Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kabisa ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa utayari mkubwa ambao amekuwa akiuonesha, hususan katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na ustawi mkubwa sana wa watu kupitia sekta ya mifugo na uvuvi; kwa kweli Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri. Ndiyo maana unaweza kuona katika kipindi kifupi alichokaa madarakani, kuna mabadiliko makubwa sana kwenye sekta hii kupitia katika bajeti, utendaji kazi wake, lakini vilevile matokeo makubwa ambayo tumeyashuhudia ambayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeyatangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, mkubwa wetu, comrade Mheshimiwa Balozi Dkt. Bashiru. Ninafikiri wote hapa Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, ni mtu muadilifu ambaye anaifanya hii kazi kwa uzalendo mkubwa sana. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri; yeye pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara. Kwa kweli commitment inaonekana kwenye hii sekta na tutaona matokeo makubwa hivi karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ambayo ameisoma Waziri leo unaona kabisa imekusudia malengo makubwa ya kumsaidia mvuvi pamoja na mtu wa mifugo (mfugaji amepata nafuu kubwa). Vilevile, watu wa uvuvi wamepata nafuu kubwa. Nitaonyesha kama eneo moja, hapa unaona katika Serikali imefanya maboresho makubwa ya kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye vifaa na zana za uvuvi ili kupunguza gharama za uendeshaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msamaha huo umetolewa katika baadhi ya zana za uvuvi na malighafi hizo ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, utaona katika eneo la nyavu na nyuzi za kutengenezea nyavu, Serikali imeondoa msamaha wa kodi katika eneo hilo; engine za kupachika kwenye maboti, Serikali imeondoa kodi ya VAT katika eneo hilo; maboya, ndoano, vifungashio, boti (fibre boats) ambazo zimekuwa zikitumika na wavuvi, Serikali imeondoa kodi ya zuio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mitambo ya ubaridi, mitambo ya kuzalisha barafu, magari yenye ubaridi kwa ajili ya kubeba samaki na mazao ya samaki, Serikali imeondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ili kumsadia mkulima. Hayo ndiyo tunayoyasema kwamba unaona nia njema ya Mheshimiwa Rais kumsaidia mvuvi kuhakikisha kwamba tunaleta ustawi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali vilevile imepunguza gharama za leseni na tozo katika maeneo mbalimbali na nyingine zimejumuishwa ili kumpunguzia tu kero mvuvi katika eneo lake. Sasa hapo unaona kabisa ni nia njema ambayo Serikali imekusudia kusaidia Sekta ya Uvuvi, lakini vilevile na kwenda kusaidia sekta ya mifugo hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kwamba, kwa sasa hivi utaona kabisa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa maana ya Serikali imeruhusu matumizi ya leseni moja ya uvuvi katika eneo moja la maji tofauti na yalivyokuwa awali ambapo unakuta kila Halmashauri ilikuwa inatoa leseni yake. Sasa hivi ukishakuwa na leseni moja ya uvuvi katika eneo la maji utatumia hiyo hiyo leseni hata kama utakwenda katika eneo lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiyo yote ni kuhakikisha kwamba Serikali inamsaidia mvuvi katika kuhakikisha kwamba tunaboresha ustawi wa maisha yake. Kwa hiyo, bado Serikali itaendelea kuhamasisha uvuvi endelevu na uhifadhi wa mazingira na kuendelea kutoa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana katika moja ya jitihada kubwa ambazo Serikali imekuwa ikifanya ni kuhamasisha watu vilevile kujiunga na hii elimu kubwa ambayo imekuwa ikitolewa ya kuhakikisha kwamba uvuvi wa vizimba (fish caging) unaendelea na unafanyika ili kuhakikisha kwamba inapofika nyakati Serikali inasema jamani tunafunga Ziwa, lengo letu ni kuacha Ziwa lipumue ili baada ya msimu ule kupita samaki wamekuwa wamezaliana maana yake sasa watakaonufaika ni wavuvi wenyewe. Sasa haya yote ni Serikali imekuwa ikiyafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Mheshimiwa Dkt. Bashiru wamekuwa wakiyasimamia kwa vitendo. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge tumuunge mkono Mheshimiwa Dkt. Bashiru, Waziri wa Mifugo na Uvuvi kuipitisha bajeti yake, lakini vilevile kuhakikisha kwamba yale yote aliyoyazungumza tunamsaidia na tunayasukuma ili yaweze kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri ni mtu makini, ana uwezo, ana nia njema dhidi ya Taifa letu na hatuna shaka kwamba haya yote aliyoyazungumza yako ndani ya uwezo wake na ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, ninakushukuru kwa nafasi hii na ninaunga mkono hoja ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Ahsante sana. (Makofi)