Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Bukene na nitumie muda huu kushukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na uchache wa muda, naomba nijielekeze kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ukurasa wake wa 90 na ukurasa wa 99, amezungumzia barabara mbili za Jimbo la Bukene ambazo ni barabara ya Nzega – Itobo – Kagongwa na barabara ya kutoka Tabora – Mambali – Bukene – Itobo. Pia ametenga fedha shilingi milioni 800 na shilingi milioni 500 kwa ajili ya maandalizi kuelekea ujenzi wa lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana watu wa Bukene, lakini fedha hizo shilingi milioni 800 hazitoshi. Shilingi milioni 500 kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa barabara hizo hazitoshi na hitaji letu kwa sasa wananchi wa Jimbo la Bukene ni barabara ya kutoka Nzega – Itobo – Bukene ili barabara hiyo sasa ikatuunganishe na mradi mama mkubwa wa SGR unaoendelea kujengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Wizara ya Uchukuzi, SGR inatarajia kukamilika eneo hilo mwaka 2028. SGR hiyo tutaitumia wananchi wa Wilaya ya Nzega na Wilaya ya Igunga ambao Wilaya mbili zote hizo zina Majimbo Matano. Wananchi wa Nzega na Igunga ni wakulima wakubwa sana, tunazalisha mpunga, pamba, tumbaku na tunazalisha mazao mbalimbali. Pia, tunazalisha matunda aina ya maembe ambayo mara nyingi huwa tunauza katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ukamilishaji wa barabara hiyo itatusaidia kusafirisha mazao hayo kuelekea kwenye mradi wa SGR ili tuweze kufanikisha usafirishaji wa mazao hayo kuelekea mikoa mbalimbali hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii nimeipitia, lakini barabara za vijijini ni barabara ambazo zina changamoto kubwa sana kwa sababu zimejengwa kwa kiwango cha changarawe na ukarabati wa barabara hizo Serikali inatumia gharama kubwa sana. Kwa mfano, barabara ya kutoka Nzega – Itobo – Mambali na kutoka Itobo – Kagongwa, mwaka huu tu wa fedha uliomalizika tumetumia zaidi ya shilingi milioni 800 kuzikarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukinunua vifaa vya ukarabati ambavyo ni grader, roller, excavator, pamoja na tipper angalau mbili, tuna uwezo wa kutumia shilingi bilioni 1,449. Sasa ukija kuangalia, ununuzi wa vifaa ni shilingi bilioni 1.449, lakini ukarabati tu kwa mwaka mmoja tumetumia shilingi milioni 800. Kwa hiyo, ni afadhali Serikali ijikite kwenye ununuzi wa vifaa vya ukarabati wa barabara zetu za vijijini kwenye kila halmashauri ili tuweze kupunguza gharama na tuweze kutimiza lengo letu la kuhudumia wananchi wetu katika barabara za kiwango.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kuangalia nchi yetu hii ina halmashauri takribani 184. Halmashauri 184 ukizidisha kwa shilingi bilioni 1.449, unapata shilingi bilioni 266.6. Fedha hizi, shilingi bilioni 266 zinaweka zikawa mwarobaini wa kuleta suluhisho la kudumu kwenye changamoto za barabara tulizonazo kwenye majimbo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaishauri sana Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI kupitia TARURA, wanunue vifaa vya ujenzi kwenye kila halmashauri ili tuwe tunaweka diesel kwenye vifaa hivyo na kusaidia kujenga barabara zetu kwa gharama nafuu kuliko ambavyo iko kwa sasa hivi tumejikita kwenye utumiaji wa kandarasi. Tunatumia fedha nyingi kuwalipa wakandarasi na wakandarasi hao wanaweka riba kubwa matokeo yake kila mwaka tunakuwa na lawama juu ya barabara hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya sana ukija kuangalia, nchi yetu ina uhitaji mkubwa wa barabara, ndiyo maana ukiangalia asubuhi hapa maswali mengi kwa TAMISEMI yanahusu barabara, maswali mengi pia yanahusu TANROADS, na maswali mengine huwa yanahusu Wizara ya Maji. Kwa hiyo, ukija kuangalia, hitaji kubwa la Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa nchi hii, ni barabara; na barabara ni uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kujua kwamba usafirishaji ndiyo uchumi pekee, angalia juzi ilivyotokea hapo Iran, wamefunga ule mfereji wa Hormuz, mafuta yamepanda kila mahali duniani. Hata sisi wananchi tunaoishi kule vijijini, barabara zinapokatika wakati wa masika ama wakati wa kiangazi tunapata tabu kubwa sana katika usafirishaji wa mazao yetu na usafirishaji wa abiria.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa muda wako umeisha, ninaomba umalizie.
MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba kumalizia kwa kuiomba Wizara ya Ujenzi, wanapokuja kutoa mrejesho wa mwisho, watueleze, kama hawajatenga fedha za ujenzi wa Barabara ya Nzega – Itobo – Bukene, watueleze alternative barabara tutakayoitumia sisi watu wa Igunga na Wilaya ya Nzega kuelekea kwenye SGR pale itakapokamilika.