Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia kuwa na afya njema na kuwa tayari kulitumikia Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia tangu asubuhi ambapo tumepata wachangiaji 30; ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Kamati yetu na ninaomba kuahidi kwamba hoja zote 11 za Kamati kama zilivyoonekana katika michango ya Wabunge tutazizingatia. Mimi sina mengi zaidi ya ufafanuzi mfupi tu wa jumla na ninaahidi kwamba hoja zote za Wabunge na za Kamati tutazifafanua zote kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza ya jumla inahusu dhana ya ujamaa ambayo imejitokeza humu ndani. Ujamaa ni imani na mimi ujamaa wangu na wenzangu siyo wa cheo ni wa imani. Misingi ya ujamaa ni kuhakikisha kwamba watu wote mnaishi pamoja kwa kushirikiana, lakini pia mnachapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mheshimiwa Rais aliomba kura kwa kauli mbiu ya Kazi na Utu, Tunasonga Mbele. Sitaki kuingiza mjadala kuhusu ujamaa upi na ujamaa wa aina gani kama nilivyosema tukubalie tu kwamba ujamaa ni imani. Ahsanteni sana kwa wale ambao wameanzisha mjadala huu kwa sababu msingi wake ni Katiba ya Nchi na ni Katiba ya Chama Cha Mapinduzi. Kwa sababu hiyo, ninaomba nigusie mambo machache yaliyojitokeza katika mjadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni kuhusu uanzishwaji wa Mamlaka ya Uvuvi. Waheshimiwa Wabunge wengi wameshauri kwamba tunahitaji chombo madhubuti kitakachosaidia kusimamia rasilimali za uvuvi na kuhakikisha kwamba uvuvi unaofanyika unazingatia sheria. Jambo hili tumeshalifikisha mahali ambapo lipo katika hatua za maamuzi na tuna hakika kabisa chombo hiki kitatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa uvuvi haramu; uvuvi unaoendelea bila kufuata sheria lazima tuudhibiti na hatutachoka. Ninadhani Wabunge wote ambao wanaishi katika maeneo ya maziwa wanatoa ushuhuda ambao unaonyesha kabisa kwamba kazi kubwa inatakiwa kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais kuhusu Bandari ya Uvuvi ya Kilwa na Bandari itakayojengwa Bagamoyo. Ninawapongeza Wabunge wote ambao wamempongeza Mheshimiwa Rais kwa kutambua kazi kubwa anayoifanya. Hata kupongeza na kutambua nafasi ya Mheshimiwa Rais siyo jambo dogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukuzaji wa viumbe maji; limetajwa hapa na Mheshimiwa Mbunge wa Mwibara na mimi nakubaliana na wewe kabisa kwamba hatuwezi tukafanya uvuvi wa vizimba kiholela. Ninadhani ndicho alichokuwa anakizungumza. Lazima tuzingatie taratibu na taratibu zipo na tusipokuwa makini kila mmoja akawa anaweka kizimba mahali fulani tutachafua maziwa yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wageni ambao wamewekeza katika ufugaji wa vizimba; lazima tuzingatie maslahi ya wavuvi wadogo na wafugaji wadogo ikiwemo kuhakikisha kwamba wanawekeza mitaji mikubwa katika teknolojia na viwanda vya chakula, kwa sababu tatizo kubwa tulilonalo katika eneo hili siyo maarifa ya watu, siyo utayari wa watu, siyo nguvu kazi ya watu isipokuwa tunalo tatizo la upatikanaji wa chakula cha samaki na upatikanaji wa vifaranga vya samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli baada ya kutatua matatizo hayo, wafugaji kwa vizimba wa kawaida wadogo wadogo wanaweza wakatoa mchango mkubwa bila kuhangaika kuleta wafugaji ambao wanaweza wakawa na mitaji inayofanana na Watanzania ambao wanashughulika na ufugaji wa samaki kwa vizimba. Kwa hiyo, ninadhani hayo malalamiko ambayo yapo tutayafanyia kazi na tutazingatia taratibu za ufugaji zinazozingatia sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe watu wasiweke vizimba kwenye maji bila kufuata utaratibu. Ni muhimu sana tuzingatie utaratibu na utaratibu huo upo. Ninakiri kwamba bado tuna tatizo la chakula cha samaki na tuna viwanda vichache (tuna viwanda viwili tu peke yake sasa hivi). Tunawahimiza wawekezaji waweze kuongeza viwanda vingi vya samaki kwa ajili ya chakula cha samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto zilizotajwa kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima. Hapa nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ziara alizozifanya na matamko na ufafanuzi alioufanya. Hata leo asubuhi kajibu swali la aina hiyo hiyo, lakini niwakumbushe Hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo ndiyo ilitumika kufungua Bunge la Kumi na Tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ametuelekeza tuwe wasikivu kwa wananchi. Tusikie shida zao na tuwajibike kwao na kwa kauli yake amesema wasiposikilizwa wananchi na tusipowajibika kwa wananchi, basi tuwe tayari yeye kutubadilisha. Pia, nimeshasema Bungeni hapa na ninarudia sipo tayari kuwa sehemu ya watu ambao Mheshimiwa Rais atawabadilikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limejitokeza katika Hotuba na katika mijadala linahusu masuala ya chanjo na utambuzi wa mifugo. Katika mambo ambayo Mheshimiwa Rais atakumbukwa kwa maarifa yake, kwa utashi wake wa kisiasa, kwa ubunifu wake katika Sekta ya Mifugo, ni suala la chanjo na utambuzi wa mifugo. Hili ni jambo kubwa sana katika historia ya uongozi wa Taifa letu na hapa niwapongeze wafugaji kwa kuelimishana na kuwa tayari kushiriki katika zoezi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kufafanua ni kwamba zoezi hili ni la miaka mitano kule ambako hatujafika wasidhani tumemaliza au tumewaacha. Kama Wabunge wameangalia bajeti tuliyoitenga, tumetenga pesa kwa mwaka unaofuata na hii kampeni imezinduliwa mwaka jana, lakini mapokeo yamekuwa makubwa kuliko tulivyotarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye eneo la utambuzi wa mifugo, mapokeo yamekuwa mazuri kuliko ilivyozoeleka huko nyuma. Kwa hiyo, kwa niaba ya Mheshimiwa Rais ninawashukuru sana wafugaji wa Tanzania kwa kupokea hiyo kampeni kwa mikono miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanikiwa ndani ya miaka mitano tutatatua matatizo makubwa mengi sana na hasa upatikanaji wa masoko nje ya nchi, lakini pia kupunguza gharama za ufugaji kwa wafugaji. Kwa hiyo, hili ni jambo kubwa katika sekta ya mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine lililosemwa ni la kufunga Ziwa kwa watu wa Tanganyika. Ninadhani hao nikikaa bila kulifafanua hili hatutaelewana. Ninawashukuru sana kwamba wanafuatilia na wameleta hoja za wananchi hapa na kama nilivyosema Mheshimiwa Rais ametuagiza Mawaziri wote tusikilize wananchi. Sasa ninasema hapa mbele yenu kwamba tuko katika hatua ya kufanya tathmini na hatutafunga Ziwa bila kuzingatia maoni ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe kabisa kwamba pamoja na Wizara yetu ya kisekta ya kushughulikia jambo hili, lakini Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira ndiyo kinara wa masuala ya mazingira. Kwa hiyo, Wizara yangu na Ofisi ya Makamu wa Rais tunafanya tathmini baada ya jaribio la miaka mitatu kukamilika mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, uamuzi wowote tutakaoufanya utazingatia tathmini tutakayoifanya na kwa kalenda ilibidi tufunge kuanzia kesho. Kwa sababu kwa utaratibu kwa miaka mitatu iliyopita tulikuwa tunafunga kila tarehe 15 mwezi Mei hadi tarehe 