mheshimiwa Ulega yeye anajua, ninampenda sana, lakini leo kwenye hoja ya barabara, kama hatatoa majibu ya haya niliyoyasema, nakamata shilingi kwa sababu bila kufanya hivyo nami 2030 hapa ndani sitarudi. Ninaomba sana jambo hilo alizingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kushikilia shilingi. (Makofi)