Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu ambayo ni Bajeti ya Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika sekta hii. Vilevile, nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi ambazo zinaendelea kufanyika na zinaonekana zimefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba tunapojenga barabara zetu kwa kiwango cha lami, ndivyo ambavyo tunachochea ukuaji wa uchumi wa eneo husika, na uchumi wa nchi kwa ujumla. Ni muhimu sana Serikali ikaipa vipaumbele barabara zote ambazo zinaenda kusaidia na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo husika na hasa zile barabara za kimkakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wetu wa Arusha ni mkoa wa kitalii, lakini ni mkoa ambao unaandaa mashindano ya AFCON itakapofika 2027. Tunatambua kwamba kuna jitihada zinaendelea na tayari kuna mikataba imeshasainiwa ya barabara zinazoelekea kwenye uwanja kujengwa kwa kiwango cha lami. Matumaini yetu sisi Wabunge wa Mkoa wa Arusha ni kwamba barabara hizo zitakamilika kwa wakati ili ziweze kuendana na mashindano hayo ya AFCON katika mji wetu wa Arusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Wilaya ya Karatu tuna barabara muhimu tatu ambazo zinasimamiwa na TANROADS, tuna barabara ambayo sasa inatumika ya Makuyuni kuelekea lango la Ngorongoro ambayo ni barabara ya muda mrefu na bado ina hali nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Barabara ya Karatu – Mbulu kwa kilometa 75 na tuna Barabara ya Njia Panda - Mang’ola kuelekea Lalago yenye urefu wa kilometa 129. Hizi zote ni barabara ambazo zinahudumiwa na TANROADS mkoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwa kweli kumpongeza sana Meneja wa TANROADS Mkoa, pamoja na timu yake. Wamekuwa wakijitahidi kufanya matengenezo ya mara kwa mara na ninajua hata sasa matengenezo yanaendelea kwa kiwango cha changarawe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na uhitaji wa muda mrefu wa barabara hizi kujengwa kwa kiwango cha lami, na tumekuwa tukiahidiwa muda mrefu kwamba barabara hii itajengwa. Pia, mara nyingi tumeuliza Bungeni, tunaambiwa upembuzi yakinifu, usanifu umekamilika lakini bado hatujaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, matumaini yetu sisi wananchi wa Karatu hasa kwa hii Barabara ya Njia Panda - Mang’ola kwenda Lalago sasa itajengwa kwa kiwango cha lami. Umuhimu wa hii barabara labda nieleze ili tuone ina umuhimu kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa Wilaya yetu na uchumi wa Mkoa kwa ujumla. Kwanza ni barabara ya kitalii, ndiko ambako wageni wetu wengi wanaenda kuangalia kabila maarufu la Wahadzabe ambao wako hapa nchini ambapo kama tunavyowajua hao kina Chabba wako kule. Kwa hiyo, barabara hii inatumika sana kwenda kwenye eneo hilo na watalii kufika katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara pia ndiko ambako inaelekea Hospitali ya Wilaya. Hapa sasa nichukue nafasi hii kwa kweli kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake. Nimeona kwenye bajeti wametenga kilometa tano ambayo itaenda mpaka Hospitali ya Wilaya kujengwa kwa kiwango cha lami. Tunawashukuru sana kwa hili, na hii ndiyo maana halisi ya kazi na utu. Wamezingatia utu kwa wananchi wetu wa Karatu wanapoenda kupata huduma katika Hospitali yetu ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, barabara hii ndiko ambako kuna kilimo kikubwa cha umwagiliaji. Wananchi wa eneo husika wanalima vitunguu maji na vitunguu hivi vinasafirishwa nje ya nchi. Wanunuzi wetu wakubwa ni watu wa Kenya, Uganda, na South Sudan. Kwa hiyo, barabara hii pia ni muhimu sana kwa uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kuwa tumepata kilometa tano, bado kilometa 45 angalau ifike mpaka eneo la Mang’ola. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri azingatie tuweze kupata hizo kilometa zilizobaki kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii pia ndiko ambako sasa hivi wanaendelea na utafiti chini ya shirika letu la TPDC kutafuta mafuta. Utafiti unaendelea na hatua imeshafanyika nzuri. Kuna uwezekano mkubwa wa kupata mafuta katika eneo hilo katika Ziwa Eyasi. Kwa hiyo, tunaona umuhimu wa barabara hii, tunaomba sana Serikali iizingatie na kufikiria kukamilisha hizo kilometa chache tuweze kupata kwa kiwango cha lami barabara husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nitoe shukrani na pongezi kubwa kwa Serikali kwa upanuzi wa uwanja wa Lake Manyara Airport. Tumeona kazi inaendelea na kazi inafanyika. Kwa kweli kwa upanuzi wa uwanja huo ni uthibitisho kwamba utachangia kwa kiwango kikubwa ongezeko la utalii au watalii katika eneo letu la Karatu ambao wanaenda kufanya utalii katika Hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kazi inaendelea. Ni matumaini yangu kwamba kazi ile haitaweza kusimama, itaendelea na uwanja ule utakamilika na utaanza kutumika ikiwa ni kichocheo muhimu sana cha utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tuna barabara hii ya kuanzia Singida kwenda Katesh – Dareda mpaka Babati. Ile barabara sasa hivi ukipita ina mashimo makubwa mno, barabara imeharibika, haipitiki. Tuna imani barabara ile sasa itatengenezwa na itaweza kupitika kama ambavyo ilikuwa inapitika huko kwa kuwa ni barabara muhimu sana, inaunganisha Mkoa wa Singida, Mkoa wa Manyara kuelekea Mkoa wa Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, ninaomba kusisitiza sana umuhimu wa ubora wa barabara zetu. Kwa kweli tunaongea hapa, tunaomba na tunasisitiza na fedha zinatengwa, unaona kabisa fedha inatengwa barabara inatengenezwa lakini ile life span ya barabara huwa hazifiki. Kwa hiyo, ni muhimu sana Serikali ikazingatia ubora wa barabara tunazotengeneza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Profesa Muhongo ameeleza hapa vizuri jinsi ambavyo tutatengeneza ubora wa barabara kwa kiwango kinachotakiwa, ndivyo ambavyo barabara hiyo itadumu zaidi na ndivyo ambavyo sasa Serikali itaelekeza nguvu kujenga barabara nyingine, na hii ikaendelea kudumu. Kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba Serikali itazingatia jambo hili na barabara zetu zitakuwa bora na zitadumu kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi, na ninaunga mkono hoja. (Makofi)