15 mwezi Agosti. Kwa hiyo, niwaombe Wabunge wa Kigoma, Katavi pamoja na Rukwa tusiondoke Bungeni bila kukutana na kushauriana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo haimaanishi kabisa kwamba utaratibu wa kufunga hautakuwepo. Kwanza ni wa kisayansi, lakini pili ni makubaliano ya sisi nchi nne tunaotumia Ziwa pamoja. Tulichokubaliana ni kwamba lazima tufanye tathmini kwanza ya matokeo ya miaka mitatu ya majaribio tuliyoyafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; makubaliano mapya tutakayoyafanya yazingatie maoni ya wananchi na mahitaji ya nchi pamoja na makubaliano ya sisi watumiaji wa Ziwa hilo. Kwa hiyo, Wabunge wawaondoe wasiwasi wavuvi wa Tanganyika kwamba tunawasikiliza na hatutafanya uamuzi wowote bila kuzingatia maoni yao ambayo yamewasilishwa vizuri hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi kusikia kabisa kwamba pamoja na kufunga au kutofunga maziwa yetu hayana samaki. Kwa hiyo maziwa yameshajifunga yenyewe hivyo, kazi yangu mimi ya kujibu suala la kufunga na kutofunga kwa kweli ni rahisi kwa sababu tumeshayafunga wenyewe kwa kuvua kiharamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshasema sehemu nyingine na ninasema hapa mbele yako; mimi siyo Waziri wa Maji, Waziri wa Maji ni Mheshimiwa Aweso. Mimi ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, sitakubali maji ambayo yanatakiwa yawe na samaki yasiwe na samaki. Maana yake ni sawa na kukataa kazi na mimi kazi hii ninaipenda sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wale ambao wanaendesha uvuvi usiozingatia sheria hakuna funika kombe mwanaharamu apite, tutapambana bega kwa bega na mimi nina mbinu nyingi kwa sababu ni shabiki wa Yanga. Kufunga magoli na kuyashangilia hilo si tatizo na hapa hakuna masihara. Tunao utashi wa kisiasa na maelekezo mahususi ya Mheshimiwa Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linaenda sambamba na wageni kuingia ndani kiholela na kuanza kuhatarisha usalama katika maeneo yetu ya uzalishaji. Tayari tumeanza mazungumzo kupitia kwa Chief Whip na sekta zote zinazohusika kuhakikisha kwamba maziwa yetu yote yanakuwa salama, mipaka yetu yote inakuwa salama, wafugaji na wavuvi wote na wakulima na Watanzania wote wanafanya shughuli zao kwa usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda siyo mrefu wataanza kuona mabadiliko. Ninachowaomba Waheshimiwa Wabunge tupewe ushirikiano wa kutosha. Tuleteeni taarifa sahihi tuchukue hatua inavyotakiwa. Hili nilitaka nilifafanue kusudi tuweze kuelewana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wabunge wanaotoka kwenye maeneo ya ufugaji mimi sina tatizo kukutana nao, lakini ninachotaka kusisitiza; sitaki tuwe Wabunge wa wafugaji kwa kujiandaa kutengeneza uhasama na wakulima au tuwe Wabunge wa kuwakilisha wakulima kwa kutengeneza uhasama dhidi ya wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge wa Mvomero kwa kuitaja Kampeni ya Tutunzane. Hii ni kampeni ilizinduliwa na Mheshimiwa Rais, ushahidi upo Mheshimiwa Rais ametuelekeza, sisi ni Taifa moja lazima tuishi kwa kupendana na kwa kufuata sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makosa ya wafugaji wawili au watatu wanaorusha mishale yasiwe makosa ya wafugaji wote. Tuwasake na tuwapeleke mbele ya mkono wa sheria. Kwa hiyo, ninawaomba na Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshasema mara nyingi, tunashindana kutumia ardhi ambayo haiongezeki, lakini sisi tunaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maekezo ya Ilani ni kupima ardhi ya wafugaji, baada ya kuipima