Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Adonis Alfred Bitegeko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ADONIS A. BITEGEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta za mifugo na uvuvi. Ninawapongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Manaibu Katibu Wakuu na watumishi wote wa sekta ya mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta ya Mifugo ninashauri yafuatayo:

(i) Serikali iendelee kuvutia wawekezaji katika ufugaji wa mifugo wa kimkakati. Ninapongeza Serikali kwa kuingia mikataba na wawekezaji wanne wa kosafu bora za mifugo kwa nia ya ufugaji wa kitaifa wa kimkakati. Ninashauri Serikali iendelee kuvutia wawekezaji wakubwa wa kimkakati katika eneo hili ambao utaleta mageuzi makubwa katika kuongeza uzalishaji na tija wa mazao ya mifugo.

(ii) Uwekezaji katika vitalu vya NARCO uwe wa kisasa. Serikali iendelee kusimamia ili kuona uwekezaji katika vitalu vya NARCO unakuwa wa tija zaidi kwa kukodisha vitalu kwa wawekezaji wenye uwezo, watakaofuga kisasa.

(iii) Uhaba wa chanjo ya FMD katika Wilaya ya Muleba. Wilaya ya Muleba imekuwa na milipuko ya mara kwa mara ya ugonjwa wa miguu na mdomo ya mifugo kwa wanyama wenye kwato. Chanjo hiyo inapatikana katika sekta binafsi ambayo ni ghali katika sekta binafsi (Sh. 3,000 mpaka 3,500 kwa chupa). Tunaomba kuletewa chanjo ya FMD ya ruzuku.

(iv) Ukosefu wa dawa za kuogeshea mifugo katika Wilaya ya Muleba. Halmashauri ya Muleba imejitahidi kujenga na kukarabati majosho, lakini Wilaya ya Muleba ina ukosefu wa dawa za kuogeshea mifugo hasa za ruzuku.

(v) Uchache wa wataalamu wa mifugo katika Wilaya ya Muleba na pikipiki. Wilaya ya Muleba ina kata 43 na ina wataalamu wa mifugo 21. Tunaomba kuongezewa wataalamu wa mifugo. Halmashauri imepewa pikipiki 11 tu, tunaomba pikipiki nyingine kama Serikali ilivyoahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Uvuvi:-

(i) Raia wa kigeni kuingia katika visiwa na kununua dagaa na samaki badala kununua katika masoko. Serikali ifuatilie suala hili kwa kushirikisha vyombo vya dola ikiwemo Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Serikali ya Mitaa. Uvamizi huu umekuwa ukitokea katika Ziwa Victoria upande wa Wilaya ya Muleba hasa Visiwa vya Goziba, Kereba na Bumbire. Hii inarudisha nyuma jitihada za Serikali za kujenga uchumi wa wananchi wazawa.

(ii) Uvamizi wa wavuvi katika Ziwa Victoria unaofanywa na raia wa kigeni. Serikali ifuatilie uvamizi huu ikiwezekana kuunda kikosi kazi cha kufuatilia matukio kama haya pamoja na uvuvi haramu.

(iii) Ununuzi wa boti za doria kama Ilani ya Uchaguzi ya CCM inavyoelekeza. Tunaomba Serikali inunue boti tatu za doria kwa ajili ya Visiwa vya Goziba, Kereba na Bumbire.

(iv) Ukamilishaji wa soko la samaki na dagaa katika mwalo wa Kyamkwiwi, Kata ya Izigo, Muleba ambao umefikia 26%. Serikali ikamilishe soko hili ambalo limechukua muda mrefu kukalimika.