Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru na mimi kwa kunipatia nafasi ya kuweza kutoa mchango wangu kwa Bajeti ya Kumi na Moja ndani ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu nimeingia Bungeni mwaka 2015 na Bajeti yangu ya kwanza ilikuwa ya mwaka 2016, nilisimama kuzungumzia barabara ya kutoka Tanga – Kibirashi – Handeni – Kiteto – Chemba – Kwa Mtoro Singida. Mimi barabara hii kila Bajeti nimekuwa nikiichangia, lakini kipekee niwashukuru sana Wahehsimiwa Wabunge wa Bunge hili la Kumi na Tatu, wameona kilio change, na wameamua kunishika mkono kuhusiana na hii barabara, ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii siyo tu Mheshimiwa Kunti anaisema, barabara hii imeandikwa kwenye vitabu vya Serikali miaka na miaka. Tunavyozungumza, huu ni mwaka wa 26 iko kwenye vitabu vya bajeti, inaandikwa kila leo. Wanachokifanya Serikali, mnabadilisha tu maneno; la mbele linakuja katikati, la katikati linaenda nyuma, la nyuma linaenda mbele; ni maneno wanatugeuzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeuliza maswali zaidi ya 30 ya barabara hii. Bajeti ya mwisho tulipokuwa tunahitimisha Bunge la Kumi na Mbili mwaka 2025, Serikali ilituambia kwa maana ya Wizara kwamba tumetoka kwenye EPC + F tunakwenda kwenye PPP, na tukaambiwa kwenye PPP tunakwenda kuchukua wenzetu na Wizara ya Uchukuzi, kwa maana ya Taasisi ya Serikali, TPA, watakwenda kujenga ile barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya mwisho wakati Mheshimiwa Waziri anahitimisha, na swali langu nililowauliza mwezi huu wa Tano, nimejibiwa kwamba mazungumzo bado yanaendelea. Nikawa ninajaribu kujiuliza, kama sisi tu ndani ya nchi mazungumzo yanakaa zaidi ya miaka mitatu, nini sababu inayofanya Serikali washindwe kukubaliana? Serikali moja, nchi moja? Ni kitu gani kinachokwamisha hayo mazungumzo ili wananchi hawa waweze kupata huduma ya barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ndiyo inayopeleka wanawake kwenda hospitalini kuongeza viongozi wa kesho ndani ya Taifa letu. Wanawake wa Wilaya ya Chemba wanafia njiani kwa sababu ya barabara hii. Mvua inaponyesha, Mto Songolo hakuna mwanamke anayeenda kujifungua akavuka kwenye ule mto. Ukija Goima, na kwa mvua za mwaka huu daraja limekatika pale, watu wamekaa siku tatu hawana njia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatamani Serikali ikija ituambie na kwenye bajeti kitabu cha Waziri, imetengwa shilingi bilioni nane. Nikawa najaribu kutafakari, hivi shilingi bilioni nane inaenda kujenga barabara ipi? Hizo kilometa 20 ambazo tumeanza kuimbiwa miaka na miaka haziishi. Kila kitabu, kila bajeti inayokuja tunakutana na kilometa 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama imeshindikana ujenzi wa hii barabara, siyo vibaya tukaambiwa kwamba jamani barabara hii imeshindikana, kuliko kuwa tunawekwa, wanatupa matumaini kila mwaka lakini barabara haijengwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao Mto Bubu ambao unapita kwenye Daraja la Bubutole, umeua zaidi ya watu wanne. Barabara hii ikijengwa, wananchi wangu hawatakufa, Serikali watuonee huruma. Sisi Uchumi wa Wilaya ya Chemba barabara hii ikijengwa ndiyo hatima ya ukusanyaji wa mapato na kujitegemea kwa halmashauri na kusukuma maendeleo kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapolia na barabara hii, hatutamani tu rangi ya barabara ibadilike, bali tunatamani maendeleo ya wananchi wetu yaweze kusonga mbele. Ninatamani Serikali ikija, Waziri wa Ujenzi, kaka yangu Mheshimiwa Ulega anafanya kazi kubwa ya kumsaidia Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais alipokuwa ziara Tanga alitoa maelekezo kuhusiana na hii barabara, kwamba barabara hii iende ikajengwe ili tuweze kusaidia mizigo ya kutoka Bandari ya Tanga inayokwenda nchi za jirani ipite ile mizigo kwenye barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachelewesha uchumi wa nchi hii kukua. Twendeni tukafungue milango, tujengeni hiyo barabara. Mheshimiwa Ulega akija atuambie ni lini wanakamilisha mazungumzo na TPA ili barabara ya kutoka Handeni – Kibirashi – Tanga – Kiteto – Chemba mpaka Kwa Mtoro – Singida inakwenda kuanza kujengwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili ni Ujenzi wa Daraja la Kelemasimba. Daraja hili limekaa zaidi ya miaka 15, bovu limekatika. Kibaya zaidi barabara hii ilisainiwa mkataba mwaka 2022, limekaa mpaka leo mkandarasi akaamua ku-terminate mkataba kwa sababu tu ya kukosa fedha kwa ajili ya kwenda kujenga lile daraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2025 niliongea nikawaambia Mawaziri, mmekuwa mkienda mnabeba na mbuzi za watu, mnakula; hii ni laana. Huwezi kwenda kuwapa wakina mama wa watu wamejinyima, wamekupa Zawadi, wameona matumaini, unawaambia tunakuja kujenga daraja, halafu matokeo yake watu wanaendelea kufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kule hatuna vyombo vya Habari. Tungekuwa mjini, mngeona wananchi wetu wanavyokufa. Vyombo vingekuwa vinarekodi, mngeona namna watu wanavyokufa kwa ajili ya hizi barabara. Ninaomba Serikali ikija iniambie kuhusu daraja la Kelemasimba ambalo nimeimba miaka yote. Tunaona raha gani kwenda na bahasha za kutoa rambirambi wakati tulikuwa na uwezo wa kuhakikisha kwamba tunawatengenezea mazingira rafiki wananchi wetu na kuokoa maisha ya Watanzania?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa muda wako. (Makofi)