kuirasimisha, kuilinda kisheria na kuweka huduma ambazo zinahitajika kusudi wafugaji waweze kutumia ardhi bila kupambana au kugombana na wenzao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kuna Mbunge mmoja hapa amesema, sasa hivi ufugaji na uvuvi hauna tena kanda au maeneo. Kwa ufugaji wa samaki sasa hivi unaweza ukafuga mpaka nyumbani kwako kwa teknolojia iliyopo, vivyo hivyo hata kwa mifugo. Kama tunakubaliana kwamba nchi hii ni ya kijamaa, lakini nchi hii kiuchumi ni ya kilimo na kilimo maana yake ni kilimo cha mazao, ni ufugaji, ni uvuvi, ni misitu, ni pamoja na nyuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna dira yetu inavyosema, mabadiliko yoyote ya kiuchumi roho yake kubwa itakuwa ni Sekta ya Kilimo na huo ndiyo ukweli. Viwanda vingi vitatokana na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi na kwa maana hiyo ajira nyingi zitatokana na sekta hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunao wajibu kama viongozi na kama Watanzania kushirikiana kugawana rasilimali zilizopo, kuhakikisha wote tunatumia kukuza uzalishaji. Matatizo makubwa tuliyonayo katika mifugo kama walivyosema ni malisho, ni huduma za afya ya mifugo, ni miundombinu wezeshi ya maji, halafu ni mipango mizuri ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya hayawezi yakafanywa na Sekta ya Mifugo peke yake, ukisikiliza hotuba ya Waziri wa miundombinu ya barabara atagusa maeneo ya kukuza sekta hizo. Jana Wabunge wamesikia tulikuwa na Waziri wa Uchukuzi, hivyo viwanja vya ndege vinavyojengwa vinahitaji viwe na mifumo ya baridi kusudi nyama ziweze kupitia kwenye viwanja hivyo kusafirishwa nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya Mheshimiwa Rais lazima sekta zote zishirikiane zifungamanishwe na Wizara tushirikiane na haya ndiyo makubaliano tuliyonayo. Tume ya Umwagiliaji itafanya kazi ya kuhakikisha kabisa kwamba inaweka miundombinu ya umwagiliaji kwa Sekta nzima ya Mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema Mwenyekiti wa Kamati ya Maji na Mazingira. Wizara ya Maji kwa mpango kabambe wa Gridi ya Maji ya Taifa, malengo yake ni kuhakikisha kwamba gridi hiyo inakuwa inasaidia watumiaji wote wa maji. Kwa hiyo, ninawahakikishia, badala ya kuanza kulaumiana na kulalamika, tuanze kushirikiana kwa sababu utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa, miaka 25 ijayo itategemea tulivyokubaliana katika namna ya kujenga sekta hizo za uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, Mheshimiwa Dkt. Mollel, alitoa hoja yake hapa nami nimemwahidi kwamba nitakwenda kufanya ziara. Baada ya Bunge nitakwenda kufanya ziara katika maeneo ambayo yana changamoto zinazojulikana ambazo ni tete.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo kwa upande wa mifugo nilipokwenda Ruvuma – Tunduru, baada ya kutumwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, nilikuta kuna matatizo Ruvuma, kuna matatizo Mtwara, kuna matatizo Lindi, Pwani, Kilimanjaro na Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninamwomba Mwenyezi Mungu anipe afya, nitafika huko tushauriane. Nitakwenda kwa utulivu zaidi kusudi tuweze kutatua matatizo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, haya mambo tunayoyasema ni ya mpango wa miaka mitano ya ilani. Niko hapa kuwathibitishia Wabunge pamoja na Watanzania kwamba, mambo yote ambayo yameahidiwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kuhusu Sekta za Mifugo na Uvuvi yote yatatekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuruni sana na ninaomba kutoa hoja. (Makofi)