Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa muda. Ninadhani malalamiko ni makubwa. Kwa hiyo, unipatie muda niwapatie na sehemu ya kutafuta fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Profesa Muhongo ni dakika sita kwa kila Mbunge, orodha ni ndefu sana…

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, kwa hiyo, nenda kwenye hoja moja kwa moja.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wawili wameshasema wananipa muda wao. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote hapa tukifanya utafiti kwenye Majimbo yetu sasa hivi, Serikali imefanya makubwa sana. Watu wanachokiomba sasa hivi kwenye kila Jimbo: moja ni maji; pili, umeme; na tatu, ni barabara. Bajeti yetu hii ya shilingi trilioni 62 hata tukitoa kwenye hivi vitatu tu hazitoshi. Kwa hiyo, tatizo hapa ni fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kwangu Musoma Vijijini. Sisi tuna barabara moja kuu inaunganisha kata 21, vijiji 68, vitongoji 374. Barabara moja tu, lakini hatuna lami. Tumeshajengewa kilometa tano, tender zimetangazwa mbili. Tender ya kwanza aliyeshinda alikuwa mtu bingwa kweli kweli wa Uganda nilimfuatilia; lakini kosa walilofanya TANROADS ni kuchukua mkandarasi mmoja ambaye majadiliano yao yalichukua muda mrefu kwa sababu alijua yuko peke yake, lazima wafuate matakwa yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa imetangazwa tena. Hii barabara imetangazwa tender mara ya pili. Kwenye bajeti iko ukurasa wa 83, ukisoma pale hata yule wa kilometa tatu hajalipwa, na hizi kilometa 40 kwa makadirio tunahitaji shilingi bilioni 100. Kwa hiyo, tatizo hapa ni fedha. Sasa yanakuja mapendekezo yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimalizie tu kwa kusema, watu wa Musoma Vijijini tumetangaziwa tender mara ya pili, hivyo tunaishukuru Serikali kwa hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yangu, na ndiyo maana ninachukua muda wa hawa wenzangu hapa. Kitu cha kwanza, barabara zetu tuzijenge kwa taratibu ambazo zinatumika pengine pote duniani. Ni lazima; ninaomba nisisitize, ni lazima Tume ya Mipango ihusike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi barabara siyo kila mtu anakuja tu na mipangilio yake. Hii mipango tuitunze kisheria. Kwa mfano, ni lazima tukubaliane kwamba tuunganishe mkoa kwa mkoa. Barabara zinazounganisha mkoa kwa mkoa mapendekezo yangu, ziwe ni mbili mpaka tatu. Zinaenda mbili au tatu, zinarudi mbili au tatu (lanes nne mpaka sita). Sasa hizi ziwepo kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Tume ya Mipango, ndiyo itaboresha hata matumizi ya fedha, tuunganishe wilaya kwa wilaya na penyewe ziwe zinaenda lanes mbili, zinarudi lanes mbili (lanes nne).

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, kuunganisha halmashauri zetu na makao makuu ya wilaya, ambapo zinaenda barabara mbili, zinarudi mbili. Kwa hiyo, hizo ni lanes nne. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo la pili ni matengenezo (road mantainence). Ndugu zangu fedha nyingi sana tunapotezea kwenye repair na maintenance. Sasa wataalamu, ndiyo maana nilichelewa kidogo mzee, nilikuwa nasubiria engineer mmoja anipe kitu kabla sijaja Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani ni kwamba usipofanya routine maintenance, inahitajika kati ya miaka mitatu mpaka mitano ile preventive lazima ifanyike. Halafu kuna periodic ambayo unaweka lami re-surfacing na sealing. Unaziba pale lami ili barabara isipokee maji. Hiyo ni kati ya miaka sita mpaka minane. Halafu barabara imeharibika kabisa, unahitaji rehabilitation re-construction. Hiyo ni kati ya miaka 15 mpaka 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya sisi hatuyafanyi haya, ndiyo maana gharama za ujenzi wa barabara zinakuwa kubwa, tunarudia mle mle. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa gharama za kutofanya matengenezo haya kwa wakati, ukidharau ikapita miaka mitatu, gharama zake zitakuwa mara sita kama ambavyo ungewahi. Ukiiacha miaka mitano, tena huyu ndio engineer wa mwisho ameniambia asubuhi; gharama zake zinaweza kwenda mara 18. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo la tatu. Vyanzo vya fedha. Kitu cha kwanza ni Bajeti ya Serikali. Bajeti yetu ndugu zangu za miradi ni shilingi trilioni 2.5, Mfuko wa Barabara umetoa shilingi trilioni 1.05, Mfuko wa Serikali umetoa shilingi bilioni 500 na fedha za nje zilikuwa shilingi bilioni karibu 920. Kwa hiyo, hicho ni chanzo cha kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo cha pili ni kutokana na rasilimali zetu; migodi… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, ninakuongezea dakika moja…

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, inabidi mnivumilie, haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachukua mfano zile kampuni zilizoingia mikataba, hata wengine hatujaingia huko Wizarani; mwaka 1995 bei ya dhahabu ounce moja ilikuwa dola 390. Miaka 30 baadaye, mwaka 2025 bei ya dhahabu ounce moja ilikuwa dola 4,000. Je, kwa nini tusitafute fedha kutokana na mikataba yetu ya madini hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni soft loans (mikopo laini). Hii inatoka IMF, World Bank na African Development Bank na nchi. Halafu hizi riba yake ni kati ya sifuri mpaka asilimia tatu, na grace period ni miaka mitano mpaka 10. Halafu repayment periods ni miaka 15 mpaka 45. Kwa hiyo, twende kwenye mikopo kama hii (soft loans). (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namba nne, sovereign wealth funds. Madini yetu na gesi yetu. Lazima tutunze fedha kama wanavyofanya Norway, na hizi fedha tutatumia sovereign bonds kuweza kupata mikopo. Duniani hapa anayeongoza mwenye mfano mzuri ni Norway ambaye ya kwake imefika shilingi trilioni 1.1 na juzi mwezi Aprili, 2026 Canada wameanzisha kama hii, na tayari wamewekeza dola bilioni 25. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni PPPs (Public Private Partnership). Hii ni sawasawa kama Barabara ya Kigamboni. Mwisho, ninamalizia, ni kwamba infrastructure investments mifano mingine duniani, na hii ni muhimu sana ulisikilize hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza, China wanatumia asilimia tano nukta tano ya pato lao la Taifa kwenye investments za infrastructure. India ni asilimia tano mpaka sita, Vietnam asilimia karibu sita, Seychelles ambayo ni nchi tajiri Barani Afrika inatumia asilimia sita, Mauritius ambayo inafuata kwa utajiri, inatumia karibu asilimia nne ya GDP yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninamalizia kwa kusema kwamba, hii bajeti tunayoiongelea kama na sisi tungeiga nchi nyingine tukatumia asilimia tano of our GDP, GDP yetu sasa hivi ni dola bilioni 95, five percent of 95 billion US dollars ni dola bilioni 4.75 ambayo ni sawasawa na shilingi trilioni 12.35…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante sana…

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa hivi tulikuwa tunapaswa kujadili bajeti ya shilingi trilioni 12, siyo ya shilingi trilioni mbili. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Profesa.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)