Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Tinnar Andrew Chenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mapinduzi makubwa aliyoyafanya katika sekta ya mifugo na uvuvi na hasa kwenye utoaji wa chanjo ya mifugo, lakini pia kwenye eneo la uvuvi hasa kwenye uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia uzinduzi wa meli kubwa ya uvuvi katika bahari kuu tarehe 25/4/2026 yenye uwezo wa kuvua zaidi ya tani 48 kwa safari moja. Tumeshuhudia pia Miradi ya Vizimba vya Samaki katika Ziwa Victoria ambavyo vimetoa fursa ya ajira kwa baadhi ya vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ninatoka ukanda wa ziwa mchango wangu nitaulekeza kwenye Ziwa Victoria ili wilaya zinazozungukwa na Ziwa Victoria na hasa Wilaya ya Busega ambayo iko katika Mkoa wa Simiyu ziendane na wakati kuhusu uchumi wa bluu. Ninashauri tuanzishe pilot project katika Wilaya ya Busega ambayo itakuwa maalum kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mantiki hii ziwa letu liwekewe mipaka ya kisheria na kistratejia, ili kuwe na umbali maalum kuanzia nchi kavu kwenda ndani ya maji (kilomita tano mpaka ishirini) kadri itakavyoonekana inafaa kitaalamu) ambapo itakuwa ni marufuku kwa uvuvi wa kawaida wa nyavu. Kanda hii ijulikane kama “kanda tulivu ya mazalia”
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo hapa ni kutengeneza “benki ya samaki” ambapo ndani ya eneo hili lililotengwa haitaruhusiwa kufanyika shughuli zozote za uvuvi ili kuondoa usumbufu kwa mazalia ya samaki. Tukifanikiwa kufanya hivi tutatengeneza mazalia ya uhakika ya samaki kwani samaki watapata mazingira tulivu ya kuzaliana kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri pia kuwa, Wizara ije na mpango madhubuti ya kuzalisha vifaranga kisayansi na kisha kuvirudisha ziwani ili viendelee kuzaliana na kwa kuwa eneo hili litakuwa tulivu, ninaamini kabisa kuwa vitaendelea kuzaliana kwa wingi. Hapa isiwe kwa Busega tu bali maeneo yote yanayozungukwa na Ziwa Victoria ili kukabiliana na upungufu wa samaki kwenye ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo hili litafanikiwa na kuwa na samaki wa kutosha kwenye ziwa, ninashauri Wizara ije na mpango wa utalii wa uvuvi (fishing tourism) kama chanzo cha mapato kwa Wilaya ya Busega na kwa Serikali pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ikiwezekana kuwe na boti ndogo ndogo maalum kwa ajili ya fishing tourism na kwa kuwa Busega iko karibu pia na Mbuga ya Serengeti, tutangaze utalii huu ambapo watalii wataruhusiwa kukodi boti hizi na kupewa ndoano ili waingie ziwani na kuvua samaki in a traditional way na kila samaki atakayevuliwa na mtalii apimwe na kulipiwa ushuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndipo umuhimu wa kujenga Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Simiyu na ule wa Serengeti unapoingia, kwani kutafungua utalii kwa Kanda ya Ziwa na kukuza uchumi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na uvuvi haramu kwenye maeneo mengi ndani ya Ziwa Victoria na Serikali imechukua hatua kadhaa ikiwemo kuwakamata wavuvi haramu na kuharibu zana hizo. Niombe tusiishie hapo tu bali pia tuwachukulie hatua wafanyabiashara wanaouza nyavu hizi na mamlaka ambazo zimeruhusu zana hizi kuingizwa nchini. suala la uwajibikaji hapa ni muhimu sana maana tunatoa adhabu kwa mtumiaji na kumwacha muuzaji akiendelea kuuza zana hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.