Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Mwantumu Mzamili Zodo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Jana nilisikiliza vizuri sana hotuba ya Mheshimiwa Waziri pamoja na Taarifa ile ya Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya yote, ninaomba kuunga mkono hoja ili nisije nikasahau mwishoni. Kwa sababu ya muda ninaomba niende moja kwa moja kwenye barabara zetu. Sisi wananchi wa Mkoa wa Tanga kwa majimbo yote 12, kipaumbele chetu cha kwanza ni barabara ya Handeni – Kibirashi – Chemba – Singida. Kwanza, barabara hii ni ya kimkakati kwa sababu inaenda kupunguza jam ya malori yanayotoka bandarini kuja kwenye mikoa mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni ya uzalishaji. Sisi katika Mkoa wetu wa Tanga, tunapata chakula kutoka Wilaya ya Kilindi na Handeni ambako ndiko barabara hii inakopita. Kwenye Taarifa ya Kamati walieleza kwamba wenzetu wa PPP wameonesha nia ya kutaka kuijenga barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Wizara, wakae na wenzetu wale wa PPP kujaribu kuangalia namna gani watajenga barabara hii. Barabara hii ni kilio cha wananchi wa mikoa takribani minne; Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Singida, Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni kilio cha viongozi wa dini. Ni juzi tu Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa na ziara na pale Chemba alifanya mkutano; na Shehe wa pale alipewa kufungua mkutano pale kwa dua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kujua barabara hii ni kilio cha watu wengi, baada ya dua Shehe alithubutu kuomba barabara hii kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Barabara hii ni kilio cha Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Madiwani. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja zake, kipaumbele cha kwanza kwa mkoa wetu wa Tanga iwe ni barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya pili ni Barabara yetu ya Tanga – Segera – Chalinze. Wote tunafahamu bandari imepanuliwa, na sasa hivi malori ni mengi, na barabara ile imezidiwa. Barabara ile ni chakavu, Barabara ya Tanga – Chalinze ina viraka barabara yote, kuanzia mwanzo mpaka mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri, nilimsikia akieleza kwamba wanakwenda kutanua kwa njia nne, lakini sasa alieleza kutoka Chalinze mpaka Segera kuelekea Arusha, hakueleza nini watafanya kutoka Tanga – Segera.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja, atueleze mkakati uliopo na ndugu yangu hapa Mheshimiwa Eng. Ulenge ameuliza swali hilo asubuhi hii. Ni mkakati gani watafanya kuendelea kuondoa ile jam kutoka Tanga mpaka Segera? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo, kuna barabara yetu inayotoka Handeni – Mzia – Turiani. Barabara hii imeelezwa na Ilani zaidi ya moja na barabara hii ilishaanza kwa kipande cha pale Magole – Turiani lakini ikaishia hapo, imesimama. Hatuelewi ni nini hatma ya kipande hiki cha kutoka Turiani – Mziha – Handeni kipande cha kilometa 108.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Taarifa ya Mheshimiwa Waziri, tumeona imetengewa shilingi milioni 500, kilometa 108. Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie, ni upi mkakati wa barabara hii ambacho kipande cha kwanza awamu ya kwanza kilishaanza na ni muda mrefu, je, upi mkakati wao wa kwenda kumalizia hiki kipande cha pili? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo barabara yetu ya kutoka Mabokweni – Maramba – Old Korogwe, inaenda mpaka kule Mlalo kwa ndugu yangu Mheshimiwa Shangazi. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, tumepewa kilometa 10, barabara hii ina kilometa zaidi ya 127. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake, atueleze hatma ya barabara hii ambayo ni kilio cha muda mrefu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana, ahsante.